Katika maisha ya uhusiano wa kimapenzi, watu wengi hujikuta wakihangaika kulazimisha uhusiano ambao tayari umefika mwisho au hauna uhai tena.
Moja ya ukweli mgumu lakini muhimu kukubalika ni huu: ukiona mwenza wako hakutaki tena, mwache aende zake. Usilazimishe mapenzi.
Mapenzi ya kweli hayawezi kulazimishwa. Yanatoka moyoni kwa hiari, si kwa mashinikizo. Unapojikuta unapigania nafasi yako kwa mtu ambaye hataki kuwa na wewe, unapoteza muda, nguvu na heshima yako binafsi.
Mapenzi ya aina hiyo hukuletea maumivu ya kihisia, kukosa amani ya moyo na hata kuathiri afya yako ya akili.
Dalili za mtu ambaye hakutaki ni wazi. Anaacha kujali kuhusu wewe, hamthamini muda au hisia zako, mawasiliano yanapungua au yanakua ya shingo upande, na mara nyingine huonesha dhahiri kuwa anafurahia zaidi akiwa mbali na wewe. Wakati mwingine, hata kuomba muda wa kukaa peke yake, ni dalili kuwa anakosa furaha katika uhusiano huo.
Ni muhimu kufahamu kuwa wewe ni mtu wa thamani. Kama mtu hakutambui au hakuthamini, hilo halimaanishi wewe hufai.
Inamaanisha tu kuwa huyo si mtu sahihi kwako. Mapenzi ya kweli ni yale yanayolipa kwa pande zote mbili, mpenzi wako anapaswa kuwa mtu anayekuthamini, kukuonesha upendo, kukuheshimu, na kuwa tayari kupambana kwa ajili ya mahusiano yenu.
Kwa nini ulazimishe mapenzi?
Unapomlazimisha mtu abaki na wewe ilhali hataki, unajivunjia heshima yako mwenyewe. Unampa mamlaka ya kukudharau zaidi.
Kujaribu kulazimisha uhusiano wa upande mmoja kunaashiria kutojiitambua. Kama ungejua thamani yako, usingekubali kubembeleza mapenzi yasiyokuwepo.
Unafungia nafasi ya furaha ya kweli. Wakati unahangaika kumshikilia mtu asiye na mapenzi na wewe, unajifungia fursa ya kukutana na mtu anayekupenda kwa dhati.
Unaumiza moyo wako. Mapenzi ya kulazimisha huumiza zaidi ya kuachana. Maumivu ya kila siku, mashaka na huzuni haviwezi kuwa sehemu ya uhusiano wenye afya.
Kumbuka kuwa kuachilia ni ushindi, si kushindwa. Wengi huona kama kuachwa au kuachana ni ishara ya kushindwa, lakini kinyume chake ni kweli.
Kukubali kuachilia mtu ambaye hakutaki ni ishara ya ukomavu wa kihisia.
Inaonesha kuwa unajithamini, unajipenda na unajua kuwa upendo wa kweli hauhitaji kufuatwa kwa mateso.
Jifunze kujipenda kwanza. Mtu anayejipenda hawezi kukubali kudhalilishwa au kufanywa chaguo la pili.
Kujipenda kunakuwezesha kujua unachostahili na kukataa kilicho chini ya viwango vyako.
Hili ni somo muhimu hasa kwa wale ambao wamezama mno katika mapenzi hadi kusahau utu na thamani yao binafsi.
Kama mwenza wako amekuonesha wazi kuwa hakutaki, usijibebe kama tatizo.
Mwache aende zake kwa amani. Heshimu uamuzi wake, jikusanye upya, jipe muda wa kupona, na endelea mbele na maisha yako.
Huko mbele kuna nafasi mpya, kuna furaha mpya, na kuna mtu sahihi atakayekupenda kwa dhati bila kulazimishwa.
Mapenzi ya kweli hayana mateso kwani yanafariji, yanatibu, na yanaimarisha. Usilazimishe mapenzi; yakikataa, yaache yaende.
