Jana katika sehemu ya pili ya simulizi ya mauaji ya kikatili ya mtoto Timotheo Mhulila, ambaye aliuawa na kisha kukatwa vipande vipande na kutumbukizwa chooni, tuliona namna shahidi ambao ni askari polisi walivyoeleza namna mshitakiwa, Joseph Mhulila alivyokiri.
Katika ushahidi huo, shahidi aliyeandika maelezo ya onyo ya mshitakiwa, alieleza kuwa Mhulila katika maelezo yake aliweka bayana kuwa baada ya kumuua mwanawe, mwili wake aliukata vipande vidogo kwa kutumia kisu na mifupa mikubwa kama fuvu aliiponda kwa jiwe ili iweze kupenya kwenye choo cha kuflashi.
Tukio hilo lilitokea kati ya Aprili 9 na 12, 2025 katika Mtaa wa Lukosi, Kata ya Mkwawa wilayani Iringa.
Katika simulizi ya leo, tunaangazia namna mshitakiwa alivyojitetea kortini baada ya Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Iringa kumuona ana kesi ya kujibu na hivyo kuamua kujitetea chini ya kiapo.
Mshitakiwa ambaye ni dereva bajaji anayeishi eneo la Mtwivila B alikiri kwamba Daima Hongoli aliyekuwa shahidi namba 1 wa Jamhuri ni mama wa mtoto Timotheo ambaye aliuawa.
Aliieleza mahakama kuwa Aprili 12, 2025 mtoto huyo alitoweka baada ya yeye kwenda kuchukua bajaji yake huko Igwana Hoteli akiwa naye, aliporudi alipomuacha, hakumkuta.
Walianza kumtafuta pasipo mafanikio na ndipo alipowaita madereva bajaji wenzake na mzazi mwenzie (Daima) ambaye alishiriki kusaidia kumtafuta hadi saa 5:00 na 6:00 usiku, ndipo walipoamua kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi.
Walipofika polisi, maofisa wa polisi waliwaonyesha chumba ambacho watoto waliopotea walikuwemo, lakini mtoto wao hakuwa miongoni mwao na hivyo askari polisi waliwaelekeza yeye na mzazi mwenzake warudi baada ya saa 24.
Siku iliyofuata, waliendelea na msako huo kwa kushirikiana na madereva bajaji wenzake, lakini Aprili 14, 2025 alipokea simu kutoka kwa ofisa wa polisi akimtaka afike dawati la jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa na alienda.
Alipofika hapo, ofisa aliyempigia simu alimjulisha kuwa anakabiliwa na tuhuma za kuiba mtoto, alikamatwa na kuwekwa mahabusu ambapo alikaa kwa wiki tatu.
Aliikana nyumba aliyopanga
Katika utetezi huo, alidai Mei 6, 2025 saa 4:00 asubuhi, alichukuliwa na maofisa wawili wa Polisi, Thony na Lazaro na kumpeleka katika nyumba ambayo haifahamu na huko walikuta watu wengi nje ya nyumba hiyo.
Alieleza kuwa maofisa hao waliwaeleza watu waliokusanyika hapo kuwa yeye anahusika na mauaji na wamemleta katika nyumba hiyo ili aonyeshe mwili ulipo.
Pia alikana kumfahamu shahidi namba 4 wa Jamhuri, Maximilian Luhwago, ambaye katika ushahidi wake alimtambua mshitakiwa kama mpangaji wake tangu 2021.
Alidai shahidi huyo alishindwa kuleta kielelezo chochote kuthibitisha kuwa yeye ni mpangaji wake na kwamba hakuwahi kuwaonyesha shahidi wa 4, 5 au shahidi yeyote, choo ambacho alidaiwa kutupa vipande vya mwili wa mtoto wake.
Kulingana na ushahidi huo, choo hicho watu wengi wanakitumia na kwamba yeye ni mgeni kabisa katika nyumba, ambayo maofisa hao wa polisi walimpeleka.
Alidai kuwa ushahidi wa maofisa wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji na wale wa Mamlaka ya Majisafi na Taka Iringa (Iruwasa) ulikuwa ni wa kujikanganya.
Aliendelea kueleza kuwa maelezo yake ya onyo ambayo yalipokewa kama kielelezo P2 yaliyoandikwa na shahidi wa 12 wa Jamhuri, yaliandikwa siku iliyofuata baada ya kutoka Mtwivila, hivyo si kweli kwamba maelezo hayo ndiyo yaliyosaidia kupatikana kwa vipande vilivyodaiwa vya mwili wa mtoto wake.
Alidai kuwa kabla ya kusaini maelezo hayo, alipigwa sana na maofisa wa polisi na kulazimishwa kusaini nyaraka ambazo tayari zilikuwa zimeandikwa huko, ramani ikionyesha eneo la tukio ni Mtwivila lakini maelezo ya kosa yanasema ni Mkwawa.
Mshitakiwa huyo aliendelea kujitetea kuwa ushahidi wa shahidi namba 10 unadai tukio lilitokea Mei 12, 2025, hata hivyo akadai ushahidi huo unajikanganya na ushahidi wa mashahidi wengine wa Jamhuri waliodai ni Mei 9, 2025.
