Chelsea Yapokea Kipigo Kingine cha Aibu Dhidi ya Everton

Global Publishers
March 21, 2026
0 Comments

Mshambuliaji Beto ameibuka shujaa wa Everton FC baada ya kufunga mabao mawili muhimu yaliyoisaidia timu yake kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Chelsea FC katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Hill Dickinson.

Everton walionyesha ubora wao tangu dakika za mwanzo za mchezo huo, huku Beto akifungua ukurasa wa mabao dakika ya 33 kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Chelsea. Bao hilo liliwapa wenyeji kujiamini zaidi na kuendelea kulisakama lango la wapinzani wao.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ileile, na Beto akaongeza bao la pili dakika ya 62 akitumia vyema nafasi aliyopata ndani ya eneo la hatari. Chelsea walijaribu kujipanga na kurejea mchezoni, lakini walishindwa kabisa kupenya safu imara ya ulinzi ya Everton.

Dakika ya 76, Iliman Ndiaye alihitimisha karamu ya mabao kwa kuifungia Everton bao la tatu, lililozima kabisa matumaini ya Chelsea katika mchezo huo.

Matokeo hayo yanaifanya Everton kujikusanyia pointi muhimu, huku Chelsea ikiendelea kupitia kipindi kigumu baada ya kupokea kipigo kingine cha mabao 3-0, ikiwa ni mara yao ya pili mfululizo kufungwa kwa idadi hiyo ya mabao kufuatia kichapo dhidi ya Paris Saint-Germain katika michuano ya UEFA Champions League.

Hali hiyo inaongeza presha kwa kikosi cha Chelsea na benchi lake la ufundi, huku mashabiki wakianza kuhoji mwenendo wa timu hiyo baada ya matokeo mabaya ya hivi karibuni.