Morogoro. Makamu wa Rais Balozi, Dk Emmanuel Nchimbi ameitaka menejimenti ya Wizara ya Maji kujenga ushirikiano na sekta binafsi ili kushughulikia changamoto za upatikanaji na upotevu wa maji, ili dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua “mama ndoo kichwani” iweze kutekelezeka.
Dk Nchimbi ameyasema hayo leo wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Ameongeza kuwa Dira ya Maendeleo ya Taifa inaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050, idadi ya watu nchini itafikia takribani milioni 118, mara mbili ya idadi ya sasa, na ongezeko hilo linahitaji kuhakikisha upatikanaji wa chakula, huduma za afya, pamoja na maji.
“Lazima tufanye uwekezaji wa kimkakati wa pamoja na sekta binafsi katika kuvilinda na kuvipanua vyanzo vya maji na pamoja na hilo lazima kufunga MITA za kieletroniki za malipo ya kabla (pre paid) za kudhibiti upotevu wa maji,” amesema Dk Nchimbi.
Akizungumzia kauli mbiu ya Wiki ya Maji ambayo ni ‘maji na jinsia” Dk Nchimbi amesema wanawake wamekuwa na mchango mkubwa wa ama shida ama raha za maji kwa kuwa asilimia 90 ya wanaotafuta maji ni wanawake ambao wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi za kiusalama wakati wa kutafuta maji.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi za maji, lakini Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano kwa kuwa na miradi mingi ya maji.
Makamu wa Rais Balozi, Dk Emanuel Nchimbi akimwagia maji mche wa mti alioupanda kwenye chanzo cha maji Cha bwawa la mindu ikiwa ni ishara ya kutunza na kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, wa kulia kwake ni Waziri wa maji Jumaa Aweso na wa kwanza ni Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mussa Hassan Zungu. Picha Hamida Shariff
“Kupitia sera ya maji ya 2022 Tanzania imepata mafanikio ambapo asilimia 92.5 ya Watanzania waishio mijini wanapata maji safi na salama na asilimia 85.2 ya Watanzania waishio vijijini nao wamepata maji safi na salama huku vijiji 10758 navyo vimefikiwa na maji safi na salama.
Ameongeza kuwa mpaka sasa vijiji 1575 ndio vimebaki kuunganishiwa maji safi na salama hata hivyo tayari wataalamu wanaendelea na kazi,” amesema Dk Nchimbi.
Akitoa taarifa ya hali ya maji nchini, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema kuwa Rais Samia ameiheshimisha wizara na menejimenti yake yote kwa kufanikisha utoaji wa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji, inayolenga kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji.
Aweso ameahidi yeye binafsi pamoja na menejimenti ya wizara hiyo kutokuwa kikwazo cha kuwapelekea maji wananchi.
Kwa upande wa sekta binafsi, Mhandisi Ngwisa Mpembe, ambaye ni mwakilishi wa rasilimali za maji, ameipongeza Serikali kwa kuimarisha sekta ya maji nchini na kuboresha mfumo wa kodi.
Mwakilishi huyo wa sekta binafsi ameahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya maji inaendelea kuboreshwa.
Amesema kuwa mpaka sasa, sekta binafsi imewekeza kiasi cha Sh1.2 trilioni kwenye sekta ya maji, huku ikichangia pia katika usafi wa mazingira.
Naye Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amesema kuwa mita za ujazo milioni 60 za maji ya Mto Ruvu zinapotea baharini kwa sababu hakuna mahali pa kuhifadhi.
Hata hivyo, amebainisha kuwa Wizara ya Maji kwa sasa imeleta matumaini katika kushughulikia changamoto hiyo.
“Tunashukuru Wizara ya Maji kwa kupokea maelekezo ya Bunge na kwamba Bunge litaunga mkono juhudi zote za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji,” amesema Zungu.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema kuwa mafuriko yamekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa mkoa huo, hasa ifikapo Machi na Aprili.
Muonekano wa bwawa la mindu ambalo ni chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi zaidi ya asilimia 85 wa Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
Amebainisha kuwa ujenzi wa mabwawa utasaidia kupunguza changamoto hiyo, huku akishukuru Serikali kwa kupeleka miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh400 bilioni mkoani humo.
“Moro ndio mkoa wenye vyanzo vingi vya maji hivyo tunaahidi kuwa walinzi wa vyanzo hivyo vya maji na tayari tumeshaweka mikakati ikiwa ni pamoja na kuwapa wananchi njia ambayo itahifadhi mazingira na vyanzo vya maji,” amesema Malima.