BODI ya Ligi Zanzibar (ZBL), inatarajia kufanya marekebisho ya kanuni za mashindano ili kuruhusu timu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kutumia viwanja vya Bara kwa ajili ya mechi.
Hatua hiyo inalenga kuongeza ushindani wa ligi hiyo na kutoa fursa kwa wachezaji wa Zanzibar kuonekana zaidi na kutambulika kwenye soka la Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Issa Kassim Ali alisema endapo mabadiliko yatapitishwa yatafungua milango kwa wachezaji wa Zanzibar.
“Bodi inakusudia kufanya mabadiliko ya kanuni za mashindano ili kuruhusu baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar kutumia viwanja vilivyopo Tanzania Bara kama vyao vya nyumbani,” alisema.
Alisema hatua hiyo itaongeza uzoefu kwa wachezaji wa Zanzibar pamoja na kuwapa nafasi ya kuonekana kwenye soka la kitaifa. Alisema, wazo hilo limetokana baada ya kutambua kuwa uwezo wa wachezaji wa Zanzibar huonekana zaidi wanaposhiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano, jambo linaloonesha kuwa wana vipaji vinavyoweza kuendelezwa zaidi.
Alisema kupitia mpango huo, wachezaji watacheza kwa ushindani hali itakayosaidia kukuza viwango na kuwapa nafasi ya kutambulika na wadau mbalimbali wa soka.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kucheza baadhi ya mechi Tanzania Bara hakutakuwa na athari kwa maendeleo ya Ligi ya Zanzibar bali ni hatua ya kuimarisha ushindani na kukuza vipaji vya vijana.
“Lengo letu ni kukuza vipaji vya vijana wa Zanzibar, hivyo hatua hii itakuwa fursa kwa wachezaji kuonekana na hata kupata soko la kucheza katika timu mbalimbali,” alisema.
Aliongeza kuwa, bodi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa soka katika kuhakikisha mageuzi hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu za mashindano. Wakati hayo yakiwa kwenye mchakato, tayari Ligi Kuu Tanzania Bara inaruhusu mechi zake kuchezwa Zanzibar na msimu huu Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga dhidi ya Simba imechezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, Machi Mosi, 2026.
