Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameieleza Mahakama ya Rufani yuko katika hatari ya afya yake kuathirika zaidi kwa kushindwa kuhudhuria kliniki ya matibabu yake kutokana na kushikiliwa mahabusu kwa muda mrefu.
Hivyo, ameiomba Mahakama hiyo kulisikiliza kwa dharura shauri la mapitio lililofunguliwa mahakamani hapo na Jamhuri dhidi yake kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kuikatalia kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi ya uhaini inayomkabili, ambalo limesababisha usikilizwaji wa kesi hiyo kusimama kwa muda usiojulikana.
Amedai kama shauri hilo lisiposikilizwa na kuamuliwa haraka basi hali ya afya yake itazidi kuathirika kwa kuzidi kukosa huduma hizo za kiafya kutokana na kuendelea kushikiliwa mahabusu, hivyo kupata madhara ambayo hayataweza kurekebishika na kukwamisha haki kutendeka.
Lissu ameelezea hofu yake hiyo ya kuathirika kwa kukosa huduma za kiafya wakati alipowasilisha majibu yake ya maandishi dhidi ya hoja za Jamhuri katika shauri hilo la mapitio.
Katika majibu yake hayo pamoja na hati ya kiapo chake kinzani dhidi ya kiapo cha Jamhuri, pia Lissu ameambatanisha hati ya dharura akiomba shauri hilo lisikilizwe kwa dharura huku akibainisha sababu ni kukosa huduma za kiafya kwa kuendelea kushikiliwa mahabusu muda mrefu.
Katika hati hiyo ya dharura Lissu anadai anathibitisha kuwa shauri hilo linastahili kusikilizwa kama suala la dharura kwa sababu aliyoibanisha.
Ameikumbusha Mahakama Septemba 7, 2017 alinusurika katika jaribio la mauaji katika shambulizi la risasi mkoani Dodoma ambapo alipigwa risasi kadhaa mwilini mwake na kumsababishia majeraha makubwa na ya kudumu na kumuacha na changamoto kubwa endelevu za kiafya.
Lissu ameeleza kufuatia shambulizi hilo amekuwa chini ya uangalizi wa mara kwa mara wa kitabibu na amekuwa nikihudhuria kliniki kwa ajili ya matibabu na ufuatiliaji wa afya yake.
Hata hivyo, ameeleza kuwa kwa sasa yuko mahabusu tangu Aprili 9, 2025.
“Kutokana na kuendelea kushikiliwa kwangu, nimekosa miadi kadhaa ya matibabu iliyopangwa, jambo linaloweka afya yangu na kupona kwangu katika hatari kubwa,” ameeleza Lissu.
“Isipokuwa maombi haya yatasikilizwa na kuamuliwa kwa haraka, nitapata madhara makubwa yasiyorekebishika, na malengo ya haki yanaweza kukwamishwa.”
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania kuwa:-
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha… sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo), James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri na tayari mashahidi 15 kati ya 30 wanaotarajiwa wameshatoa ushahidi wao.
Februari 23, 2026, upande wa mashtaka ulieleza Mahakama kuwa, Februari 18, 2026 uliwasilisha mahakamani kwa njia ya mtandao, notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo chini ya kwa mujibu wa kifungu 308(1) cha CPA.
Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga alisema katika notisi hiyo wanaomba kuongeza ushahidi mpya katika ushahidi wa Kamishna Msaizidi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba kwani haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi, kwenye Mahakama ya ukabidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu,
Katuga alisema kuwa, notisi hiyo imeambatanishwa na kiini cha ushahidi huo ni kwamba, ACP Mahamba alikuwa ni kiongozi wa timu ya upelelezi wakati uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi.
Alibainisha kuwa, ushahidi huo umetambulika kwa upande wa mashtaka wakati wa maandalizi ya shahidi huyo Februari 16, 2026.
Hata hivyo, Lissu aliibua pingamizi akidai kuwa 308(1) cha CPA (kilichotumiwa na Jamhuri) kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Alieleza kuwa, ushahidi wa ACP Mahamba ambaye Jamhuri inataka kuuongeza ushahidi wake ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wake wa kuleta ushahidi mpya umeshafungwa.
Hata hivyo, akijibu hoja hizo Wakili Katuga alidai kuwa kifungu cha 308(1) cha CPA kinazungumzia notisi hiyo ya shahidi mpya au ushahidi wake ambao haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.
Lissu aliendelea kuipinga akisisitiza hoja zake za awali
Lissu alieleza kuwa, kosa analotuhumiwa lilifanyika Aprili 3, 2025, akashtakiwa Aprili 10, 2025 na kupelekwa mahabusu, lakini maelezo hayo ya nyongeza yanahusu kabla na baada ya uchaguzi.
Mahakama katika uamuzi wake Februari 24, 2026 ilikubaliana na hoja za pimgamizi la Lissu.
Akisoma uamuzi huo Jaji Ndunguru, alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 308 CPA, maelezo au ushahidi unaotolewa notisi, unapaswa uwe ule ambao wakati wa mwenendo kabidhi ulikuwepo, lakini haukusomwa na si ushahidi mpya ambao haukuwepo.
Alisema kuwa, wakati mwenendo kabidhi unafanyika ushahidi huu haukuwepo, basi notisi hiyo ya Jamhuri kuongeza ushahidi, inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA na akasema kuwa mahakama imeitupilia mbali.
Baada ya uamuzi huo ndipo Jamhuri ilipofungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude alieleza kuwa maombi hayo yanaungwa mkono na hati ya kiapo cha Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi iliyosainiwa siku hiyo Februari 24, 2026.
Alieleza kuwa, maombi hayo yalipokewa katika mifumo ya kieletroniki siku hiyo hiyo na kusajiliwa kama shauri la jinai la mapitio namba 7203216/2026.
Kutokana na hatua hiyo, Mahakama Kuu kama ilivyo utaratibu wa kisheria ililazimika kusimamisha mwenendo wa kesi hiyo kwa muda usiojulikana kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika shauri hilo la mapitio.
