Katika toleo la jana, katika mfululizo wa simulizi ya mauaji ya mtoto Timotheo Mhulila (miaka 4 na miezi 6), tulikuletea utetezi wa mshtakiwa, Joseph Mhulila, ambaye ni baba mzazi, akisema hafahamu kama mwanaye ni marehemu.
Tulikuletea pia mawasilisho ya mwisho ya mawakili wa pande mbili, kila mmoja akivutia upande wake, lakini leo tunakuletea uchambuzi wa ushahidi na hukumu aliyoitoa Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama Kuu Iringa.
Kuhusu swali la kama mtoto Timotheo alikufa kifo kisicho cha kawaida, Jaji alisema ushahidi unaonresha kuwa mshtakiwa alikuwa na utamaduni wa kumchukua mtoto kutoka kwa mama yake, Daima Hongoli, kila Ijumaa, kisha humrudisha jioni ya Jumapili.
Alisema Machi 28, 2025, kama ilivyo ada, mshtakiwa alimchukua mtoto, lakini hakumrudisha Machi 30, 2025 na alitoa visingizio mbalimbali.
Jioni ya Aprili 12, 2025, mshtakiwa akamjulisha mzazi mwenzake kuwa mtoto amepotea na hajui alipo, lakini Mei 6, 2025, alikiri mbele ya mashahidi wa 5 na 8 wa mashtaka kuwa mtoto hakuwa amepotea, bali amemuua.
Kwamba baada ya kumuua, alimkatakata vipande vidogo vidogo na kuvitupa chooni, kisha akamwaga maji ili kuvisukuma viende kwenye shimo la choo, ni yeye aliyewapeleka makachero wa polisi katika chumba alichopanga.
Huko nako, mshtakiwa alikiri mbele ya mashahidi namba 3, 4, 5, 8, 9 na 12 wa Jamhuri, na aliwaonesha chumba alichokitumia kumuua mtoto wake na choo alichokitumia kutupa mwili, na kilipovunjwa, vipande hivyo vilipatikana.
Miongoni mwa vipande vilivyopatikana ni viungo vya binadamu, mifupa ya miguu na mikono, mifupa ya shavu, meno, mbavu na vidole, na uchunguzi wa vinasaba (DNA) ulithibitisha kuwa ni vya marehemu, hivyo alikufa kifo kisicho cha asili.
Je, mshtakiwa ndiye mhusika?
Jaji alisema swali la pili ambalo mahakama ina wajibu wa kulijibu ni iwapo mshtakiwa aliyepo mbele ya mahakama ndiye aliyesababisha kifo hicho.
Kulingana na Jaji, katika kesi hiyo hakuna mtu aliyeshuhudia mshtakiwa akimuua marehemu, hivyo kesi ya upande wa mashtaka imeegemea ushahidi wa mazingira kuthibitisha kuwa ni mshtakiwa pekee na hakuna mtu mwingine aliyefanya mauaji.
Jaji alisema Jamhuri ilitegemea kanuni ya mshtakiwa kuwa ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu, maelezo yake ya ungamo, maungamo ya mdomo, ripoti ya DNA na matendo ya mshtakiwa kabla na baada ya tukio.
Katika utetezi wake kortini, mshtakiwa alikubali ndiye mtu wa mwisho kuwa na marehemu akiwa hai, na kwamba anaamini hajafariki, akieleza kuwa aliachana naye Aprili 12, 2025 alipokwenda naye katika hoteli ya Igwana.
Jaji alisema ingawa mshtakiwa alijaribu kueleza namna alivyoachana na marehemu, lakini maelezo yake yanatia mashaka, kwani hakueleza alikwenda hapo saa ngapi na kwa nini alimwacha mtoto mdogo nje ya hoteli alipoingia ndani.
“Maelezo ya mshtakiwa hayakutosheleza kumfanya aondolewe katika mazingira yaliyosababisha kutoweka kwa marehemu,” alisema Jaji an kuongeza kuwa ushahidi mwingine mzito ni maelezo yake ya ungamo ya maandishi na ya mdomo.
Jaji alisema ni msimamo wa sheria kuwa maungamo yanayosababisha kupatikana kwa ushahidi unaohusiana na kosa la jinai yanakubalika, na kwamba inafahamika kuwa mshtakiwa anayekiri kutenda kosa ni shahidi bora katika kesi.
Hata hivyo, Jaji alisema maelezo yake ya onyo yaliyopokelewa kama kielelezo, hakuna ubishi kuwa mshtakiwa hakusaini cheti kuonesha kuwa alisoma maelezo hayo, hivyo yanafanya maelezo hayo yasiwe na maana yoyote mahakamani.
Upande wa utetezi ulidai ukusanyaji, utunzaji na usafirishaji wa sampuli za DNA haukuwa sahihi, hoja ambayo Jaji alikubaliana nayo kuwa kuna uwezekano sampuli zilizochukuliwa eneo la tukio zikawa siyo zile zilizopelekwa kwa mkemia.
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikana kuishi mtaa wa Lukosi, akakana kuwa mpangaji wa nyumba ya shahidi wa 4, alikanusha kumfahamu shahidi wa 3 na wa 4, na akakanusha pia kuwapeleka polisi hadi chumba alichomuulia mtoto wake.
“Alikubali tu kwamba ni kweli marehemu ni mtoto wake aliyezaa na shahidi wa kwanza (Daima), na kwamba alimchukua Machi 28, 2025 na kwamba alipotea Aprili 12, 2025, na anaamini mwanaye hajafariki,” alisema Jaji Mwipopo na kuongeza:
“Mshtakiwa alikana kukiri kumuua marehemu wala kuonesha mahali alipomuulia, kumkatakata vipande na kuponda mifupa na kutupa vipande hivyo katika choo na kisha kuflashi (kumwaga maji ili viende shimoni).”
