Mtibwa vs Yanga mtego uko hapa!

YANGA inarudi uwanjani leo ikiendelea na ziara ya mechi za ugenini itakapokutana na Mtibwa Sugar na timu zote mbili zitakuwa na akili moja tu ya kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.

Huu utakuwa mchezo wa mwisho kwa timu zote kabla ligi haijasimama kupisha michezo ya timu za Taifa na Taifa Stars itakwenda Rwanda kushiriki michuano ya Fifa Series.

Katika michezo miwili iliyopita Yanga haijashinda hata moja, ikiangusha pointi nne, lakini Mtibwa nayo haijashinda mechi zake nne zilizopita, ikiangusha pointi 11, timu yoyote itakayoondoka na alama tatu zitakuwa na maana kubwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wenyeji wakiwa wanatamani hilo.

Yanga ipo kwenye presha kubwa ya matokeo baada ya kutoa sare tatu mwezi huu kwenye mechi tatu tofauti, ikianza na Simba, ikafuata ile ya Azam na TRA United, ikiangusha jumla ya pointi sita kwenye mechi hizo.

Matokeo hayo yalikuwa yameshawapa presha na Simba ambayo juzi ilikuwa ugenini dhidi ya Pamba Jiji, kama ingeshinda tu timu hizo zingekuwa zimekaribiana kwa pointi, zikitofautiana kwa pointi moja pekee, jambo ambalo limekwama kufuatia wekundu hao nao kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Ikiwa imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa juu ya msimamo, Yanga inakwenda kuanza mzunguko wa pili leo dhidi ya Mtibwa, ikikumbuka ilianza msimu na ushindi mzuri wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo.

Changamoto kubwa kwa Yanga sasa ni uwepo wa idadi kubwa ya majeruhi kwenye kikosi chao, ambapo timu hiyo imesalia na mshambuliaji halisi mmoja pekee, Emmanuel Mwanengo, baada ya wenzake Clement Mzize, Laurindo Aurelio ‘Depu’ na Prince Dube  kuwa na majeraha na wataukosa mchezo huo.

Yanga leo italazimika kuwa na mpango mpya wa kutengeneza ushindi, ikitegemea zaidi viungo wakiongozwa na Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Allan Okello wakisaidiana na Mwanengo.

Pedro hatakuwa na presha kwenye safu  ya ulinzi ambayo haina shida, licha ya mabeki wake watatu Dickson Job, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na Chadrack Boka nao kuwa majeruhi, lakini timu hiyo haijaruhusu bao kwenye mechi zake saba zilizopita.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, akizungumzia mchezo huo aliendelea kulia na ratiba ngumu ya timu yake na majeruhi, lakini akasema wamefanya maandalizi mafupi wakiongeza ubora wa kufunga mabao sambamba na kuiboresha safu yake ya ushambuliaji.

“Tuna majeruhi wengi lakini pia tuna ratiba ngumu ya ligi, mechi zetu zipo karibu sana tena chini ya masaa 72 lakini hatujakata tamaa, tunaendelea kutafuta ushindi tukiwa juu ya msimamo, tumepata siku moja ya maandalizi hatuwezi kubadilisha mengi lakini tunaweza kuwa na utofauti katika muundo wa kikosi,” alisema Pedro.

“Haitakuwa mechi rahisi, tunakutana na timu yenye wachezaji vijana wenye nguvu lakini pia wenzetu nao wanatafuta ushindi kutokana na namna mechi zao zilizopita walivyopambana na matokeo mazuri.”

Mtibwa Sugar kwenye mechi tano za mwisho imeshinda moja nyumbani hapohapo Jamhuri dhidi ya Prisons mabao 2-1 Februari 2, 2026, baada ya hapo ikatoa sare moja na kupoteza tatu.

Eneo ambalo benchi la ufundi litakuwa limeweka nguvu kubwa kuliboresha ni safu ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao 11 kwenye mechi hizo tano zilizopita, lakini safu ya ushambuliaji nayo ikifunga mabao matano tu.

Mtibwa nguvu yao kubwa itakuwa kwa watu wao watatu walioanza msimu kwa kuwa na namba nzuri ndani ya kikosi chao, mshambuliaji Magata anayeongoza kwa ufungaji kwenye timu hiyo akiwa na mabao matatu, akifuatiwa na Ismail Mhesa na Said Mkopi ambao kila mmoja amefunga mabao mawili. Mtibwa ikishinda leo, itawasaidia kutoka nafasi ya tisa hadi ya saba na pointi 24, na kuzishusha Dodoma Jiji na Namungo.

Kocha msaidizi wa Mtibwa, Awadh Juma akizungumzia mchezo huo alisema wamejipanga kupata ushindi dhidi ya Yanga huku akirusha dongo gizani kwa wapinzani wake ukiona timu inalia na majeruhi hiyo itakuwa haijajipanga.

“Tupo vizuri, maandalizi yetu yamekwenda vizuri, tumefanya marekebisho kwa vijana, timu ipo tayari kutafuta ushindi kwenye mchezo wa kesho, tunajua tunakutana na timu yenye wachezaji wazoefu, hiyo kuhusu majeruhi ukiona timu inalia hivyo ujue haijajipanga,” alisema Awadh.