Geita. Waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuendelea kumfanya Mwenyezi Mungu kuwa kimbilio lao kwenye maisha kwa kudumisha matendo mema kama ilivyokuwa wakati wa Ramadhani, ili awajalie kufanikiwa katika haja zao ambazo walimuomba.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Machi 20, 2026 na Sheikh Dauda Bushumbilo kutoka Taasisi ya Ansari Geita Mjini, wakati wa swala ya Eid el-Fitr iliyofanyika katika Msikiti wa Al Mtakuja, Geita Mjini.
Sheikh Bushumbilo amesema mfungo wa Ramadhani umewafundisha waumini wa Kiislamu kuomba toba na kumtegemea Mwenyezi Mungu kupitia maombi, hivyo ametoa rai kwa misikiti kutobaki wazi baada ya kukamilika kwa mfungo. Pia amesema swaumu ni kati ya Mungu na mwanadamu, hivyo kila muumini anao wajibu wa kudumisha uchamungu kwa kutenda wema.
“Tunapomaliza swaumu, huyo Allah hajaondoka, imeondoka Ramadhani. Tujikite katika kumcha Mungu na ndipo itakapopatikana tija ya swaumu. Haiwezekani miaka yote inapita swaumu, inapita Ramadhani, inakuacha vilevile hujabadilika, hujapata lengo la uchamungu,” amesema Sheikh Bushumbilo.
“Tunapomaliza Ramadhani, hii ni ibada kubwa ambayo inatufundisha kumcha Mungu. Kunakuwaje baina yako wewe na baina ya Allah? Kwa hiyo unapomcha Mungu ujue uko mbele ya Allah; anakuchunga, anakulinda, anajua unachokifanya.”
Aidha, waumini hao wametakiwa kutowaonea wanyonge na badala yake kuendelea kuwajali wahitaji kwa kujitoa fedha na vitu mbalimbali kama walivyofanya wakati wa mfungo, kama Qur’an inavyoelekeza kupitia Mtume Muhammad (SAW).
Katika hatua nyingine, Sheikh Bushumbilo amewataka wanawake kuendelea kudumisha maadili kwa kujistiri kama walivyofanya wakati wa mfungo. Pia wanaume wametakiwa kutokuwa kikwazo kwa wanawake kujistiri kwa mavazi ya stara kwa kisingizio kuwa wakivaa kwa stara wanaonekana wazee.
“Utamwona amevaa pengine nguo ya laki tano, pengine nguo ya milioni mbili, lakini haijamstiri. Anapenda kimini akiwalingia majirani; vichwa vyao wameachia kama nundu ya ngamia. Sisi wanaume ni wachunga. Kuna wanaume anaona mwanamke anajistiri, anamwambia unajizeesha wewe. Siku ya Kiyama utaulizwa.”
Abdulrahman Yassin, muumini katika Msikiti wa Al Mtakuja, ametoa rai kwa waumini wenzake kuendelea kumcha Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye huabudiwa wakati na baada ya Ramadhani. Pia amesema Waislamu wanatakiwa kuendelea kutoa sadaka na kuwajali wanyonge kwa kuwa itamtetea wakati wa Kiyama.
Naye Kassim Abdallah ameishukuru Serikali kwa kuendelea kudumisha amani na kutoa wito kwa wananchi wote bila kujali itikadi zao kudumisha amani nchini.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutulinda sisi wananchi kuwa na amani. Tunaomba amani sisi Waislamu na ambao sio Waislamu, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani.”