Hata hivyo, Jaji alisema ushahidi wa mashahidi namba 3, 4, 5, 8 na 9 unaeleza kuwa mshtakiwa alikiri mbele yao kumuua marehemu na kuwapeleka eneo la tukio na kuwaonesha choo alichokitumia kutupa mabaki ya mwili wa marehemu.
“Maungamo ya mdomo ndiyo yaliyosababisha kupatikana kwa mabaki hayo. Maungamo hayo yalikuwa kwa mapana kiasi kwamba yalitoa hadi sababu ya kwa nini mabaki ya mwili ule yalipita katika choo,” alisema Jaji.
“Kwa ujumla niliwaona mashahidi wa Jamhuri wakitoa ushahidi. Naona wote wanaaminika na sioni sababu za kutowaamini. Hakuna kitu chochote kinachoonesha mashahidi hao walikuwa na sababu yoyote ya kumsingizia.”
“Ushahidi wa utetezi wa mshtakiwa ulishindwa kuibua mashaka juu ya ushahidi wa upande wa mashitaka,” alisema Jaji, na kusema ipo hoja ya utetezi kuwa tarehe halisi aliyouawa marehemu haijulikani, na pia ushahidi ulikuwa na mkanganyiko.
“Kwamba katika kesi ya sasa, hakuna uhakika ni lini marehemu aliuawa kama ilivyoelezwa na wakili wa utetezi. Hata maelezo ya kosa katika taarifa ya kosa hilo yanaonyesha hivyo,” alieleza Jaji wakati akichambua ushahidi huo.
Jaji alisema sababu ni kwamba ushahidi katika kesi hiyo ni wa mazingira, kwani hakuna mtu yeyote aliyeshuhudia wakati mshtakiwa akifanya mauaji hayo.
“Kwa ushahidi wa jumla, nimeridhika kwamba ni mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha Timotheo Mhulila na si mtu mwingine. Naona kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana naye (marehemu) na kukiri kwa mdomo vilithibitisha bila shaka kuwa ni mtuhumiwa aliyemuua marehemu na si mtu mwingine,” alisema Jaji Mwipopo.
Swali la mwisho ambalo Jaji alisema mahakama ina wajibu wa kulijibu ni iwapo mtuhumiwa alimuua marehemu kwa nia ovu.
Jaji alisema nia ovu inachukuliwa kuthibitishwa na ushahidi unaothibitisha nia ya kusababisha kifo au kumdhuru mtu yeyote, iwe mtu huyo ndiye aliyeuawa au la, chini ya kifungu 200(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyorejewa mwaka 2023.
Akirejea msimamo wa kisheria katika kesi namba 150 ya mwaka 1994 katika Mahakama ya Rufaa kati ya Enock Kipera dhidi ya Jamhuri, majaji walisema kwa kawaida mshambuliaji hawezi kutangaza nia yake ya kusababisha kifo au kudhuru mwili.
Ili kuthibitisha nia hiyo, vipo vigezo vinavyoangaliwa ambavyo ni pamoja na aina na ukubwa wa silaha iliyotumika, nguvu iliyotumika, maeneo yaliyoshambuliwa, idadi ya mapigo, aina ya majeraha na matamshi ya mshitakiwa.
Katika kesi hiyo, Jaji alisema hakuna shahidi aliyeshuhudia mshtakiwa akifanya mauaji, bali mashahidi namba 5, 8 na 12 walieleza kuwa mshtakiwa alikiri mbele yao na kuwaeleza hadi sababu ya kwa nini aliamua kumuua mtoto wake.
“Mashahidi hao walisema alikiri mbele yao kuwa alimuua marehemu kwa kuwa alitamani pesa baada ya kusikia kuwa akipeleka baadhi ya viungo vya marehemu kwa mganga, basi mganga huyo atamtajirisha,” alisema Jaji Mwipopo.
“Akaamua kumuua, akamkata vipande vidogo vidogo na kuponda mifupa katika vipande vidogo na kuvitupa chooni na kumwaga maji ili viende. Mshtakiwa alitakiwa kufahamu kwamba kitendo alichofanya kingesababisha kifo cha marehemu.”
Jaji akasema matendo ya mshtakiwa pale alipojaribu kuficha ukweli wa mauaji kwa kutunga hadithi kwamba marehemu amepotea au kutoweka, yalimfanya aridhike kuwa alimuua akiwa na nia ovu.
Akahitimisha kwa kusema kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya mshitakiwa bila kuacha mashaka, hivyo anamtia hatiani kwa kosa hilo.
Baada ya kutiwa hatiani, mawakili wa Serikali, Mwakalinga na Mwakiborwa, waliieleza mahakama kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, hivyo itumie kifungu 197 cha kanuni ya adhabu kumpa adhabu anayostahili.
Kwa upande wake, wakili Mwakasage, aliyemtetea mshtakiwa, alisema Ibara ya 14 ya Katiba ya Tanzania inasema kila mtu ana haki ya kuishi, hivyo aliiomba mahakama isimhukumu kifo kwa sababu alimuua kutokana na imani za kichawi.
Jaji Mwipopo, akitamka adhabu, alisema ingawa wakili Mwakasage amenukuu kifungu hicho cha Katiba, kwa sheria za sasa hakuna nafasi ya kupunguziwa adhabu ya kifo kwa kosa la kuua kwa kukusudia chini ya vifungu 196 na 197.
Kwa msingi huo, Jaji alisema kwa kuegemea kifungu 26(1) na 197 cha Kanuni ya Adhabu na kifungu 341(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), anamhukumu Joseph Mhulila kunyongwa hadi kufa.
