Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kuwa limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Athumani Nyanza, ambaye mwili wake ulipatikana umefukiwa kwenye shimo karibu na makazi yake, Mtaa wa Kimya Kimya, Chanika jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, Nyanza anadaiwa kuuawa na mpenzi wake kabla ya mwili wake kufukiwa katika eneo hilo kwa lengo la kuficha uhalisi wa tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa Machi 20, 2026 ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watuhumiwa hao walikamatwa Machi 18, 2026 mkoani Morogoro kufuatia uchunguzi uliofanywa kwa kushirikiana na wananchi.
Kamanda Muliro amesema mtuhumiwa mmoja ametambuliwa kwa jina la Rahema Maulidi (42), mkazi wa Kigamboni, huku jina la mtuhumiwa wa pili likihifadhiwa kwa sababu za uchunguzi unaoendelea.
“Watuhumiwa wote wanashikiliwa na wanaendelea kuhojiwa kwa kina kuhusiana na tukio hilo, huku taratibu za kisheria zikiendelea ili waweze kufikishwa mahakamani,” amesema Muliro.
Jeshi hilo limepongeza ushirikiano uliotolewa na wananchi, likisema umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Aidha, Kamanda huyo amesesisitiza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuwa nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Kamanda Muliro pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha usalama katika maeneo yao.
Licha ya kwamba Muliro haingia kwa undani, chanzo cha Mwananchi kimeeleza kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa Rehema ambaye ni mpenzi wa Nyanza kulitokana na mienendo yake ya kuwasiliana na ndugu na marafiki wa marehemu, akituma ujumbe unaohusiana na mtoto.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, mawasiliano hayo yaliwapa fursa maofisa wa upelelezi kufuatilia nyendo zake kupitia simu, hatua iliyosaidia pia kubaini alikokuwa amejificha mkoani Morogoro na hatimaye kukamatwa.
“Alikuwa akituma ujumbe kwa watu mbalimbali kuhusu mtoto, jambo lililowezesha kufuatiliwa kwa urahisi kupitia mawasiliano yake hadi alipokamatwa,” kimeeleza chanzo hicho.
Mbali na ndugu wa marehemu, chanzo hicho kimesema mtuhumiwa huyo alikuwa akiwasiliana pia na watu wengine, wakiwamo ndugu zake waliokuwa wakijaribu kumsaidia kukwepa kukamatwa, hata kwa kutumia mbinu mbalimbali.
Akizungumza na Mwananchi Machi 19, 2026, rafiki wa marehemu, Madebe Lidai alisema mpenzi wa Nyanza aliwekwa chini ya ulinzi baada ya kuibuka kwa wasiwasi kufuatia kutoweka kwa marehemu.
Alisema mwanamke huyo alihojiwa na Polisi kuhusu alipo Nyanza lakini hakuwa na majibu ya kuridhisha na mara kadhaa alikuwa akizima simu yake, hali iliyoongeza mashaka na kuibua uchunguzi wa kina dhidi yake.
“Mimi nilimuuliza kama amewasiliana na Nyanza akasema hajui alipo. Hata hivyo, kabla ya kupotea, marehemu aliniaga kuwa anakwenda kwa mpenzi huyo Kigamboni, jambo lililonifanya nianze kupata mashaka na mpenzi huyo,” alisema Lidai.
Aliongeza kuwa hata awali alipofikishwa Polisi Chanika kwa mahojiano, mtuhumiwa huyo alikuwa akitoa majibu yanayokinzana na kuomba aachiwe ili akamtafute mpenzi wake.
Kwa mujibu wa Lidai, polisi walimwchia kwa dhamana kwa masharti ili kuendelea na uchunguzi naye akitakiwa kwenda kumtafuta Nyanza. Dhamana hiyo ilisimamiwa na dada yake.
Hata hivyo, alisema hatua ya kuachiwa kwa dhamana ilizua mashaka zaidi kwa familia ya marehemu, kutokana na uzito wa tukio hilo.
“Sikuelewa mantiki ya kumwachia mtu katika mazingira kama haya, lakini nilijipa moyo kuwa huenda kulikuwa na sababu za kiupelelezi,” alisema.
Baada ya kuachiwa, mtuhumiwa huyo hakurejea wala hakuonekana, hali iliyozidisha wasiwasi. Inadaiwa kuwa mdhamini wake naye hakuwa akipatikana kwa urahisi na hakuwa na majibu ya kuhusu alipo mtuhumiwa.
Kutokana na hali hiyo, polisi waliendelea na uchunguzi na mdhamini alikamatwa kupitia mawasiliano yake, huku juhudi za kumtafuta mtuhumiwa mwenyewe zikiwa zinaendelea, hasa katika makazi yake ya Kigamboni.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari, binti mmoja aliyekuwa akiishi katika nyumba ya marehemu alikamatwa pia kwa tuhuma za kusaidia kutoa taarifa kwa watu waliokuwa wakifika eneo hilo.
Hata hivyo, taarifa zinadai walipomuhoji binti huyo kuhusu alipo Nyanza alidai hana taarifa zozote na kuwa yeye alikuwa amehamia tu katika nyumba hiyo hivi karibuni. Hata hivyo, polisi walimchukua kwa mahojiano zaidi.
Inaelezwa kwamba baada ya kuwakamata watu hao, uchunguzi uliendelea na mahojiano ya kina, ambapo askari waliambatana na wanafamilia kwenda Kigamboni kufuatilia taarifa zaidi.
“Tulipofika, wapangaji wenzake walisema hawajamuona kwa siku kadhaa, lakini alikuwa akija nyumbani kwa kujificha,” amesimulia Lidai.
Kwa mujibu wa wapangaji wenzake, mtuhumiwa huyo alikuwa akivaa mavazi ya kininja na miwani myeusi, ili kuficha utambulisho wake, jambo lililozua wasiwasi miongoni mwao.
Aidha, ilielezwa kuwa kabla ya kutoweka, mtuhumiwa aliwaambia wapangaji wenzake kuwa anauza baadhi ya vitu vyake vya ndani ya nyumba anataka kusafiri na hangerudi.
“Aliuza baadhi ya vitu vyake vya ndani kama makochi na akawaambia wenzake anaondoka na hatarudi tena,” alisema.
Baada ya kupata taarifa hizo, ndipo familia ilishtuka na kuwaomba Polisi kuchunguza shimo lililochimbwa karibu na nyumba ya Nyanza ili kubaini ndani kumefukiwa nini.
Kwa kushirikiana na polisi, shimo hilo lilifukuliwa na kukutwa mwili wa Nyanza.
Mwananchi lilipotaka kufahamu endapo maiti imekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko, Lidai amesema wameambiwa bado uchunguzi wa kitabibu wa vipimo vya vinasaba (DNA) unaendelea, ukikamilika watakabidhiwa kwa hatua ya maziko.
“Tulitarajia kupewa mwili jana ili tufanye mazishi leo, lakini bado tunasubiri majibu ya vipimo vya DNA ambavyo tumeambiwa huchukua kati ya saa 24 hadi 48,” amesema.
Mwananchi iliporejea kwa Jeshi la Polisi kutaka kujua hatima ya mwili huo, imeeleza kuwa bado uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wote wa tukio hilo kabla ya hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na mauaji hayo.