M/kiti CCM aonya maneno matamu kwenye shida ya maji

Dar es Salaam. Katika kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Joseph Masunga amewataka wasimamizi wa sekta ya maji kupunguza maneno mengi na michakato mirefu isiyo na majibu ya haraka kwa kero za maji zinazowakabili wananchi.

Amesema wakati mwingine viongozi wanaosimamia sekta ya maji hutoa maelezo yanayoweza kuwaburudisha wasikilizaji, lakini yasiyotoa suluhisho la changamoto halisi za upatikanaji wa maji.

“Hayajibu shida ya mabomba kutotoa maji au kutoa hewa badala ya maji. Sasa unapotoa maelezo ya kutetea hali iliyopo, watu wanakusikiliza lakini wanakuambia hayo maneno baki nayo, sisi tunataka maji,” amesema Masunga.

Masunga ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 22, 2026, wakati akiwasilisha salamu za chama katika Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani na Kilele cha Wiki ya Maji yaliyofanyika mkoani Morogoro. Mgeni rasmi ni Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Amesema licha ya changamoto zilizopo, hali ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Morogoro inaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na jitihada za Serikali na wadau wa sekta hiyo.

Kufanyika kwa maadhimisho haya duniani kila mwaka ni kutokana na azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN), linalotaka nchi wanachama kuadhimisha siku hiyo kila ifikapo Machi 22.

Maadhimisho haya yanafanyika yakiongozwa na kaulimbiu  ya: “Maji na Jinsia,” inayolenga kuonesha uhusiano uliopo kati ya rasilimali za maji na usawa wa kijinsia katika jamii.

Akizungumzia kaulimbiu hiyo, Mjumbe wa Bodi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ngwisa Mpembe amesema inakumbusha maendeleo katika sekta ya maji lazima yawe jumuishi na yanayozingatia makundi yote katika jamii.

“Kwa mtazamo wa sekta binafsi, kuwekeza katika sekta ya maji ni kuwekeza katika usawa wa kijinsia, bila kuhakikisha upatikanaji rahisi wa maji, jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi hazitafikiwa kikamilifu,” amesema Mpembe.

Ameongeza kuwa, sekta binafsi ipo tayari kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta ya maji nchini, akiahidi kushirikiana na Wizara ya Maji katika ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Akielezea hali ya upatikanaji wa maji mkoani Morogoro, Mkuu wa mkoa huo, Adam Malima amesema kuna miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh400 bilioni inayotekelezwa ndani ya mkoa huo.

Amesema Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) peke yake ulipatiwa Sh130 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji vijijini na mijini, kuna miradi mingine yenye thamani ya Sh300 bilioni inayotekelezwa katika wilaya mbalimbali za mkoa huo

“Morogoro bado ni chanzo kikubwa cha maji kwa mkoa wenyewe, pamoja na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Hata hivyo, changamoto tunazokutana nazo zinatokana na athari za mazingira,” amesema Malima.

Ameongeza mkoa huo umejipanga kulinda mazingira kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, huku ukihamasisha tafiti na uhifadhi wa uoto wa asili ili kulinda vyanzo vya maji.

Kwa upande mwingine, Malima amesema ili kupunguza uharibifu wa mazingira, ni muhimu kuwapa wananchi mbinu mbadala za kiuchumi.

Amesema Morogoro imejipanga kuwa kinara wa kilimo cha mazao ya biashara kama parachichi, karafuu na kakao, hasa katika maeneo ambayo awali wananchi walijihusisha na ukataji miti kwa ajili ya mkaa.

Makamu wa Rais Balozi, Dk Emanuel Nchimbi akimwagia maji mche wa mti alioupanda kwenye chanzo cha maji Cha bwawa la mindu ikiwa ni ishara ya kutunza na kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, wa kulia kwake ni Waziri wa maji Jumaa Aweso na wa kwanza ni Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mussa Hassan Zungu. Picha Hamida Shariff

Akizungumza katika kilele hicho, Dk Nchimbi amesema ukosefu wa maji umekuwa changamoto kubwa duniani lakini Tanznaia imekuwa mfano wa kuigwa wa upatikanaji wa maji safi na salama duniani kote.

Dk Nchimbi ameelekeza wizara na taasisi zote za umma nchini kujenga mtandao wa ushirikiano katika kukabili, kutatua na kurekebisha changamoto za maji, ili dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwa na nchi iliyoondokana na changamoto ya maji safi inafanikiwa.

Ili pia mpango huo wa Rais Samia ufanikiwe pia, Dk Nchimbi amewataka wadau wote wa maendeleo kuona wajibukatika kulinda vyanzo vya maji ili kuwa na nchi yenye utosheleu wa maji itakayoridhishwa kwa vijazi vijavyo.

“Nitoe wito kwa wizara zote, taasisi zote za umma kujenga mtandao wa ushirikiano katika kukabili, kutatua na kurekebisha changamoto za maji ili dhamira ya Rais ya kuwa na nchi ya kuondokana na changamoto yam ahi inafanikiwa,” amesema.

Pia, Dk Nchimbi katika amelekezo yake, ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha ufungaji wa mita katika maeneo mbalimbali nchini ili kuepusha upotevu wa maji na kuwafanya wanaotumia huduma hiyo wanawajibika kulingana na matumizi yao.

Magizo mengine ya Dk Nchimbi ni wizara hiyo kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kukuza sekta ya maji na wasitegemee chanzo kimoja ili kukuza sekta hiyo.

Mbali na hayo Dk Nchimbi ametaka kufanyiwa kazi kwa mifumo ya maji taka ili kuepusha majisafi kuchanganyika na majitaka.

Akitoa wasilisho kuhusu usalama wa maji na mwelekeo wa sekta hiyo kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Robert Sande amesema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi za maji ikiwamo mito, maziwa, mabwawa na maji ya chini ya ardhi.

Ametaja Mto Rufiji kuwa ndio mto mkubwa zaidi nchini, wenye uwezo wa kukusanya maji kiasi cha mita za ujazo bilioni 28 kwa mwaka, huku Mto Ruvuma ukiwa ndio mto mrefu zaidi kwa urefu wa takribani kilomita 800.

Aidha, amesema Tanzania ina maziwa makubwa matatu ambayo ni Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa, ambayo yanahifadhi sehemu kubwa ya majisafi duniani.

Kuhusu mabwawa, amesema nchi ina zaidi ya mabwawa 650, huku makubwa yakiwa ni Nyumba ya Mungu, Mtera na Julius Nyerere. Mabwawa hayo yanahifadhi takribani mita za ujazo bilioni 40 za maji, ambapo asilimia kubwa ya maji hayo ipo katika mabwawa makubwa matatu.

Muonekano wa bwawa la mindu ambalo ni chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi zaidi ya asilimia 85 wa Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Palamagamba Kabudi amesema Serikali imejipanga kudhibiti mafuriko katika Mkoa wa Morogoro ili kuyageuza kuwa fursa ya maendeleo badala ya kuwa chanzo cha hasara.

Amesema mpango huo unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti maji ya mafuriko katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mabonde ya mito inayopita katika Wilaya ya Kilosa na maeneo jirani.

“Tukiweka mifumo madhubuti ya udhibiti wa mafuriko katika maeneo kama Kilosa, Mkondoa na maeneo mengine, pamoja na ujenzi wa mabwawa, hatua hiyo itasaidia kudhibiti athari za mafuriko,” amesema.

Ameongeza ni wajibu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira, ikiwamo milima na vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tuache kuharibu mazingira, adhabu ya uharibifu wa mazingira tunaiona hapa hapa duniani kupitia majanga mbalimbali,” amesema.