Ofisa wa benki ahukumiwa kulipa Sh152 milioni kwa wizi

‎Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu aliyekuwa ofisa wa benki ya Equity Tanzania Limited, Lilian Koka (27), kulipa fidia ya Sh152 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la wizi.

Mbali na adhabu hiyo, Koka ambaye ni mkazi wa Ukonga, amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12, akitakiwa kutotenda kosa lolote la jinai katika kipindi hicho.

Hukumu hiyo ilitolewa Machi 19, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Franco Kiswaga kufuatia mshtakiwa huyo kuingia majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kukubali kukiri kosa ili kumaliza kesi dhidi yake.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tayari Koka amelipa Sh76 milioni na anatakiwa kulipa kiasi kilichobaki cha Sh76 milioni ndani ya miezi 12 tangu kusainiwa kwa mkataba huo.

Aidha, ameweka dhamana ya hati ya nyumba yenye thamani ya Sh300 milioni iliyopo Bunju, ambayo itataifishwa endapo atashindwa kukamilisha malipo ya fedha zilizobaki.

Akitoa hukumu, Hakimu Kiswaga alisema amezingatia makubaliano kati ya mshtakiwa na DPP pamoja na hoja za utetezi zilizowasilishwa kupitia wakili wake, Godian Magusa.

“Mahakama imekutiwa hatiani kwa kosa la kuiba kama ulivyoshtakiwa, hivyo inakuhukumu kifungo cha miezi 12 cha kutotenda kosa lolote la jinai ndani ya kipindi hicho,” alisema Hakimu Kiswaga.

Aliongeza kuwa mshtakiwa anatakiwa kuzingatia masharti ya makubaliano na kukamilisha malipo ya fedha zilizobaki kwa wakati, akionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kutasababisha kufutwa kwa mkataba na kurejeshwa mahakamani kuendelea na kesi.

Awali, Wakili wa Serikali Mkuu, Karen Mrango akishirikiana na Ignas Mwinuka, alieleza kuwa upande wa Jamhuri hauna kumbukumbu ya makosa ya awali dhidi ya mshtakiwa, hivyo waliomba mahakama itoe adhabu kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa.

Mrango alibainisha kuwa awali mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka mengi, lakini baada ya majadiliano na DPP, mashtaka hayo yalipunguzwa na kubaki shtaka moja la wizi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025 katika makao makuu ya benki ya Equity Tanzania Limited, Ilala, Koka aliiba Sh152 milioni zilizokuwa katika akaunti ya ‘clearing and settlement’ iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mali ya benki hiyo.

Ilidaiwa kuwa fedha hizo alizihamisha na kuziweka katika akaunti mbalimbali za watu wasiokuwa wafanyabiashara.

Uchunguzi uliofanyika baada ya tukio hilo uliibua tuhuma hizo, ambapo mshtakiwa alikiri kosa lake mahakamani baada ya kufanyika kwa majadiliano na DPP.

Koka ni miongoni mwa washtakiwa tisa katika kesi ya uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025 yenye mashtaka 20, ikiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa njia ya udanganyifu, mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.

Kesi hiyo bado ipo katika hatua ya kutajwa, huku washtakiwa wengine wakiendelea na majadiliano na DPP kwa lengo la kuimaliza.

Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Aprili 1, 2026, ambapo Jamhuri itawasilisha mrejesho wa majadiliano hayo mahakamani.

Washtakiwa wanaoendelea na kesi hiyo ni Jasmine Elphas (ofisa wa benki makao makuu), Fredrick Elphas Ogenga, Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, ambao wote ni wafanyabiashara.