Pointi 27 kufunga hesabu za Uhamiaji

KOCHA Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh, amesema licha ya kuwepo ugumu wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026, lakini sio sababu ya kuacha kupigania malengo yao.

Alisema kwa hatua ambayo imeshafikia Uhamiaji ya kuwa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo kilichobaki ni kuongeza bidii na kuvuna pointi kati ya 25 hadi 27.

Alisema Uhamiaji inaendelea kuimarika na ipo tayari kuziangusha timu zenye uzoefu ili kupambania malengo kwani kila mchezo ni muhimu kwao.

“Ingawa ligi ni ngumu hususani kwa mechi 10 za mwisho lakini kwa ilipofikia ni kuzidisha bidii ili kuhakikisha timu zenye uzoefu tunaziangusha,” alisema.

Alisema, timu hiyo inalazimika kuilinda nafasi iliyopo kwa sasa kisha kupigana kuelekea nafasi za juu kwenye ligi.

Alisema, lengo la kupambana huko ni kutafuta nafasi ya ushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, hivyo juhudi hizo zina malengo mapana kwa baadaye.

Kocha Abdul alisema timu hiyo inaanza mazoezi yake leo Jumatatu, baada ya kusimama kwa ligi hiyo kwa ajili ya kupisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao tayari umemalizika.

Timu hiyo imecheza mechi 20 za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, kati ya hizo  imeshinda 11, sare tatu, imepoteza sita na kuvuna alama 36 ikiwa nafasi ya nne tofauti ya pointi mbili na kinara wa ligi hiyo.