Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaja mambo makuu matatu yanayokwamisha uchumi wa Zanzibar kukua kwa kasi na jinsi wanavyoyatafutia ufumbuzi yote kwa mpigo.
Mambo hayo ni ufinyu wa bandari, uhaba wa umeme na hifadhi ndogo ya mafuta.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 22, 2026 wakati akihutubia wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo itagharimu Dola za Marekani 300 milioni sawa na zaidi ya Sh770 bilioni.
Dk Mwinyi amesema licha ya uchumi wa Zanzibar kuendelea kukua vyema kati ya asilimia 7.1 hadi 7.4, unakabiliwa na changamoto hizo tatu ambazo zinarejesha nyuma.
“Uchumi wetu unakuwa kwa kasi nzuri kati ya asilimia 7.1 hadi asilimia 7.4, ni ukuaji mzuri wa uchumi, lakini kuna mambo matatu ni kikwazo cha ukuaji zaidi katika nchi yetu,” amesema Dk Mwinyi.
Kuhusu bandari, Dk Mwinyi amesema bandari ya Malindi ambayo ilijengwa mwaka 1920 ina msongamano mkubwa na haiwezi kupanuliwa hivyo meli zinakaa muda mrefu kabla ya kushusha kutokana na kuwa na ghati moja tena ndogo.
Akieleza tatizo la pili la uhaba wa umeme, amesema unaotoka Tanzania Bara hautoshi tena wanatakiwa kuwa na umeme wa ziada.
Mwonekano wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani itakavyokuwa ikikamilika Mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar
“Tatizo la tatu ni uwepo wa hifadhi ndogo ya mafuta, jambo ambalo linasababisha gharama za mafuta katika nchi yetu kuwa kubwa kwasababu mafuta yanayotoka nje lazima kwanza yashushwe Dar es Salaam au Tanga ndio yaje Unguja, hii inaongeza gharama,” amesema Dk Mwinyi.
“Serikali tumeamua kuyamaliza matatizo yote matatu kwa mpigo, tunajenga bandari hapa Mangapwani ambayo katika Afrika Mashariki nzima haitokuwepo kama hiyo inayoleta meli kubwa za kisasa ya kubeba makontena 15,000.
Amesema maana yake Zanzibar Mangapwani itakuwa ni kitovu cha biashara ya makontena katika Afrika Mashariki.
Kiongozi huyo wa nchi, amesema pia watajenga matangi ya kuhifadhia mafuta ambayo yanaweza kukidhi mahitaji ya ndani kwa zaidi ya miezi mitatu, zaidi ya lita milioni 60 (tani 60,000) za mafuta zitajengwa katika bandari hiyo kuhakikisha biashara ya mafuta inakuwa na gharama nafuu na kushusha nishati hiyo.
Katika eneo hilohilo la Mangapwani, utawekwa mitambo ya kuzalisha megawati 200 za umeme ili kwa miaka 15 ijayo wasiwe na changamoto ya umeme.
“Mambo haya matatu ndugu zangu yakikamilika, uchumi wa Zanzibar utapaa. Nataka nikuhakikishieni kwamba sasahivi uchumi wetu ni mkubwa katika Afrika Mashariki kuliko wenzetu wengi, lakini haya matatu sasa yatatupeleka katika uchumi mkubwa zaidi katika eneo lote la Afrika Mashariki,” amesema.
Amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano akisema Serikali inatambua bado inatakiwa kulipa fidia na kujenga nyumba kwa ajili ya kuwapa watu ili wakae kwenye mazingira mazuri zaidi.
“Hayo yote yatafanyika ili bandari iwe na ufanisi ili tusijenge bandari isiwe na miundombinu, nataka niwaahidi hapa, kila mtu atapata stahiki yake hakuna atakayedhulumiwa,” amesema
Akitoa taarifa za kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakari amesema mradi huo unagharimu Dola za Marekani 300 milioni sawa na Sh770 bilioni.
Amesema utekelezaji wake umeanza Septemba 2025 utachukua miaka mitatu hadi Septemba 2028 unatakiwa kukamilika.
Mwonekano wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani itakavyokuwa ikikamilika Mkoa wa Kaskazini Unguja Zanzibar
“Kutakuwa na ghati tatu kwa ujumla wake, ghati namba moja ina urefu wa mita 680 ikiwa na kina chenye urefu wa mita 20 na uwezo wa kuhudumia meli ya mzigo wa tani laki mbili ikiwa ni meli ya Kontena 15000 hadi 20,000 ambapo hakuna ghati Afrika Mashariki yenye uwezo kama huo.
“Hii ni bandari ya kisasa itajumuisha maeneo ya kuegesha meli kubwa, makontena, maeneo ya mizigo ya jumla, kituo cha mizigo (CFS), jengo la utawala, mfumo wa umeme wa kujitegemea na mifumo ya kisasa ya mawasiliano na usalama,” amesema.
Miundombinu hiyo itaifanya kuwa ya kipekee katika eneo hilo la Afrika Mashariki.
Amesema ghati nyingine mbili zitakuwa na urefu wa mita 217 hadi 220 na kina cha maji mita 15 zikiwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 30,000 na ghati dogo la kushushia magari zaidi ya mawili.
Pia, kutakuwa na maeneo ya makontena milimita za mraba 47,000 na sehemu za jumla ya mzigo mita za mraba 22,000.
Amesema maeneo hayo yatakuwa na uwezo wa kuhudumia makontena 200,000 na tani milioni moja za mizigo ya jumla kwa mwaka.
Katibu mkuu huyo, amesema Serikali imeshatenga eneo la ziada la utanuzi wa bandari hiyo hadi kufikia uwezo wa kuhudumia kontena milioni moja kwa mwaka.
“Tafiti zote muhimu ikiwamo utafiti wa udongo, mawimbi ya bahari, kina cha maji na mazingira zimekamilika, na kazi za awali tayari zimeanza ikiwamo usafishaji wa eneo, uchimbaji wa eneo la kuweka makontena na ujenzi wa kambi ya mradi, kiwanda cha zege na kazi hiyo imefikia asilimia 14.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Bandari (ZPC), Akif Ali amesema bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia mizigo meli za ndani na ‘transshipment port’ na katika awamu ya kwanza ya ujenzi itakuwa na jumla ya hekta 18 ardhini.
Amesema waliingia mkataba na kampuni ya China Harbour Ltd (HEC) mwaka 2025 kujenga bandari hiyo na wanatakiwa kukamilisha ujenzi huo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed amesema ujenzi wa bandari hiyo imewekwa alama nyingine kubwa katika visiwa hivyo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano na kuchangamkia fursa ziatakazopatikana kutokana na bandari hiyo.
“Bandari hii itakuwa mkombozi na kuimarisha uchumi wa mwananchi mmojammoja na taifa kwa ujumla wake,” amesema.
Amesema itakuza fursa za ajira itaunganisha mkoa wa Kaskazini na Zanzibar kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, Bai Yinzhan amesema watahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa huku akisema mradi huo utaleta tija na kupanua wigo wa uchumi kwa Wazanzibari.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni za mafuta, Lameck Hiliyai kutoka Puma amesema Serikali imeleta mabadiliko katika sekta hiyo kutokana na kuweka sera nzuri na kuongeza ushindani.
“Ushirikiano tunaoupata na mazingira bora ya biashara vinatupa amani kuendelea kuwekeza Zanzibar,” amesema.
