Ukiwaona wanandoa wapya wakitembea kwa bashasha, nyuso zikiwa zimejaa matumaini na mioyo ikidunda kwa ahadi za kesho njema, ni rahisi kuvutiwa na uzuri wa mwanzo wao.
Lakini pia, si ajabu kwa wanandoa wakongwe, waliodumu katika taasisi ya ndoa kwa miongo kadhaa, kuwakazia macho kwa tabasamu lenye kumbukumbu nyingi, furaha, majaribu na ushindi wa safari ndefu.
Swali ni hili: je, kila upande unamwonaje mwenzake? Kwa uzoefu wa maisha, mara nyingi wanandoa wapya huwaonea huruma wanandoa wazee wakidhani wameshafika mwisho wa safari ilhali wao ndio wanaanza.
Nao wanandoa wakongwe, kwa hekima ya miaka, huwatazama wapya kwa jicho la tahadhari wakijua safari waliyoianza si rahisi kama inavyoonekana. Ndiyo mzunguko wa maisha. Lakini ndani ya tofauti hiyo ya kizazi, kuna darasa kubwa la kujifunza.
Wanandoa wapya ni sawa na majani mabichi; yanachanua kwa nguvu, yakipeperushwa na upepo wa matumaini.
Wanandoa wakongwe ni kama majani makavu; yamepitia jua na mvua, yameona misimu yote. Kuna methali isemayo: jani bichi lisicheke jani kavu, maana lilikuwa lilipo na linaelekea litakapofika. Hivyo ndivyo ilivyo katika ndoa.
Kwa wanandoa wapya, kufunga ndoa ni mwanzo wa ukurasa mpya. Ni wakati wa kusomana, kuzoeana, kujifunza kuvumiliana na kujenga misingi ya maisha ya pamoja.
Ndoto ni nyingi—kujenga familia, kupata watoto, kulea, kujitegemea na hatimaye kufikia uzee wakiwa pamoja. Huu ni wakati wa kuweka mawe ya msingi ya taswira ya kesho.
Lakini taswira hiyo haiwezi kujengwa hewani. Njia bora ya kuielewa kesho ni kuangalia jana. Wanandoa wakongwe wamepitia milima na mabonde ambayo wanandoa wapya wanayaona kwa mbali. Wamevuka changamoto za kiuchumi, misukosuko ya malezi, misuguano ya kimtazamo na hata mitihani ya kiafya. Leo wanajivunia si tu miaka waliyoishi pamoja, bali pia vizazi walivyovilea na busara waliyoikusanya.
Kwa wanandoa wakongwe, huu ni wakati wa tafakari na mavuno. Ni wakati wa kujivunia watoto waliowalea, wajukuu wanaowazunguka na historia waliyoijenga pamoja.
Lakini pia ni kipindi cha kukabiliana na uzee—miili kubadilika, afya kuyumba, kumbukumbu kufifia. Haya ni mambo ambayo wanandoa wapya wanaweza kuyaona, lakini wasiyape uzito wakidhani yapo mbali. Ukweli ni kwamba, safari yao inaelekea huko kama watadumu.
Kinachowatofautisha makundi haya mawili si thamani wala hadhi, bali ni wakati tu. Mzee wa leo alikuwa kijana wa jana; kijana wa leo ndiye mzee wa kesho. Wanandoa wapya ni wanandoa wakongwe wa baadaye, na wakongwe ni kumbukumbu hai ya mwanzo wa safari waliyoianza kwa bashasha kama ilivyo kwa wapya wa leo.
Hivyo basi, wanandoa wapya, mfungapo ndoa mkumbuke kuwa mnaingia darasani. Wanandoa wakongwe wako kwenye maktaba ya uzoefu.
Badala ya kuwatazama kwa jicho la huruma au dharau, watazameni kama walimu na rejea ya maisha ya ndoa. Ulizeni, sikilizeni na jifunzeni.
Na kwa wanandoa wakongwe, kumbukeni kuwakaribisha wapya kwa upendo na kuwapa hekima yenu bila kuwakatisha tamaa. Maisha ya ndoa ni safari ya pamoja ya vizazi tofauti, lakini lengo ni moja yaani kujenga, kudumu na kuacha alama njema.
Mwisho wa yote, ndoa si mbio za kasi bali ni safari ya masafa marefu. Mwanzo ni tamu, katikati kuna majaribu, na mwisho hujaa tafakari.
Hivyo, kila kundi limheshimu mwenzake. Maana ndani ya taswira ya mwenzako, unaiona sura yako ya jana, leo au kesho.
