ZPL kuongezwa thamani kuitangaza Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema lengo la kuwekeza fedha nyingi kwenye sekta ya michezo ni kuhakikisha inakuwa msingi unaowezesha kukuza vipaji, kuongeza ushindani na kuifikisha Zanzibar katika viwango vya kimataifa.

Hayo yalielezwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi wakati alipokutana na uongozi wa taasisi ya Tanzania Securities Limited, Ikulu mjini Zanzibar.

Alisema Serikali hiyo ina dhamira ya dhati kuona michezo inaimarika na kupata maendeleo makubwa, huku akisisitiza kuwa iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha azma hiyo.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kuimarisha miundombinu ya viwanja vya michezo pamoja na kuanzisha akademi mbalimbali ili kuinua sekta ya michezo nchini,” alisema Dk Mwinyi.

Aidha, ameihakikishia taasisi hiyo kuwa serikali itaendelea kushirikiana nayo kukuza mpira wa miguu ikiwemo kuongeza thamani za klabu, kuimarisha maslahi ya wachezaji na kuwawezesha kutambua thamani yao katika soko la michezo. Alisema, ni muhimu kwa taasisi hiyo kuzijengea uwezo klabu na vyama vya michezo, hususani kwenye masuala ya uongozi na uendeshaji.

Dk Mwinyi amebainisha kuwa changamoto ya uongozi duni imekuwa ikikwamisha maendeleo ya sekta hiyo, hususani soka.

“Tunahitaji vilabu vyenye uongozi imara, unaozingatia misingi ya kitaaluma na uwajibikaji ili kufikia malengo ya kuikuza michezo yetu,” alisema Dk Mwinyi.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo, George Shumbusho alisema taasisi hiyo imejipanga kuiongeza thamani Ligi Kuu ya Zanzibar ili iwe chombo muhimu cha kuitangaza Zanzibar katika jukwaa la kimataifa.

Alifafanua kuwa pamoja na hilo, taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha mfuko maalumu wa uwekezaji katika mpira wa miguu utakaosaidia kuimarisha klabu pamoja na kuendeleza vipaji vya wachezaji. Vilevile, Shumbusho aliongezea kuwa watawajengea wachezaji uelewa wa masuala ya fedha ili kuwaandaa vyema kwa maisha yao baada ya kustaafu soka.

Alisema, hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha wanakuwa na maisha bora hata baada ya kumaliza kucheza, sambamba na kuchangia maendeleo ya sekta ya michezo.