Watatu wafariki ikidaiwa kunywa dawa za kutoa nyongo, kuongeza hamu ya kula

Serengeti. Watu watatu wakazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara wamefariki dunia huku mmoja akipelekwa hospitalini baada ya kunywa dawa ya miti shamba waliyopewa kwa lengo la kutoa nyongo tumboni na kuongeza hamu ya kula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amesema tukio hilo limetokea jana Machi 19, 2026, saa 5 asubuhi. 
Amewataja waliofariki ni Kashi Joseph (52), Marko Machota (51) na Debora Nyamuhanga (58) wote wakazi wa Kijiji cha Burunga, huku mmoja akinusurika lakini akilazimika kupata matibabu hospitalini.

“Maji hayo yalipelekwa nyumbani na mmoja wa marehemu kwa ajili ya matibabu ya asili. Tayari tumeanza uchunguzi wa tukio hili,” amesema Kamanda Lutumo.

Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya wilaya ya Serengeti, huku manusura akiendelea na matibabu.

Kamanda Lutumo amewataka wakazi kuepuka kutumia dawa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika ili kuepuka madhara, ikiwemo vifo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linatoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kabla ya kutumia dawa bila kufuata maelezo kutoka kwa wataalamu walioidhinishwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, ambao watawaelekeza dawa gani watumie, kwa namna gani na kiasi gani,” amesema.

Wakiongea kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo, baadhi ya mashuhuda wa tukio wamesema dawa hiyo ilipelekwa nyumbani na Kashi Joseph ambaye wamedai alikuwa ni mtaalamu wa tiba za asili. 

“Huyu Kashi Joseph ambaye kwasasa ni marehemu huwa anachimba dawa hizo ambazo anadai zinatibu UTI na vidonda vya tumbo na magonjwa mengine,” amesema Nyangige Marwa. 
Amefafanua kuwa kabla ya kifo chake, Joseph alikuwa akifanya shughuli za utabibu wa kutumia dawa hizo za miti shamba ambazo alikuwa akitembeza mitaani na kuuza kwa watu mbalimbali kwaajili ya kutibu magonjwa mbalimbali. 

Marwa Matiko amesema alishuhudia watu hao wakinywa dawa hiyo siku ya tukio saa 2 asubuhi huku wakieleza kuwa dawa ilikuwa inasaidia kuondoa sumu mwilini na kuongeza hamu ya kula. 

“Dawa ilikuwa kwenye sufuria wakawa wanakunywa ilikuwa ni saa 2 asubuhi wote wanne walikuwa wanasema inaondoa sumu na kuongeza hamu ya kula lakini mwisho wa siku watatu wamefariki na mmoja ana hali mbaya,” amesema.