YANGA ilirejea nyumbani jana kwa mafungu ikitokea Mkoani Dodoma ilikokwenda kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kutengeneza sare nyingine ya tano msimu huu lakini matokeo hayo yameibua presha kubwa kwa kocha wa timu hiyo Pedro Goncalves.
Presha kubwa ya Pedro ni kwamba Yanga ikiwa chini yake haijapoteza mchezo wowote lakini kwenye sare tano ambazo imezipata, nne ni wakati kikosi hicho kikiwa chini yake.
Kilichotibua zaidi ni baada ya mabosi wa klabu hiyo kuona kiwango cha timu yao kinaendelea kuporomoka taratibu, kuliko kuimarika sambamba na viwango vya wachezaji wengi kushuka.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema mabosi wa timu hiyo walitarajiwa kukutana kwa dharula jana mchana kujadili mwenendo wa timu yao lakini hapohapo wakataka kupata ripoti kutoka kwa Pedro ambayo ndio inaweza kumnusuru au kugeuzwa kitanzi kwa kocha huyo raia wa Ureno.
“Mtu sahihi wa kutupa kwanza majibu ya kwanini timu yetu imefika hapa ni kocha (Pedro), tutakutana naye lakini kwanza sisi wenyewe tutatangulia kukutana kwanza leo (jana mchana),tujadiliane kuhusu hili,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya Yanga.
“Baadaye ndio tutakutana na huyu kocha tumsikilize. Unajua ni ukweli kwamba timu yetu imeshuka sana. Yanga haitakiwi kuzoeleka hivi na tukisema tubaki kuangalia tunaweza kupotea zaidi. Kwenye haya mapumziko ya mechi za kalenda ya Fifa tunataka kubadilisha mambo.”
Pia, inaelezwa kwamba sio Pedro peke yake ambaye atakuwa kwenye presha kubwa, ambapo inaweza pia kumkumba kocha wa mazoezi ya viungo, Chyna Mokaila, ambaye bado kazi yake haijakubalika ndani ya kikosi hicho.
Kufuatia taarifa hizo Mwanaspoti lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, Rodgers Gumbo ambaye alithibitisha uongozi wao kumtaka Pedro kuwapa ripoti ya haraka kwenye mechi ambazo ameiongoza timu hiyo.
“Nikweli hatufurahii namna ya matokeo ambayo tumeyapata sasa, haya sio malengo ya klabu yetu lakini kila sehemu kuna utaratibu wake. Tumemtaka kocha atupe kwaza ripoti yake haraka, tunataka kujua kwanini tumefika hapa tulipo,” alisema Gumbo.
“Tukishapata ripoti uongozi utakaa na kuipima na baadaye tutakaa naye sasa kocha kujadiliana juu ya yale ambayo yatatoka kwenye tathimini ya ripoti yake, wakati huu tunawaomba mashabiki wetu watulie tunataka kuitumia hii breki ya mechi za timu za taifa kupambana kurekebisha mambo.”
Ndani ya mechi 16 ambazo Yanga imecheza msimu huu kwenye ligi, Pedro amehusika kwenye michezo 13 ambapo katika hizo ameshinda michezo tisa akitoa sare nne zikiwemo tatu mfululizo huku akiwa hajapoteza mchezo wowote.
Yanga bado inaongoza kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 38 baada ya kucheza mechi 16 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 29 ikiwa nafasi ya pili, matajiri hao wa Chamazi wakiwa na pungufu ya mchezo mmoja wakati Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 28, huku Wekundu hao wakiwa na pungufu ya michezo mitatu.
