KIKOSI cha Simba jana kilikuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, jijini, Dar es Salaam, kucheza dhidi ya TRA United, huku kiungo mpya wa timu hiyo, Kelvin Nashon, akiingiza zaidi ya Sh230 milioni, ili kukamilisha dili hilo.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu, ni ya raundi ya pili, baada ya ile ya kwanza iliyopangwa kufanyika Machi 14, 2026, Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini, Arusha, kushindwa kuchezwa kutokana na uwanja huo kujaa maji yaliyotokana na mvua kubwa.
Wakati miamba hiyo ikichuana katika mechi hiyo kali na ya kusisimua, tayari mabosi wa Simba wameanza hesabu mapema kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027, ambapo tayari imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Pamba Jiji, Kelvin Nashon.
Nashon anayeichezea Pamba Jiji, amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia Simba kwa msimu ujao wa 2026-2027, ambapo dili hilo la kiungo huyo mkabaji, limewagharimu mabosi wa kikosi hicho zaidi ya Sh230 milioni kukamilika.
Chanzo cha ndani kutoka ndani ya Simba, kimeliambia Mwanaspoti, kiungo huyo atapata kiasi cha Sh200 milioni ambazo ni za usajili wake (A signing-on fee), huku Sh30 milioni zilizobakia ni za kununulia gari lake kwa ajili ya matembezi binafsi.
Mtoa taarifa huyo, aliliambia Mwanaspoti makubaliano hayo bado hayajajulikana ni ya aina gani ya gari atakalotaka nyota huyo, ingawa, thamani yake ni kuanzia Sh30 milioni, ambazo mabosi wa kikosi hicho tayari wameshakubaliana na suala hilo.
Mwanaspoti linatambua Nashon aliyewindwa na vigogo wa soka nchini kwa muda mrefu, kwa sasa amekamilisha taratibu zote za kujiunga na Simba, ambapo ataanza kuivaa rasmi jezi ya timu hiyo ya mitaa ya Msimbazi kuanzia msimu ujao wa 2026-2027.
Usajili wa nyota huyo, ulianza kuibuka mapema kabla ya mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Pamba Jiji dhidi ya Simba ambayo ilipigwa, Machi 19, 2026, Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini, Mwanza na miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Katika mechi hiyo, Simba ilianza kutangulia kupata bao kupitia kwa nyota wa timu hiyo, Alain Anicet Oura, dakika ya 33, ingawa, kiungo, James Mwashinga, aliisawazishia Pamba, baada ya kupiga ‘Frii-Kiki’ kali dakika ya 36, nje ya eneo la 18.
Mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kutokana na ushindani uliokuwepo, ilidhihirisha wazi nyota huyo kujiunga na Simba, baada ya kushindwa kucheza bila ya sababu zozote za msingi, huku ikielezwa ilikuwa ni mkakati wa kukamilisha dili hilo.
Nashon aliyewahi kufanya majaribio, Venda Football Academy iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza, Afrika ya Kusini, akiwa Geita Gold, alihitajika pia na Simba, tangu mwaka 2022, bila ya mafanikio, ingawa, kwa sasa dili hilo limetiki.
Kabla ya kuichezea Pamba Jiji, kiungo huyo aliyefunga mabao mawili ya Ligi Kuu msimu huu, alikuwa Singida Black Stars, ingawa, kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, ilimlazimu kutolewa kwa mkopo, ili akapate timu nyingine ya kuchezea.
Nashon ambaye kwa sasa mkataba wake na Singida Black Stars, unafikia mwishoni mwa msimu huu, atajiunga na Simba akiwa ni mchezaji huru, jambo linaloipa nafasi kikosi hicho cha Msimbazi kuipata saini yake mapema kabla usajili haujafunguliwa.