Bagamoyo. Pamoja na jitihada za Serikali za kujenga shule za sekondari katika kila kata nchini, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba baadhi ya wanafunzi bado wanatembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi nyumbani.
Shule hizo, pamoja na nyingine, ziliwekwa ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania, hasa walioko vijijini, anapata fursa ya elimu ya sekondari karibu na makazi yake.
Hata hivyo, Mwananchi imebaini kuwa katika baadhi ya maeneo nchini, baadhi ya wanafunzi bado wanatembea umbali mrefu wa kilometa 7 hadi 15 ili kufika shule.
Hali hii ni kinyume na Mkakati wa Ujenzi na Matengenezo ya Shule (SCMS) wa mwaka 2019, unaoainisha kwamba mtoto anayesoma elimu ya awali hatakiwi kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 1.5, unaokadiriwa kuchukua takribani dakika 25.
Aidha, mwanafunzi wa shule ya msingi hatakiwi kutembea zaidi ya kilometa tatu, ambazo zinakadiriwa kuchukua dakika 40, huku mwanafunzi wa sekondari akipendekezwa kutembea umbali usiozidi kilometa tano kwenda shule na kurudi nyumbani, jambo linalokadiriwa kuchukua chini ya saa moja.
Hata Sura ya 3.8 ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, imeweka wazi wajibu wa Serikali kushirikiana na wadau kuhakikisha mazingira salama na rafiki kwa upatikanaji wa elimu na mafunzo.
Mwanzoni mwa Mei 2025, Taasisi ya Msichana Initiative ilifanya ziara katika kata ya Fukayosi, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kugawa baiskeli 50 kwa wanafunzi wa kike wanaopitia changamoto ya kutembea umbali mrefu.
Wakati wa hafla ya ugawaji baiskeli, wakisoma risala kwa mgeni rasmi, Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Bagamoyo, Alois Kaziyareli, wanafunzi walieleza jinsi changamoto ya kutembea umbali mrefu inavyowaathiri katika masomo yao.
Wanafunzi hao walisema kwamba baadhi yao wanalazimika kutembea umbali wa kilometa saba hadi 15 kutokana na shule kuwa mbali na maeneo wanayoishi.
Walisema changamoto hiyo inaathiri ujifunzaji wao, kwani hufika shule wakiwa wamechelewa na wamechoka.
Hali hiyo ilisukuma Mwananchi kufanya uchunguzi, ili kubaini kiini cha tatizo hilo na athari zake kwa wanafunzi.
Uchunguzi wa Mwananchi katika baadhi ya vijiji vya kata ya Fukayosi, ikiwemo Mkenge, Kidomole na Mwavi, vilivyopo katika Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani, umebaini kuwa baadhi ya wanafunzi, hasa wa sekondari, hutumia zaidi ya saa moja wakitembea kwenda shule.
Katika kata hiyo ambayo ina shule ya sekondari moja, baadhi ya wanafunzi hutembea takribani kilometa saba hadi 15 kwenda shule na kurudi nyumbani.
Hama hama ya wakazi, ukubwa wa maeneo ya kiutawala, gharama za bweni, changamoto za miundombinu na upungufu wa usafiri kwa wanafunzi ni baadhi ya sababu zilizobainika kuchangia hali hiyo.
Wanafunzi walioanza kidato cha kwanza mwaka 2023 katika Shule ya Sekondari Fukayosi wanatarajiwa kumaliza mwaka 2026, lakini hali ni tofauti kwa Asha Salum (18), ambaye alilazimika kuacha masomo akiwa kidato cha kwanza.
Kutembea umbali mrefu kwenda shule na hali duni ya kiuchumi ya familia ni baadhi ya sababu zilizokwamisha ndoto yake ya kuwa mwanasheria, baada ya kusoma kidato cha kwanza kwa miezi sita pekee.
Asha, mkazi wa Kijiji cha Mkenge kilichoko takribani kilometa 11 kutoka barabara kuu, anaeleza kuwa hakuna usafiri wa daladala, wanakijiji hutumia bodaboda kwa gharama ya Sh5,000 hadi Sh7,000 kulingana na umbali wa kwenda shule.
