Global Publishers
March 21, 2026
0 Comments
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewapongeza viongozi wa dini nchini kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha maadili ya jamii na kudumisha mshikamano wa Taifa.
Akizungumza katika Baraza la Eid al-Fitr lililofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere Convention Centre jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema viongozi wa dini wamekuwa sauti ya matumaini na mwongozo muhimu kwa waumini hasa katika nyakati za changamoto za kijamii na kimaadili.

Amesema kupitia mafundisho yao, viongozi hao wamekuwa wakifariji waliokata tamaa, kuwatia moyo wenye dhiki na kuwaongoza wananchi katika misingi ya uadilifu, uvumilivu na kumcha Mungu. Hata hivyo, ameonya kuwa uhuru wa kuabudu haupaswi kutumiwa vibaya kwa kuchochea chuki, mgawanyiko au kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa.

Rais Samia amesisitiza kuwa dini inayojenga maadili mema huweka msingi imara wa amani na maendeleo ya taifa, akionya kuwa mmomonyoko wa maadili unaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu na kuibuka kwa vurugu.
Akizungumzia hali ya dunia, Rais Samia amesema licha ya migogoro na mivutano inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani, Tanzania imeendelea kubaki kisiwa cha amani. Hata hivyo, alionya kuwa si kila mtu anatamani kuona hali hiyo ikiendelea.




