Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema wametekeleza ibada ya swaumu katika hali ya amani na utulivu, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kudumisha mshikamano na kuleta umoja kwa maslahi ya Taifa hilo.
Pia, amewataka kuendeleza mema waliyoyafanya wakati wa swaumu kwani kitabu kitukufu cha Quran hakina ukomo wa kufanya mema jambo ambalo litachochea ustawi wa jamii na kukuza maendeleo yao.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 21, 2026 katika Baraza la Eid la kitaifa lililofanyika katika ukumbi wa makao makuu ya Polisi Zanzibar Ziwani ikiwa ni hitimisho la mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Tumetekeleza ibada ya swaumu katika hali ya amani na utulivu, hakika hii ni neema kubwa kwani kama sote tunavyojua wapo waislamu wengi hususani Mashariki ya Kati wanaokabiliwa na changamoto za kiusalama,” amesema.
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akisalimiana na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika kipindi cha awamu ya kwanza ya utawala wake, Othaman Masoud katika msikiti wa Zinjibar iliposwaliwa sala ya kitaifa ya Eid Unguja Zanzibar
Dk Mwinyi amesema “tunamuomba Mungu atujalie na kuilinda na kuidumisha neema ya amani katika nchi yetu na awajaalie waislamu wote duniani kuwe na amani katika ustawi wa kuleta maendeleo yetu sote.
Amesema mwezi wa Ramadhani walioukamilisha ni msimu na chuo maalumu, kuhuisha imani zao na kukuza ucha Mungu, katika kipindi chote walitekeleza ibada mbalimbali wakiwa na matarajio kupata fadhira nyingi za utukufu kwa mwezi huu wa Ramadhani.
“Ni wajibu wetu kuendeleza hayo yote katika maisha yetu yote ili kupata mafanikio ya duniani na kesho mbele ya haki, tumuombe Mwenyezi Mungu atuwezeshe kudumu katika mwenendo huo mwema,”
Amesema wakati wa kipindi cha Ramadhani kulikuwa na utaratibu wa kusoma quran ambao sio tu kuleta neema pekee, bali unachangia kuwarithisha watoto katika makuzi mema.
Ili kuwa na jamii njema yenye kuwa na hofu ya Mungu na kufanya mambo mema na kujiepusha na vitendo viovu wanawajibu kuendeleza hayo hata baada ya Ramadhani kwani Quran ni mwongozo wa kila siku hata kwa watoto.
Amesema miongoni mwa mambo mema waliyoyafanya ni kuhurumiana na kufanyiana hisani kutoa sadaka kuwasaidia wenye uwezo mdogo kukidhi mahitaji yao.
“Sadaka hizo zimesaidia katika kupata mahitaji yao na kuwaondolea wasiwawasi kutopata futari na kuwasaidia, kutekeleza ibada ya swaumu na kuleta mapenzi baina yetu,” amesema
Kwahiyo, “tuendeleze utaratibu huu mzuri kuwasaidia na kuwakumbuka wenye mahitaji katika maisha ya kila siku kwa kutoa sadaka na zaka ni miongoni mwa mambo tunayohimizwa kufanya kutokana na faida zake kuchochea ustawi wa jamii.
Katika kuhakikisha wanasherehekea sikukuu kwa amani na furaha, kiongozi huyo mkuu wa serikali, amezitaka mamlaka zinazosimamia usalama viwanja vinavyotumika kusherehekea sikukuu kuhakikisha vinakuwa salama.
Kadhalika amewataka polisi na mamlaka zinazosimamia vyombo vya barabarani kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinazingatiwa na wananchi wanapata fursa kusherehekea kwa amani.
Akizungumza kuhusu Hijja, Dk Mwinyi amesema wanawatakia maandalizi mema wanaotarajia kwenda kwenye ibada hiyo huku akitumia fursa hiyo kuitaka kamisheni ya wakfu na mali ya amal bila kuzitaja, kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili maujaji hao.
Amesema kwa upande wa serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi zinazoshughulikia maujaji ili idadi yao iongezeke, huku akiahidi kwamba wataendelea na taratibu za kukamilisha mfuko wa hija ili kutoa fursa kwa watu wengi zidi waweze kutekeleza ibada hiyo.
Awali katika swala ya Eid iliyoswaliwa katika msikiti wa Zinjibar Mazizini, ambapo Rais Mwinyi aliungana na viongozi wengine wa kitaifa na waumini, Sheikh kutoka ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Khamis Gharib Khamis amesema siku hii inadhihirisha furaha kwa kula vyakula vizuri, kuvaa vizuri na kutembeleana mambo yanayozidisha upendo miongoni mwa waislamu.
“Furaha ya kweli inaendana na matendo mema, tujiepushe na machukizo na kukosena kutendeana mabaya, tuendeleze yale yote tuliyoyatenda wakati wa funga,” amesema Sheikh Khamis.