Safari yake ya kila siku ilihusisha kutembea zaidi ya kilometa 15 au kutumia bodaboda, hali iliyosababisha uchovu na kuchelewa masomo.
Mwanafunzi mwingine wa kidato cha tatu kutoka Kijiji cha Mwavi anasema kuwa ili kufika shuleni kwa wakati, lazima aondoke mapema sana, kwani umbali wa nyumbani hadi kituo cha daladala ni takribani kilometa tatu, na baada ya kushuka anatembea tena kilometa mbili hadi shule.
Changamoto hiyo ya umbali inasababisha kuchelewa mara kwa mara na uchovu, hali inayodhuru ujifunzaji wao kila siku.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka Kijiji cha Mwavi, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, anasema umbali wa shule unaathiri sana ujifunzaji wake.
Kila siku analazimika kuamka saa 11 alfajiri kuanza maandalizi na kuanza safari ya kwenda shule kati ya saa 11:45 hadi 12:00.
“Kutoka nyumbani hadi kituo cha daladala ni takribani kilometa tatu, lakini wakati mwingine lazima nitembee kilometa tano hadi sita. Kama napanda daladala, napaswa kutembea zaidi ya kilometa mbili hadi kufika shule,” anasema.
Anabainisha kuwa uchovu kutokana na kutembea umbali mrefu mara nyingi humfanya achelewe vipindi vya asubuhi, jambo linalokwamisha ujifunzaji wake, kwani mara nyingine anakuta vipindi vimeanza kufundishwa.
Kukataliwa na wasafirishaji
Pamoja na baadhi ya wanafunzi kutembea umbali mrefu, uchunguzi umebaini pia changamoto ya baadhi ya daladala kukataa kuwasafirisha.
Hali hiyo huwafanya wengine kuchagua kutembea, ili kuwahi shule na kurudi nyumbani.
Wanafunzi wanasema mara nyingine wanabaguliwa kwa sababu ya nauli ndogo ya Sh200 wanayolipa, na baadhi hawana fedha za usafiri kutokana na uchumi duni wa familia, jambo linaloongeza ugumu wa kufika shule.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka Kidomole anasema anaanza safari yake kwa kuamka saa 11:30 alfajiri ili kuhakikisha anafika kituoni hadi saa 12:00, lakini wakati mwingine hukataliwa kuingia daladala, hivyo kuchelewa shule.
Wanafunzi wengine huomba lifti kwa bodaboda au watu wenye magari binafsi, lakini msaada huo si wa kudumu.
“Baadhi ya bodaboda wanakupa lifti siku kadhaa, kisha wanakutongoza, ukiwakataa wanaacha kukusaidia. Hii inatuweka hatarini kupata vishawishi,” anasema mwanafunzi huyo.
Wazazi wanasema umbali wa shule unawalazimisha watoto kurudi nyumbani wakiwa wamechoka, jambo linalosababisha baadhi yao kutaka kuacha shule.
Wanaeleza pia kuwa barabara zenye miti na majani marefu huwapa hofu, huku gharama za nauli zikizidi kuathiri uchumi wa familia.
Christina John, mkazi wa Kijiji cha Mkenge, anasema baadhi ya wazazi huwapangishia watoto vyumba (geto) karibu na shule kwa Sh15,000 hadi Sh20,000, ingawa uangalizi ni mdogo.
Abdallah Juma, mkazi wa Kijiji cha Kidomole na mlezi wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Fukayosi, anasema alitarajia ujenzi wa bweni utapunguza changamoto ya usafiri, lakini hali imekuwa tofauti.
Anabainisha kuwa gharama ya bweni ya Sh770,000 kwa mwaka ni kubwa kutokana na kipato chake kidogo.
“Nimechagua kumpangia mtoto wangu chumba (geto) jirani na shule, ambacho nalipia Sh15,000 kila mwezi, ili imsaidie kufika shuleni kwa wakati,” anasema.
Mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Fukayosi, ambaye hakutaka kutajwa jina, anasema wamekuwa wakiwaonya wazazi dhidi ya kuwapangia vyumba watoto wao na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa bweni.
Anasema shule imeruhusu kulipa kwa awamu zaidi ya tano, lakini mwamko wa wazazi kubadilisha mpangilio bado ni mdogo.
Akizungumza na Mwananchi, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa anasema Serikali inahakikisha kila kata nchini inapata shule ya sekondari.
Hata hivyo, baadhi ya halmashauri zina maeneo makubwa na changamoto za kijiografia, jambo linalofanya baadhi ya kata kuhitaji shule hadi tatu.
“Kuna kata ambazo hadi sasa zina shule tatu ili kupunguza umbali wanafunzi wanatakiwa kutembea kila siku,” anasema Kwagilwa, akisisitiza juhudi za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa elimu karibu na kila mtoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, Shauri Selenda, akizungumza na Mwananchi anasema kwa upande wa Fukayosi, moja ya sababu inayochangia uwepo wa changamoto hiyo ni asili ya jamii inayoishi katika kata hiyo, ambao ni wakulima na wafugaji.
“Kama unavyojua, wakulima na wafugaji si watu wanaopendelea kuishi eneo moja, hivyo makazi yao yametawanyika,” anasema.
Hata hivyo, anasema licha ya changamoto hiyo, Serikali kwa kushirikiana na halmashauri hiyo inaendelea kuhakikisha wanasogeza shule karibu zaidi na wananchi walio wengi.
“Hadi sasa tumefanikiwa kujenga shule mbili shikizi za msingi katika kata hiyo. Pia, katika Kijiji cha Mkenge kuna shule ya sekondari inajengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na halmashauri,” anasema Selenda.
Anasema Serikali kupitia halmashauri hiyo inaendelea kujenga shule shikizi katika maeneo mengine ambayo wakazi wake wako mbali na shule mama.
Anasema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu katika halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkenge, Xavery Mtunze, anakiri kuwa na taarifa ya baadhi ya watoto kupitia changamoto ya kutembea umbali mrefu.
Anasema kijiji hicho kina shule moja ya msingi ya Serikali ya Mkenge ambayo wanafunzi zaidi ya 50 huhitimu darasa la saba kila mwaka na huchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Fukayosi.
“Shule hiyo ipo umbali wa zaidi ya kilometa 15, na gharama ya bweni katika shule hiyo ni Sh770,000 kwa mwaka, gharama ambayo baadhi ya wazazi wamekuwa wakieleza kushindwa kulipa,” anasema.
Anasema ameshapokea kesi kadhaa za watoto kuacha shule na baadhi ya wazazi kuwataka watoto kujifelisha kwa makusudi darasa la saba kwa kuwa hawana uwezo wa kumudu gharama za kuwapeleka shule.
Anasema sababu ya wazazi kuchukua hatua hiyo ni uoga wa kukamatwa kwa kushindwa kumpeleka mtoto shule, hivyo wanaingia makubaliano na watoto wao kufanya vibaya ili wasifaulu.
Diwani wa Kata ya Fukayosi, Mrisho Some, anasema wameanza mchakato wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkenge kwa ushirikiano na wananchi na Halmashauri ya Bagamoyo.
“Tayari tuna ekari 21.7, kati ya hizo 10 zimehakikiwa na wazazi, na tumeanza kupeleka vifaa vya ujenzi, ikiwemo matofali na saruji. Tunatarajia kuanza kuchimba msingi hivi karibuni,” anasema.
Kuhusu malalamiko ya gharama kubwa za bweni katika Shule ya Sekondari Fukayosi, anasema hajawahi kupokea kero rasmi kutoka kwa wananchi.
“Nimeshafanya vikao zaidi ya vitano katika kata, lakini sijapokea malalamiko haya, labda wanalalamika pembeni, nitayafuatilia zaidi,” anasema.
