Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameeleza kwa kina sababu kuu zinazofanya Tanzania kuwa kitovu cha kimkakati kwa wawekezaji wa China na dunia kwa ujumla.
Waziri Kapinga, amesema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye Mkutano wa Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na China uliofanyika mjini Fuzhou, Fujian, leo Jumapili Machi 22, 2026.
Kapinga amewaeleza wajumbe na viongozi wa pande zote mbili kuwa, Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa kirafiki na wa karibu kwa zaidi ya nusu karne.
“Historia hii ya ushirikiano imejenga msingi thabiti wa kuaminiana na kutoa uhakika wa mazingira salama kwa uwekezaji,” amesema.
Akizungumzia hali ya uchumi, Kapinga amesema: “Tanzania imekuwa ikifuata sera thabiti za kiuchumi ambazo zimeiwezesha nchi kudumisha ukuaji wa wastani wa asilimia 7 kwa muongo mmoja uliopita, huku mfumuko wa bei ukibaki chini ya asilimia 3.3.”
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga (Kulia) akiwa na kiongozi wa China katika ziara yake ya kikazi iliyoanza nchini humo. Picha na Mtandao.
Amesema ukuaji huo wa uchumi unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika.
Aidha, Waziri Kapinga amesisitiza kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu wa kisiasa, hali inayowapa wawekezaji uhakika wa kulinda mitaji yao na kuendesha shughuli bila hofu ya misukosuko.
“Serikali imeweka sera na sheria rafiki kwa biashara na inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kila inapohitajika,” amesema.
Akieleza ukubwa wa soko, Kapinga amesema, Tanzania yenye watu takribani milioni 64, na kwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), inatoa fursa ya kufikia soko la zaidi ya watu milioni 500.
Pia, ametaja nafasi ya kijiografia ya Tanzania, inayopakana na nchi nane na bandari ya Dar es Salaam inayohudumia nchi sita zisizo na pwani, inaiweka Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda huu.
Kapinga pia ametaja nguvu kazi ya vijana kama rasilimali muhimu, akibainisha kuwa idadikubwa ya Watanzania ni vijana.
“Idadi kubwa ya Watanzania ni vijana wanaotafuta ajira, huku Serikali ikiwa imewekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu na mafunzo ya stadi za kazi. Hii ni faida kubwa kwa wawekezaji wanaohitaji wafanyakazi wenye ujuzi na ari ya kazi,” amesema.
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga, akiwa na viongozi mbalimbali wa Tanzania na China katika ziara yake ya kikazi iliyoanza nchini humo. Picha na Mtandao.
Akitaja takwimu za miradi, Kapinga amesema kuwa kati ya mwaka 2021 hadi Desemba 2025, miradi 876 kutoka China ilisajiliwa nchini Tanzania, ikiwa na thamani ya dola Sh8.861 bilioni na kuajiri watu 146,250 katika sekta za kilimo, viwanda, nishati, huduma na usafirishaji.
Kapinga ametaja miradi mikubwa kama ile ya Keda Tanzania Ceramics, Kinglion Investment, Goodwill Ceramic na EACLC Limited, pamoja na uwekezaji wa Fujian Hexingwang Industry katika sekta ya chuma na mradi wa sponge iron kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).
Mbali na hayo, pia ameeleza miradi mikubwa ya kimkakati kama Bagamoyo Eco Maritime City na Kwala Industrial Park inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kimataifa cha biashara, viwanda na huduma za baharini.
“Serikali imeweka motisha za kipekee kwa wawekezaji, ikiwamo msamaha wa kodi ya kampuni kwa miaka 10, punguzo la ushuru wa forodha na msamaha wa VAT katika maeneo maalum ya kiuchumi,” amesema.
Katika mkutano huo, Waziri Kapinga amewaalika wawekezaji wa China si tu kuwekeza, bali pia kutambua uzuri wa Tanzania kupitia vivutio vya utalii kama Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Zanzibar na Ngorongoro.
“Tanzania si tu mahali pa biashara, bali ni safari ya kipekee yenye uzuri, usalama na ukarimu wa watu wake. Karibuni Tanzania,” amesema.