Ofisa wa Polisi jela miaka miwili kwa mauaji

Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti Rogers Mmari (F.4987) wa Kituo cha Polisi Ipogolo, kwenda jela kwa miaka miwili baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Tukio hilo lilitokea Desemba 14, 2024 Mtaa wa Ipogolo, Manispaa ya Iringa ambapo Mshtakiwa huyo alimpiga marehemu Nashoni Kiyeyeu (23) mpaka kufariki dunia kwa tuhuma za wizi wa simu.

Hukumu hiyo imetolewa jana Machi 19, 2026 na Jaji Angaza Mwipopo kufuatia kupitia ushahidi wa pande zote na kujiridhisha pasipo shaka juu ya ushiriki wa mshtakiwa katika tukio hilo.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo ulieleza kuwa Sajenti Rogers alipata taarifa kutoka kwa mwananchi Beatrice Kimata aliyemtuhumu marehemu kuiba simu yake.

Baada ya taarifa hiyo, askari huyo alimtafuta kijana huyo na alipompata alimshambulia kwa kumpiga akimtaka kurejesha simu inayodaiwa kuibwa.

Mahakamani ilielezwa kuwa kipigo hicho kilimsababishia majeraha makubwa marehemu hadi kupoteza fahamu na baadaye alipelekwa katika hospitali binafsi kwa matibabu kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa ambako alithibitishwa kufariki dunia kutokana na hali yake kuwa mbaya.

Aidha, mahakama ilibaini kuwa licha ya madai ya wizi, mshtakiwa hakuwahi kufungua kesi rasmi dhidi ya marehemu.

Katika utetezi wake, Sajenti Rogers alikiri kumpiga marehemu, akieleza kuwa alichukua hatua hiyo kutokana na kijana huyo kumjibu kwa dharau wakati wa mahojiano.

Baada ya kusikiliza mashahidi sita wa upande wa Jamhuri na watatu wa upande wa utetezi, mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia chini ya vifungu vya 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu na kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela.

Kwa mujibu wa mahakama, marehemu alipatikana na majeraha mbalimbali mwilini yaliyosababishwa na kipigo cha kitu chenye ncha kali, pamoja na kupasuka kichwa hali iliyosababisha kuganda kwa damu kwenye ubongo upande wa juu wa kulia.

Aidha, mahakama ilieleza kuwa baada ya tukio hilo, mshtakiwa alikimbilia Moshi kwa lengo la kupoteza ushahidi, kabla ya kukamatwa na kurejeshwa Iringa kwa ajili ya kuendelea na mwenendo wa kesi hiyo.

Aidha, ushahidi wa mazingira uliwasilishwa mahakamani ulionyesha kuwa marehemu alionekana kwa mara ya mwisho akiwa na mshtakiwa ndani ya gari lake aina ya Noah.

Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa kwa mujibu wa vifungu namba 195 na 198 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Katika hatua nyingine, wakili wa utetezi, Cleofas Mheluka, aliiomba mahakama kupunguza adhabu kutoka miaka minne mpaka kuwa miwili akieleza kuwa mshtakiwa ana familia yenye watoto watano na anakabiliwa na matatizo ya kiafya, huku akisisitiza kuwa tukio hilo halikuwa la kukusudia.

Mara baada ya hukumu hiyo, baba mzazi wa marehemu Nashon Kiyeyeu, mkazi wa Ipogolo, amesema familia haijaridhika na uamuzi huo, akieleza kuwa huenda imechangiwa na uzito wa kosa lenyewe.

Ameongeza kuwa kama wangekuwa na uwezo, wangeendelea na hatua zaidi za kisheria, hivyo wameiomba serikali iwasaidie ili haki ipatikane.