Nuksi ya sare imeendelea kuiandama Yanga baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Huo umekuwa ni mchezo wa tatu mfululizo kwa Yanga kupata matokeo ya sare tasa katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Azam FC na TRA Unted.
Sare hiyo inaonekana kuwa na faida kwa Simba ambayo kama ikipata ushindi katika viporo vyake vitatu, itakuwa nyuma ya Yanga kwa pointi moja.
Katika mchezo wa jana ambao haukuwa wa kuvutia sana pengine kutokana na eneo la kuchezea la Uwanja wa Jamhuri kuonekana kutokuwa rafiki kwa sababu ya hali ya unyevu iliyotokana na mvua zilizonyesha siku za hivi karibuni, Yanga ndio ilitangulia kupata bao kupitia kwa Pacome Zouzoua katika dakika ya 23.
Pacome alifunga bao hilo akimalizia pasi iliyotokea upande wa kushoto ambayo ilipigwa na Emmanuel Mwanengo.
Mwanengo alitumia vyema kosa la kipa Costantine Malimi aliyetema mpira wa shuti uliopigwa na Allan Okello na kumpasia Pacome aliyeujza wavuni.
Bao hilo lilidumu hadi katika dakika za majeruhi ambapo Mtibwa Sugar ilisawazisha kupitia kwa Ismail Mhesa ambaye alifunga kupitia mpira wa kona uliojaa moja kwa moja wavuni baada ya kushindwa kuokolewa na walinzi wa Yanga.
Pamoja na Yanga kutoka sare jana, timu hiyo imeendeleza rekodi yake ya kibabe ya kutopoteza mechi katika Ligi Kuu ya NBC ikifikisha idadi ya michezo 35 mfululizo bila wapinzani kupata ushindi dhidi yake.
Mara ya mwisho kwa timu hiyo kupoteza mchezo wa Ligi Kuu ilikuwa ni msimu uliopita ilipofungwa mabao 3-1 na Tabora United (sasa TRA United), katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Novemba 7, 2024.
Katika mechi hizo 36 ambazo Yanga haijapoteza, michezo 30 imepata ushindi na mitano imetoka sare.
Matokeo ya jana yameifanya Yanga iendelee kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha pointi 38 huku Mtibwa Sugar ikisogea hadi nafasi ya nane baada y kufikisha pointi 22.
SIMBA, TABORA UNITED KITAELEWEKA
Mchezo mwingine wa Ligi hiyo leo utakuwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, Simba itaikaribisha TRA United kuanzia saa 1:30 usiku.
Timu hizo zinakutana zikiwa na kumbukumbu ya mchezo wao uliopangwa kuchezwa Machi 14, 2026 ambao TRA United ilikuwa mwenyeji, kutofanyika kutokana na Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kujaa maji, hali iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jijini humo kabla ya mechi.
Simba yenye pointi 28, ushindi katika mechi ya leo utaifanya isogee hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na iwapo TRA United iliyo katika nafasi ya 10 ikipata ushindi, itafikisha pointi 23 ambazo zitaivusha hadi katika nafasi ya saba.
Mchezo huo unakutanisha timu mbili ambazo zote zilipata matokeo ya sare katika mechi zao zilizopita kabla ya leo ambapo TRA United ilitoka sare tasa na Yanga huku Simba ikifungana bao 1-1 na Pamba Jiji.