Pia alikanusha kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli za damu na mate kama alivyoeleza shahidi namba 9 na kwamba hakuna nyaraka yoyote iliyotolewa kuthibitisha sampuli zilitoka kwake.
Aliendelea kudai kuwa shahidi wa 13 wa Jamhuri alidai vipande vya mifupa alivyovifanyia uchunguzi wa vinasaba (DNA) vilioana na sampuli ya damu na mate yake, lakini akadai shahidi huyo siye aliyechukua sampuli hizo.
Alidai kuwa hana uhakika kama sampuli alizozitumia kulinganisha na mifupa hiyo zilikuwa zimetoka kwa mzazi mwenzake au kwake na kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa marehemu anayetajwa ni mwanaye aliyepotea.
Akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa Serikali walioendesha shauri hilo, alidai kuwa hafahamu kama mtoto wake amekufa au la na kuwa hakumrudisha mtoto kwa mama tangu alipomchukua Machi 28, 2025.
Alidai pia hafahamu nyaraka ambayo shahidi kutoka Iruwasa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walitakiwa kuzitoa kama kielelezo kuthibitisha kuwa walinyonya maji kutoka katika shimo la choo katika nyumba iliyopo Mtwivila.
Katika majibu yake, alidai hakuna sampuli za DNA zilizochukuliwa kutoka kwake na wala hafahamu chochote kuhusu sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa marehemu na mama wa mtoto.
Alieleza kuwa mzazi mwenzake huyo alikuwa sahihi kutoa taarifa Kituo cha Polisi Aprili 14, 2025 juu ya kupotea kwa mtoto na kwamba polisi walikuwa na sababu za kutosha za kumkamata kwa vile mtoto huyo alitoweka mikononi mwake.
Alisisitiza kuwa hahusiki na kifo cha mwanae, kwamba alilazimishwa kusaini maelezo ya onyo ambayo tayari yalikuwa yameandikwa na hajawahi kupewa cheti cha kifo cha mwanaye, hivyo akaomba mahakama imwachie huru.
Katika mawasilisho ya mwisho ya upande wa utetezi, Wakili wa mshitakiwa, Geofrey Mwakasage alisema shitaka dhidi ya mteja wake lilikuwa halijathibitishwa kwa kuwa hakuna uhakika wa muda na eneo ambapo mtoto huyo aliuawa.
Wakili Mwakasage alieleza kuwa kulikuwa na kujikanganya katika ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri na kwamba maelezo ya kukiri kosa ya mshitakiwa hayakupatikana kwa hiyari na wala hayakurekodiwa kwa usahihi na polisi.
Alieleza pia kulikuwa na kukosekana kwa nyaraka sahihi wakati wa uchukuaji wa sampuli za DNA zilizochunguzwa na mkemia mkuu wa Serikali na kukosekana huko kunafanya kusiwepo uthibitisho wa namna sampuli hizo zilivyosafirishwa.
Kwa upande wao, upande wa mashitaka walieleza kuwa shauri hilo limejengwa katika msingi wa mazingira, hasa kupitia kanuni ya kisheria kuwa mtu anayekuwa wa mwisho kuwa na marehemu kabla ya kifo chake, anachukuliwa ni mhusika.
Mawakili hao, Mwakalinga na Mwakiborwa Walieleza kuwa marehemu ni mtoto mdogo asiye na hatia, aliyeuawa na baba yake mzazi na kiini cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwamba kwa kufanya hivyo kungemwezesha kuwa tajiri.
Walieleza kuwa ushahidi unaonyesha viungo vya marehemu vilikatwa katika vipande vidogo vidogo na uchunguzi wa DNA wa mifupa ulithibitisha kuwa marehemu alikuwa ni mtoto wa damu wa mshitakiwa pamoja na Daima.
Kwa mujibu wa mawakili hao, kupatikana kwa viungo vya mtoto huyo kunathibitisha kuwa ni marehemu na hakufa kifo cha kawaida na maelezo ya ungamo ya mshitakiwa, yanathibitisha ndiye aliyefanya ukatili huo.
Mawakili hao walisema mshitakiwa ndiye aliyekuwa na mtoto hadi anatoweka na kwamba matendo ya mshitakiwa yanadhihirisha alikuwa na nia ovu katika kufanya mauaji hayo, kwa kumkata kata viungo vyake na kuvitumbukiza shimo la choo.
Waliendelea kujenga hoja kuwa mshtakiwa alijaribu kuficha uhalifu huo kwa kumpotosha mama wa mtoto, kuwa amepotea eneo la Hoteli ya Kani na kwamba utetezi wa mshitakiwa haujaweza kuvunja ushahidi madhubuti wa Jamhuri.
Kuhusu mkanganyiko wa eneo la tukio, mawakili hao wamerejea ushahidi wa shahidi wa 3 wa Jamhuri aliyesema eneo la tukio lipo mpakani kwa Kata ya Mtwivila na Mkwawa na kwamba ushahidi wa Jamhuri ulikuwa ni madhubuti.
Usikose kusoma simulizi hii kesho wakati Jaji akichambua ushahidi wa pande mbili na kutoa hukumu.
