Mabingwa Watetezi Pyramids Waaga CAFCL Kwa Maumivu

Global Publishers
March 22, 2026
0 Comments

Mabingwa watetezi wa CAF Champions League, Pyramids FC, wameaga rasmi michuano hiyo baada ya kutolewa na AS FAR Rabat kwa jumla ya mabao 3-2 katika hatua ya robo fainali.

Baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, Pyramids walishuka dimbani wakiwa na matumaini ya kusonga mbele, lakini walijikuta wakizidiwa mbinu na wapinzani wao katika mchezo wa marudiano uliomalizika kwa ushindi wa 2-1 kwa AS FAR Rabat.

AS FAR walitangulia kupata bao la mapema dakika ya 9 kupitia kwa Reda Slim, kabla ya kuongeza la pili dakika ya 54 likifungwa na Hrimat, mabao yaliyoipa timu hiyo udhibiti mkubwa wa mchezo.

Pyramids walijaribu kurejea mchezoni na kufanikiwa kupata bao dakika ya 63 kupitia kwa mshambuliaji wao Fiston Mayele, lakini juhudi zao hazikutosha kubadilisha matokeo.

Kwa ushindi huo, AS FAR Rabat wanatinga hatua ya nusu fainali ambapo watasubiri mshindi kati ya RS Berkane na Al Hilal Omdurman watakaokutana katika mchezo mwingine wa robo fainali.

Matokeo hayo yanaashiria mwisho wa safari kwa Pyramids FC katika utetezi wao wa taji, huku AS FAR wakionyesha ubora wao na dhamira ya kufanya makubwa zaidi katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.