Timu kutathmini majengo ya Serikali yasiyotumika Dar

Dar es Salaam. Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, amesema timu maalumu ya kutathmini majengo ya Serikali yasiyotumika jijini Dar es Salaam inaendelea na kazi hiyo.

Timu hiyo iliundwa kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyoyatoa Januari 22, 2026, alipotembelea mji wa Serikali, Mtumba mkoani Dodoma, akimtaka Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi, amuelekeze Katibu Mkuu wake kuunda kikosi kazi kitakachobaini majengo yote ya Serikali yasiyotumika katika jiji hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumapili, Machi 22, 2026, Dk Yonazi amesema mchakato wa tathmini unaendelea na utakapokamilika, taarifa itawasilishwa kwa Waziri Mkuu kwa hatua zaidi.

“Timu ya tathmini bado iko kazini na ikikamilisha jukumu lake, taarifa itawasilishwa kwa Waziri Mkuu kama ilivyoelekezwa,” amesema Dk Yonazi.

Awali, akitoa maelekezo hayo, Dk Mwigulu alikazia umuhimu wa kubaini majengo yasiyotumika ili yaweze kutolewa kwa taasisi nyingine za Serikali zinazopanga, huku Serikali ikiwa na rasilimali hizo bila matumizi.

“Tathmini hii itatusaidia kufahamu majengo yaliyo wazi ili yaweze kutumika na taasisi nyingine badala ya kuendelea kupanga,” amesema.

Pia, amesema Dodoma ndiyo makao makuu rasmi ya nchi na si kambi ya muda, akibainisha kuwa, Serikali haitarajii kuwa na makao makuu mawili yanayofanya kazi kwa wakati mmoja.

Alisema taasisi zote ambazo tayari zimekamilisha uhamisho wa ofisi zao kwenda Dodoma zinapaswa kuachana na majengo wanayoyamiliki Dar es Salaam ili yaweze kutumiwa na taasisi nyingine zinazohitaji nafasi.

“Tunataka shughuli zote za Serikali zifanyike katika makao makuu ya nchi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha maamuzi muhimu yanapatikana kwa wakati,” amesema.

Amesema hatua hiyo inalenga kuboresha matumizi ya rasilimali za Serikali pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kupitia makao makuu ya nchi, Dodoma.