Simba juzi Alhamisi, Machi 19, 2026 ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Pamba Jiji katika mechi ya Ligi Kuu ya NBC iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
Matokeo hayo yameifanya Simba ipande hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 28 huku Pamba jiji ikibaki katika nafasi ya tano ikifikisha pointi 25.
Kitendo cha Simba kufunga bao moja katika mchezo huo kimeifanya ishindwe kuifikia au kuivunja rekodi ya Yanga ya kuwa timu pekee iliyopata idadi kubwa ya mabao dhidi ya Pamba Jiji katika Uwanja wa CCM Kirumba, tangu timu hiyo ya Mwanza iliporejea kushiriki Ligi Kuu msimu uliopita.
Katika mechi 23 ambazo Pamba Jiji imecheza nyumbani tangu ilipopanda Ligi Kuu, mchezo iliyofungwa idadi kubwa ya mabao nyumbani ni dhidi ya Yanga msimu uliopita ambapo ilichapwa mabao 3-0.
Ukiondoa mchezo huo, Pamba Jiji imeonekana sio timu inayoruhusu idadi kubwa ya mabao kirahisi pindi inapokuwa nyumbani katika mechi za Ligi Kuu.
Katika mechi 23 ilizocheza nyumbani kuanzia msimu uliopita hadi sasa, ni mechi mbili tu ambazo timu hiyo imefungwa zaidi ya bao moja, ukiondoa huo wa Yanga ambao ilichapwa mabao matatu.
Mechi hizo mbili ambazo Pamba Jiji ilifungwa mabao mawili kwa kila mechi, zote zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 ambazo moja ni dhidi ya Mashujaa FC msimu uliopita na nyingine dhidi ya Azam FC msimu huu.
Lakini mechi nyingine 20 zilizobakia, ukuta wa Pamba umeonekana kuwa mgumu kufunguka pindi Pamba Jiji inapokuwa nyumbani.
Timu hiyo imefungwa bao mojamoja katika michezo tisa na katika mechi 11 ilimaliza bila kuruhusu wapinzani kupata bao (clean sheet)