Jaji Warioba aeleza hatua kwa hatua alivyosoma, kufanya kazi na Jaji Manning

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema aliyekuwa Jaji wa kwanza mwanamke nchini, Julie Manning alikuwa kiongozi shupavu aliyeiongoza Wizara ya Sheria katika kipindi kigumu cha mageuzi makubwa ya kisiasa na kikatiba nchini.

Manning amefariki dunia leo Ijumaa Machi 20, 2026 akiwa na umri wa miaka 87.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu kifo hicho, Jaji Warioba amesema amemfahamu marehemu tangu walipokuwa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kabla ya kuendelea kushirikiana naye katika ngazi mbalimbali za utumishi wa umma.

“Namfahamu Julie Manning tangu akiwa mwanafunzi. Tulisoma pamoja chuoni, ingawa yeye alikuwa mbele yangu kwa madarasa mawili,” amesema jaji huyo.

Amesema baada ya kuhitimu masomo yao, wote waliingia katika utumishi wa umma kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo Manning alianza kazi kama mwandishi wa sheria, akionesha uwezo mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

Warioba amesema mwaka 1973, Manning aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria, huku yeye akiteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatua iliyowafanya kufanya kazi kwa karibu katika kuongoza wizara hiyo nyeti.

Amesema wakati huo, wote walikuwa vijana lakini walipewa dhamana kubwa akibainisha kuwa Manning alikuwa na umri wa miaka 37 pekee alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

“Manning alikuwa Waziri wa Sheria akiwa na umri wa miaka 37 na mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu nikiwa kijana kabisa, lakini tulifanya kazi nzuri sana katika wizara hiyo,” amesimulia Jaji Warioba.

Kwa mujibu wa Warioba, kipindi cha uongozi wa Manning kilikumbwa na changamoto kubwa zilizohusisha mabadiliko ya mifumo ya uongozi na sheria nchini.

“Manning aliongoza kipindi kigumu sana, kwani mwaka 1977 CCM na ASP ziliungana, kukawa na mabadiliko ya Katiba na baadaye mwaka 1978 ikaibuka vita ya Kagera lakini Manning alituongoza vizuri sana tukafanya kazi nzuri,” amesema.

Aidha, Jaji Warioba amesema kipindi hicho kilifuatiwa na kuzuka kwa Vita ya Kagera mwaka 1978, hali iliyoongeza uzito wa majukumu kwa viongozi wa serikali, hususan katika wizara ya sheria.

“Manning aliongoza katika kipindi kigumu sana. Kulikuwa na mabadiliko makubwa ya kikatiba baada ya muungano wa vyama mwaka 1977, na baadaye vita ya Kagera mwaka 1978, lakini alituongoza vizuri na tuliweza kutekeleza majukumu yetu ipasavyo,” amesema.

Warioba amesema mwaka 1983 Manning aliondoka katika wadhifa wake na kwenda nje ya nchi na ndipo alipoteuliwa kuchukua nafasi hiyo ya Waziri wa Sheria.

“Baada ya yeye kuondoka, niliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria kuanzia mwaka 1983. Kwa kweli tunamkumbuka kwa mengi, alikuwa kiongozi shupavu na mwenye uwezo mkubwa sana,” amesema.

Amesisitiza kuwa mchango wa Manning katika sekta ya sheria na uongozi wa umma utaendelea kukumbukwa, akieleza kuwa alikuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi wanawake na watumishi wa umma nchini.