Dodoma. Waislamu nchini wametakiwa kudumisha amani na utulivu huku wakisisitizwa kujiepusha na tabia ya kuchanganya masuala ya dini na matamanio yao binafsi.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Machi 21, 2026 na Sheikh Omar Itara wakati akitoa mawaidha katika Swala ya Idd El-Fitri iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akizungumza mbele ya waumini, Shekhe Itara amesisitiza umuhimu wa kulinda amani, akieleza kuwa haikubaliki kwa mtu kutumia dini kama chombo cha kutimiza matamanio yake binafsi.
“Yeyote anayetekeleza mambo ya dini kisha akayachanganya na matamanio yake binafsi huporomosha maslahi na hadhi yake. Katika dini ya Kiislamu, mambo ya dini yanapaswa kutekelezwa mahali na wakati unaostahili,” amesema.
Ameongeza kuwa vitendo vya kutumia kivuli cha dini kutekeleza mambo yenye maslahi binafsi vinaweza kusababisha mtafaruku ndani ya dini na pia kuchochea kuvurugika kwa amani ya jamii, hali ambayo haipaswi kuvumiliwa.
Sheikh Itara amesema Uislamu ni dini inayohimiza amani, mshikamano na kuheshimu dini nyingine, akionya kuwa madhara ya kupotea kwa amani huonekana wazi pindi inapokosekana.
“Hivyo, ni wajibu wa kila Muislamu kuhakikisha analinda amani na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa wananchi,” amesisitiza.
Aidha, amewataka waumini kusherehekea sikukuu ya Idd kwa amani na utulivu huku wakijiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuleta madhara kwa jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya waumini wa dini hiyo wamemshukuru Mungu kwa kuwafikisha salama kumaliza mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea sikukuu ya Idd kwa amani.
Mmoja wa waumini hao, Jasmin Shamwepu, amewataka wanawake wa Kiislamu waliokuwa wakijistiri katika kipindi cha Ramadhani kuendeleza mwenendo huo hata baada ya mwezi huo, akieleza kuwa ni njia ya kumpendeza Mungu.
Naye Omar Ijumaa amesema siku ya Idd ni ya kusherehekea pamoja na familia na jamii, hivyo ni muhimu kwa waumini kujiepusha na matendo maovu.
“Ni vyema kila mmoja akajilinda na matendo maovu katika siku hii muhimu, kwa kuwa kufanya maovu siku ya Eid ni jambo lisilokubalika,” amesema Ijumaa.
