FORLAND YAHAMASISHA MATUMIZI YA MITI MINGINE YA ASILI

Na Mwandishi Wetu Michuzi Tv

WIZARA ya Maliasili na Utalii, kupitia mradi wa FORLAND, imesema inaendelea kuhamasisha matumizi ya miti mingine ya asili tofauti na inayojulikana sasa ya Mninga na Mkongo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya siku misitu, yanayoendelea kwenye viwanja vya Ilulu vilivyopo Manispaa ya Lindi, mkoani humo, Afisa misitu na Mratibu wa mradi huo, Emma Mzunda anasema kuna miti mingi ya asili ambayo haijulikani, hivyo kupitia mradi huo wamekuwa wakitangaza miti mingine ya asili inayoweza kutumika kwa bidhaa mbalimbali.

Miti hii ni pamoja na Mtundu, msasa, mtondolo/muwa, muhumbuti, mpilambati, mngoji/mlakwenzi, mpangapanga/pangapanga, mkarati, msolo, mgongachuma/mbanga-wanga na mlondolo/mdamudamu.

“Matumizi ya miti ya mkongo na mninga yamekuwa makubwa, sasa kupitia mradi huu tumekuwa tukifanya kazi ya kuitambulisha na kuitangaza miti mingine ya asili ambayo nayo inaweza kutumika katika matumizi mengine na kupunguza matumizi ya miti ya mkongo na mninga,”amesema Mzunda.

Kwa upende wake, Mkukufunzi wa Chuo cha Misitu Mafinga kinachosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Saidi Omari amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa vijana mbalimbali hapa nchini ikiwemo namna na kuhudumu kwenye misitu na mamna ya kuhudumia mashamba ya misitu

“Tunafanya kazi kwa karibu na mradi wa FORLAND, tumekuwa tukitoa mafunzo kwa vijana wengi hapa nchini hasa namna na kuhudumia mshamba ya misitu. Misitu inafaida kubwa kibiashara, lakini ipo namna ya kufanya ili kuweza kunufaika nayo,”ameongezea Omari.

Naye, Agustino Floidi Mnufaika wa mradi huo, anasema wamekuwa wakifaidia, kwani wameweza kunzisha vitalu vya miti pamoja na kuvuna mbegu mbalimbali na kuziotesha.

Hivi karibuni, Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Finland zimesaini hati ya makubaliano ya kikanda [MoU] chini ya Mradi wa Maendeleo ya Matumizi ya Ardhi na Minyororo ya Thamani ya Misitu Tanzania [FORLAND] ili kuimarisha usimamizi na uratibu wa mandhari ya misitu katika mikoa ya Ruvuma na Lindi, Iringa na Njombe ambako FORLAND inaendesha miradi yake.

Mradi huu unatekelezwa katika nyanja tofauti zikiwemo za uzalishaji wa mbegu bora za miti, mikakati ya mapambano ya moto na utoaji elimu kwa wakulima wa miti na itahusisha mnyororo mzima wa zao la misitu kuanzia wakulima wenyewe,wasafirishaji viwanda vya uchakataji pamoja na kuwajengea uwezo wadau wa misitu.

Maonyesho ya kuelekea kilele cha Siku ya Misitu Duniani yalifunguliwa na Makamu wa Rais, Mh Dkt. Emmanuel Nchimbi Alhamisi na yanatarajiwa kufungwa Jumamosi, Machi 21, 2026.