MISIMU mitano ya Ligi Kuu Bara imekuwa ikitawaliwa na mastaa wakubwa kutoka nje ya nchi wakitwaa kiatu cha ufungaji bora mara tatu, lakini kwa sasa inaonekana mambo yanaweza kubadilika na mzani ukawa sawa.
Kwa sasa staa kutoka DR Congo, Fabrice Ngoy anayechezea Namungo ndiye kinara wa mabao akiwa ameshafunga manane, lakini bado takwimu zinaonyesha kuwa ana kazi ngumu kuhakikisha anakomaa kwenye msimamo hadi mwisho.
Hata hivyo, anaonekana kuwa na nyakati bora kwa kuwa mastaa kutoka kwenye timu kubwa za Simba, Yanga na Azam viwango vyao vya kufunga mabao vimeshuka kwa kasi kubwa, huku wengine wakisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale.
Mastaa wa zamani wa Simba na Yanga wameangalia mwenendo wa msimu huu ulivyo mgumu, hivyo kufikiwa ama kuvunja rekodi ya kinara wa mabao wa msimu huu, wakisema itategemeana na ushindani wao dhidi ya mabeki, lakini jina la Feisal Salum ‘Fei Toto’ linaonekana kuwa kwenye mawazo ya wengi.
Msimu wa 2024/2025 kinara wa mabao alikuwa kiungo wa Simba, Jean Ahoua ambaye alifunga mabao 16 msimu mzima, huku nafasi ya pili ikishikwa na Clement Mzize wa Yanga ambaye alimaliza msimu akiwa na mabao 14 na asisti tano.
Kwa msimu wa 2023/24 aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ndiye aliyeibuka kinara wa mabao akifunga 21, huku mzawa Feisal Salum ‘Fei Toto akishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 19.
Wakati 2022/23 kinara alikuwa mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibanzokiza na straika wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele wote wakimaliza na mabao 17, huku 2021/22 kinara alikuwa George Mpole kipindi yupo Geita Gold alipomaliza na mabao 17 nyuma yake akiwa Mayele ambaye alifunga 16.
Aliyekuwa nahodha wa Simba, John Bocco aliyehamishia majukumu yake ya kuinoa timu B ya klabu hiyo ndiye alikuwa kinara wa mabao 16 msimu wa 2020/21.
Wakizungumza mastaa mbalimbali wa soka la Tanzania wamesema kila mchezaji amekuwa akionyesha ubora wake, hivyo lolote linaweza kutokea, lakini kama mabeki wataendelea kukaza, basi ni ngumu kwa mfungaji kufikia idadi ya mabao yaliyofungwa msimu uliopita.
Nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi ambaye sasa ni kocha wa timu ya wanawake (Simba Queens), alisema mwenendo wa Ligi Kuu ulivyo msimu huu itategemeana na ushindani wa washambuliaji na mabeki, kuvunja rekodi ya mabao aliyomaliza nayo Ahoua msimu uliopita.
Msimu wa 2010/11, Mgosi aliyeweka rekodi ya kuibuka mfungaji bora akiwa na mabao 18 alisema: “Kama anayeongoza ana mabao manane inategemeana na wastani wake wa kufunga mabao. Lakini, kama anacheza mechi nne ama tatu bila kufunga anaweza akaibuka mwingine akawa mfungaji bora. Mfano Fei Toto akiamua kukaza buti kwa namna alivyo na mwendelezo wa kiwango, basi unaweza kuwa mwaka wake.”
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Meddie Kagere ambaye ndani ya misimu minne aliyoichezea timu hiyo alifunga jumla ya mabao 65 na kuibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu mara mbili mfululizo, alisema siyo msimu rahisi, lakini kila kitu kinawezekana ndani ya uwanja.
Misimu ambayo Kagere aliibuka kinara wa mabao ni 2018-2019 alipofunga 23 na 2019-2020 akitupia kambani mabao 22, alisema: “Kutabiri mfungaji bora atakuwa na mabao mangapi inategemeana na juhudi zake mwenyewe, ila wanacheza kwa kiwango cha juu pia naona hawajapishana sana mgeni na mzawa katika msimamo wa mabao, wanachotakiwa wakaze buti kama ilivyokuwa kwa Mpole na Mayele.”
Kagere ambaye misimu mingine ya 2020-2021 alifunga mabao 13 na 2021-2022 mabao 7, aliongeza: “Ninachokiamini penye ushindani ndipo penye mafanikio ya hali ya juu, kwa namna ninavyofuatilia baadhi ya mechi ninapopata muda naona utakuwa na mabao mengi.”
Mwenye rekodi yake iliyodumu kwa miaka 27 straika wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao 26 mwaka 1999 alisema: “Kufunga mabao zaidi ya 16 ama kutofikiwa inategemeana na ushindani wa wachezaji wenyewe, ila ligi ni ngumu na ina ushindani, jambo la msingi inahitaji mwendelezo wa kiwango.”|