Amnyonyesha mtoto uume akiusaka utajiri, Polisi yasema…

Tabora. Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia msanii wa filamu mkoani humo, Ibrahim Kitundu (18) kwa tuhuma za kumnyonyesha uume wake mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita ili kukamilisha sharti la mganga la kupata mafanikio ya kazi zake za sanaa.

Akizungumzia tukio hilo jana Jumapili, Machi 22, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,  Richard Abwao alisema, “Tunamshikilia kijana Ibrahim kwa tuhuma za kunyonyesha uume mtoto mdogo kwa sababu za kutaka utajiri, mahojiano yanaendelea ili kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.”

Amesema mbinu aliyoitumia ni kumlaghai kwa juisi na biskuti na kumpeleka kwenye studio za kuingiza nyimbo akafunga mlango na kumlazimisha mtoto huyo amnyonye uume wake tukio ambalo alifanikiwa.

Aliongeza baada ya kitendo hicho mtoto huyo alianza kutapika sana na baada kuulizwa aliweka wazi kilichotokea ambapo baada ya watu kumfuata katika studio hiyo, alijaribu kukimbia bila mafanikio hivyo kukamatwa na wananchi.

“Tunashukuru wananchi kwa ushirikiano wao kwani wametupa taarifa na bado kwa juhudi zao wamemshikilia mtuhumiwa mpaka askari wakamkamata, kwa sababu alikua tayari anatoroka,” alisema.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nyerere lilipotokea tukio hilo, Yasin Husein alisema wakati wanamuhoji kijana huyo baada ya kumkamata alisema alishawishiwa na msanii mwenzie aitwaye Johari wakaenda kwa mganga, ambapo aliwapaka dawa na kuwataka walale pamoja wafanye mapenzi lakini wakimaliza wasioge na mwanaume huyo atafute mtoto mdogo wa kiume amnyonyeshe huo uume.

Alisema mtoto huyo amenyonyeshwa uume ambao pia ulitoka kufanya mapenzi usiku na kwa maelekezo kuwa akikamilisha hiyo shughuli  mafanikio yatakuwa tayari kwa hiyo sanaa yao ya uigizaji itakuwa.

“Huyu bwana tumeongea naye lakini kwenye mahojiano katuambia mambo ya ajabu na hovyo kabisa, kwamba mtu anataka afanikiwe badala ya kufanya kazi na kuomba Mungu, vitendo kama hivi hatuvikubali kwenye jamii yetu kabisa,” alisema.

Mbali na tukio hilo, Kamanda huyo alisema kuwa historia inaonyesha mtuhumiwa akiwa na umri wa miaka 15 amewahi kubaka mtoto na alipewa adhabu ambayo pia iliendana na umri wake wakati huo.

“Mwaka 2024 mtuhumiwa akiwa kata ya Mwinyi aliwahi kumbaka mtoto, kwa hiyo tunaendelea kumuhoji kujua lengo hasa lakini kujua kikundi chake anachofanya sanaa na njia zipi wanatumia,” alisema.

Sada Himidi mkazi wa Ipuli aliiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya watu wanaofanya ukatili kwa watoto kwa sababu inawaumiza sana watoto.

Husein Malukwi, mkazi wa Tabora alisema kila mmoja inabidi kuwa mlinzi wa mtoto kwenye jamii yake ili kudhibiti waharibifu wa watoto.

“Tunasema watoto ni hazina na Taifa la kesho sasa kama watakua wanalawitiwa na kufanyiwa kila aina ya matukio mabaya, hilo Taifa litakua la aina gani,” alisema na kuhoji Malukwi.