Mwanamama aliyegeuza, kuijenga upya taswira ya Sheria Tanzania

Dar es Salaam. Jaji wa kwanza mwanamke nchini na Afrika Mashariki, Julie Catherine Manning amefariki dunia leo Ijumaa, Machi 202, 2026 katika Hospitali ya Hitech Sai Healthcare Upanga jijini Dar es Salaam alikokuwa akipata matibabu.

Jaji Manning ambaye ni mstaafu aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 1973 hadi 1975 na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria.

Alikopita, alama zake Tanzania

Jina la Julie Manning linabaki kuwa alama ya mageuzi ya kina yaliyolenga kuifanya sheria iwe hai, jumuishi na inayoendana na uhalisia wa jamii ya Kitanzania.

Akiwa Waziri wa Sheria kati ya mwaka 1975 hadi 1983, Manning hakutosheka na hadhi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika nyadhifa za juu serikalini.

Badala yake, alitumia nafasi hiyo kama jukwaa la kuibadili mifumo iliyorithiwa kutoka enzi za ukoloni na kuijenga upya kwa misingi ya utaifa na haki za kijamii.

Kuzaliwa kwa Tume ya Marekebisho ya Sheria

Mojawapo ya mafanikio makubwa yaliyohusishwa na uongozi wake ni kuanzishwa kwa Tume ya Marekebisho ya Sheria mwaka 1980.

Kabla ya hatua hiyo, sheria nyingi zilikuwa zimepitwa na wakati na hazikuakisi mahitaji ya Tanzania huru.

Kupitia tume hiyo, Serikali ilianza safari ya kuchambua, kurekebisha na kuboresha sheria ili ziendane na maadili ya jamii, utamaduni wa Kitanzania na changamoto mpya za kijamii.

Hatua hiyo iliweka msingi wa maboresho yanayoendelea kushuhudiwa hadi sasa.

Kusimamia Utekelezaji wa Sheria ya Ndoa

Ingawa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ilitungwa kabla hajawa Waziri, Manning alijipambanua kwa kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa na tija kwa wananchi, hasa wanawake.

Alisisitiza haki ya mwanamke ndani ya ndoa, ikiwemo umiliki wa mali na ulinzi dhidi ya ukatili.

Aidha, alitoa msukumo mkubwa katika kuhakikisha ridhaa ya mwanamke inakuwa sharti muhimu kabla ya ndoa kufungwa, hatua iliyobadili mitazamo ya kijamii na kisheria kwa kiasi kikubwa.

Kuifanya sheria kuwa ya Kitanzania

Katika juhudi za kuondoa utegemezi wa wataalamu wa kigeni, Manning aliongoza mchakato wa “Africanization” ya mfumo wa sheria.

Alihimiza mafunzo na ajira kwa wanasheria wazalendo, jambo lililosaidia kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa ndani.

Pia, alihamasisha matumizi ya Kiswahili katika baadhi ya ngazi za mahakama, hatua iliyoongeza uwazi na uelewa kwa wananchi wa kawaida waliokuwa wakihudhuria kesi mahakamani.

Kulinda haki za watoto, familia

Katika kipindi chake cha uongozi, jitihada zilielekezwa pia katika kulinda makundi yaliyo hatarini, hususan watoto.

Marekebisho ya sheria yalihakikisha watoto waliozaliwa nje ya ndoa wanapata haki ya matunzo, jambo lililokuwa hatua muhimu katika kujenga jamii yenye usawa zaidi.

Pia, alifungua milango kwa wanawake akilenga zaidi mageuzi ya kisheria, Manning alifanya mapinduzi ya kimtazamo ndani ya mfumo wa mahakama.

Akiwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi za juu za utoaji haki, alivunja dhana kuwa wanawake hawawezi kushughulikia kesi nzito.

Ufanisi wake ulihamasisha uteuzi wa wanawake wengi zaidi katika nafasi za juu za kimahakama kama ambavyo imetokea kwenye miaka ya karibuni.