Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia askari mgambo watatu kwa tuhuma za mauaji ya Rashid Nyandonga (31), fundi simu na mkazi wa Bugando Jeshini, Wilaya ya Nyamagana mkoani humo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, iliyotolewa leo, Jumapili, Machi 22, 2026, imeeleza kuwa mgambo hao walikamatwa usiku wa Machi 20 baada ya tukio hilo na wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na kifo cha Nyandonga.
Kamanda Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea saa 12:45 jioni katika mtaa wa Mission, eneo la Sahara, Kata ya Pamba, ambapo askari hao walimtilia shaka Nyandonga kuwa anauza dawa za kulevya aina ya mirungi.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Zongoli Makongoro (38), askari mgambo wa Kata ya Mahina, mkazi wa Bugarika, Genge Mwita (45), askari mgambo wa Kata ya Igogo, mkazi wa mtaa wa Kambarage na Ibrahim Mwita (25), askari mgambo wa Kata ya Pamba, mkazi wa Bugando Mission, wote wakazi wa Wilaya ya Nyamagana.
“Jioni hiyo ya tukio, askari hao walikuwa eneo la Mission walimtilia shaka marehemu kuwa alikuwa anauza dawa za kulevya aina ya mirungi. Kutokana na mashaka hayo, walianza kumfuatilia,” amesema Mutafungwa.
Amesema baada ya kuanza kumfuatilia, Nyandonga alikimbia kukwepa kukamatwa na askari hao wakaanza kumkimbiza na kufanikiwa kumkamata umbali mfupi, na kumkuta akiwa na gramu 50 za mirungi.
Amesema baada ya kukamatwa, marehemu (Nyandonga) alikuwa akihema kwa nguvu na kuonesha dalili za kuishiwa nguvu, hali iliyowalazimu mgambo kumpeleka Hospitali ya Sekou Toure kwa huduma za matibabu.
“Wakati akiendelea kupatiwa matibabu hapo hospitalini ndipo zilipatikana taarifa kutoka kwenye mamlaka ya hospitali kwamba mtu huyo alikuwa amefariki dunia. Kutokana na mazingira hayo ya ukamataji, askari hao mgambo wote walikamatwa na Jeshi la Polisi usiku huo huo kuhusiana na tukio hilo,” ameeleza.
Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa wakati wa ukamataji, askari hao walikuwa peke yao na hakuna operesheni ya Jeshi la Polisi iliyohusisha askari mgambo katika eneo hilo.
“Uchunguzi wa kitaalamu umefanyika Machi 21, 2026, ambapo mwili wa marehemu umefanyiwa post mortem (uchunguzi wa kitabibu), wakiwepo ndugu na jamaa zake hapo hospitalini, na kisha mwili huo kuchukuliwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya mazishi,” ameongeza.
Amesema Jeshi la Polisi linahakikisha uchunguzi wa kina unaendelea, na endapo ushahidi utaonesha watuhumiwa wamehusika na mauaji hayo, watawajibika kwa mujibu wa sheria.
Aidha, ameonya askari mgambo kuzingatia taratibu za ukamataji salama wanapotekeleza majukumu yao na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
