Pemba. Waumini wa dini ya Kiislamu wamehimizwa kuendeleza amali njema walizokuwa wakizifanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kustahili malipo mema Akhera.
Wito huo umetolewa na Sheikh Hamad Khamis mara baada ya kumalizika kwa swala ya Idd El-Fitr iliyoswaliwa katika Msikiti wa Ijumaa Sizini, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza na waumini hao, Sheikh Khamis amesema kuwa kipindi cha Ramadhan kilitawaliwa na ibada nyingi, zikiwemo swala za usiku (Tahajud) na Tarawehe, hivyo ni vyema kuendeleza ibada hizo hata baada ya mfungo kumalizika.
Amesema si sahihi kwa waumini kusitisha ibada na kuacha sunnah walizozizoea mara tu Ramadhan inapomalizika, akisisitiza umuhimu wa kudumisha mwenendo huo wa kiibada.
“Niwaombe waumini wa dini ya Kiislam, Ramadhan imekwisha lakini si kwa maana ya kuacha ibada mlizokuwa mkizifanya. Inapaswa kuendelezwa,” amesema Sheikh Khamis.
Ameonya kuwa baadhi ya waumini huacha kwenda msikitini na kurejea katika vitendo visivyofaa mara baada ya Ramadhan, jambo alilosema halikubaliki, akiwataka kuendelea kushikamana na matendo mema.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuwajibika katika malezi ya watoto wao, hususan kuhakikisha wanazingatia maadili ya mavazi yanayokubalika kidini.
Amesema si vyema mzazi aliyefunga mwezi mzima kushindwa kusimamia mienendo ya watoto wake, ikiwemo namna ya mavazi yao, akisisitiza kuwa wazazi watawajibika kwa malezi hayo.
“Mzazi unapaswa kusimamia maadili ya mtoto wako. Si sahihi kumuacha avae mavazi yasiyofaa, kwani hilo ni jukumu lako na utawajibika mbele ya Mwenyezi Mungu,” amesema.
Vilevile, amewahimiza waumini kulinda swaumu zao kwa kuepuka vitendo viovu vinavyoweza kuharibu thamani ya ibada zao, akibainisha kuwa kufanya maovu siku ya Idd ni kinyume cha mafundisho ya dini.
Kwa upande wake, Imamu wa msikiti huo, Maalim Abdalla Hamad, amewasihi waumini kuelekeza nguvu katika utoaji wa sadaka, hususan kwa watu wasiojiweza na mayatima.
Amesema wapo watu wenye hali ngumu wanaohitaji kusaidiwa ili nao waweze kusherehekea Sikukuu ya Idd kwa furaha na utulivu wa nafsi.
“Ni muhimu kuwasaidia wenye uhitaji, mayatima na wagonjwa ili nao wajisikie faraja katika kusherehekea Sikukuu ya Idd El-Fitr,” amesema.
