KOCHA wa Mbeya City, Mecky Maxime amesema anahitaji kulifanyia kazi zaidi eneo la saikolojia kwa wachezaji wake ili waweze kuwa na utulivu wanapokuwa uwanjani.
Mecky aLIkabidhiwa Mbeya City hivi karibuni na imeonekana kutokuwa na matokea mazuri uwanjani kwenye michezo yake iliyocheza kwa sasa ikiwa katika nafasi ya 14 na pointi 13 imecheza jumla ya mechi 16 ikishinda tatu, sare nne na kupoteza tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars na Mtibwa Sugar alisema kuwa katika soka la kisasa, nguvu ya akili ni muhimu sawa na maandalizi ya kimwili na kiufundi, hivyo anataka kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa imara kiakili.
Alieleza kuwa, kumekuwa na presha kwa baadhi ya wachezaji hasa pale matokeo yanapokuwa hayaji kama ilivyotarajiwa, jambo linaloweza kuathiri kiwango chao uwanjani.
“Kupitia mazoezi maalumu ya kisaikolojia, natarajia kuwajenga wachezaji kuwa na utulivu na kujiamini zaidi wanapokutana na changamoto ndani ya mchezo.
“Sambamba na hilo, nataka kila mchezaji aelewe kuwa mafanikio yanahitaji subira na nidhamu, hivyo hawapaswi kukata tamaa mapema.
“Unajua matokeo mazuri hayaji kwa haraka bali ni mchakato unaohitaji juhudi za pamoja na kuamini kile wanachokifanya hivyo natamani kuona wakibadilika kifikra na kuwa na mtazamo chanya hata wanapokutana na nyakati ngumu.”
Mbeya City imetoka kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Fountain Gate 0-1 na Singida Black Stars iliwachezeshea kipigo cha mabao 1-4 na sasa itakuwa kwenye mapumziko hadi mwanzoni mwa mwezi ujao.
