Uingereza kutegemea mifumo ya Marekani kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Iran

Uingereza italazimika kutegemea mifumo ya ulinzi wa makombora ya Marekani iliyoko Ulaya iwapo Iran itafanya shambulizi la roketi dhidi ya nchi hiyo, sawa na lile lililojaribiwa kulenga kisiwa cha Diego Garcia mwishoni mwa wiki hii.

Onyo hilo limetolewa baada ya Iran kurusha makombora mawili ya balistiki usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita kuelekea kambi iliyoko Bahari ya Hindi, ambayo inaendeshwa kwa pamoja na Marekani na Uingereza.

Kisiwa hicho kiko umbali wa maili 2,360 kutoka Iran, mbali zaidi ya maili 1,240 zilizokuwa zikiaminika kuwa ndio kiwango cha juu cha uwezo wa kufika wa makombora ya utawala huo.

Hali hiyo inaashiria kuwa miji kama Paris, iliyo umbali wa maili 2,609, na hata London – maili 2,750 – inaweza kuwa ndani ya wigo wa mashambulizi ya Iran iwapo, kama baadhi ya wachambuzi wanavyohofia, nchi hiyo itatumia teknolojia yake ya kurusha vyombo vya anga aina ya Simorgh kuongeza uwezo wa makombora yake.

Kituo cha Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) Akrotiri kilichoko Cyprus kiko umbali wa maili 1,000 tu kutoka Tehran. Wakati huohuo, Israel imeonya kuwa kombora jipya la Iran linaweza kufikia bara la Ulaya.

Mkuu wa Majeshi ya Israel (IDF), Luteni Jenerali Eyal Zamir alisema katika video iliyotolewa Jumamosi usiku kuwa: “Iran ilirusha kombora la masafa marefu la hatua mbili lenye uwezo wa kufika kilomita 4,000 kuelekea shabaha ya Marekani katika kisiwa cha Diego Garcia.

“Makombora hayo hayakulenga Israel. Masafa yake yanafikia miji mikuu ya Ulaya. Berlin, Paris na Roma zote ziko katika hatari ya moja kwa moja.” Baadaye, IDF iliongeza kuwa hata London iko ndani ya umbali huo.

Steve Prest, aliyewahi kuwa kamodori wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza, alisema: “Makombora ya balistiki kimsingi ni roketi za anga. Hurushwa, hupaa juu sana angani na kisha hushuka kwa kasi kubwa. Ukiwa na programu ya anga, basi pia una programu ya makombora ya balistiki.”

Katika tukio la shambulizi la aina hiyo, wataalamu wa ulinzi wanasema Uingereza italazimika kutegemea mifumo ya Marekani ya SM-3 iliyoko Ulaya Mashariki, au makombora ya Patriot yanayotumiwa na Ujerumani ili kuyazuia makombora hayo.

Jaribio la kushambulia Diego Garcia limekuja wakati Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer ameongeza ruhusa kwa Marekani kutumia kambi za kijeshi za Uingereza kufanya mashambulizi katika Mlango Bahari wa Hormuz, kwa lengo la kulinda usafirishaji wa meli dhidi ya mashambulizi ya Iran.

Hata hivyo, hakuna kati ya makombora mawili yaliyolenga Diego Garcia yaliyofikia shabaha, ambapo moja linaaminika kudunguliwa na mfumo wa SM-3 kutoka meli ya kivita ya Marekani, huku jingine likishindwa likiwa angani.