Sugu asimulia alivyovuka kiunzi cha ‘Team Mbowe, Team Lissu’-1

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amesema kwamba ingawa katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho alimuunga mkono Freeman Mbowe, katika maisha yake binafsi alikuwa rafiki zaidi wa Tundu Lissu tangu walipokuwa pamoja bungeni.

Mbunge huyo wa zamani wa Mbeya Mjini amekiri kuwa uchaguzi huo ulimweka katika wakati mgumu, akidokeza kilichomsaidia ni kutovuka mipaka ya ushabiki, jambo lililomfanya awe tayari kumpokea mshindi yeyote, akiamini ushindi wowote ni wa chama.

Sugu, katika uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa Chadema uliofanyika Januari 21 mwaka jana, alimuunga mkono Mbowe, aliyeshindwa kwa kupata kura 482 sawa na asilimia 48.3, dhidi ya kura 513 sawa na asilimia 51.5 alizopata mshindi Lissu.

Uchaguzi huo uliibua makundi mawili ndani ya chama hicho, kati ya wale waliomuunga mkono Mbowe, ambao wengi walihama na kwenda Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), huku waliokuwa wanamuunga mkono Lissu wakibaki ndani ya Chadema.

Sugu amesema hayo alipozungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Alivyoruka kiunzi cha Team-Mbowe, Lissu

Katika uchaguzi huo, Sugu amekiri alimuunga mkono Mbowe, ingawa katika maisha yake binafsi yeye ni rafiki zaidi wa Lissu.

“Of course (bila shaka), mimi nilikuwa kambi ya Mbowe, lakini sikuvuka mipaka yangu, nikijua kwamba hawa ni viongozi wetu. Sawa, mimi nilikuwa namuunga mkono Mbowe, lakini Lissu ni mwanangu zaidi kuliko Mbowe. Hata tukiwa Dodoma wakati ule mchana namuuliza bwana uko wapi twende nyumbani tukale ugali, uko wapi twende tukale Pizza, ni kaka yangu,” amesema.

Kwa sababu hiyo, amesema hata Mbowe aliposhindwa haikumsumbua wala kumkatisha tamaa, kwani aliamini ushindi wa Lissu ni wa Chadema.

Baada ya uchaguzi huo, amesema kwa nafasi yake anapaswa kufanya jambo kuhakikisha chama kinasonga, ndiyo maana ziara ya kampeni ya ‘No Reforms No Election’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) ilianzia katika kanda anayoiongoza.

“Chadema ipo imara kuliko kipindi chochote. Tunawaambia kila siku, hasa hawa wanaojaribu kuiuwa. Chadema ilishavuka kuwa chama cha viongozi, kwamba kwa sababu ya kiongozi fulani chama kinasimama, Chadema kipo kwenye mioyo ya Watanzania,” amesema.

Tunatokaje baada ya Oktoba 29

Oktoba 29 mwaka jana kulitokea maandamano yaliyozaa vurugu, kuharibu mali za watu binafsi na miundombinu ya umma. Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya kuchunguza kiini cha tatizo, inayotarajiwa kumaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, katika mahojiano maalumu aliwahi kutoa masharti ya chama kuingia kwenye maridhiano baada ya matukio hayo, akitaka wakosaji wawajibishwe, Lissu aachiwe huru, na chama kiweze kufanya shughuli za kisiasa.

Sugu yeye amependekeza njia ya kuliunganisha Taifa na kurudisha mshikamano baada ya matukio hayo, akitaka uwepo wa uwajibikaji, wakosaji wakiri na Lissu aachiwe huru.

“Tunahitaji uwajibikaji, tunahitaji watu wakiri. Turudi kwenye uhalisia na ukweli. Lissu sio mhaini, wamwachie mwenyekiti wetu. Chadema imepigwa kesi za kihuni ili kuizuia kufanya shughuli za siasa, waifungulie,” amesema.

Amesema ni vema mambo yazungumzwe hadharani, kama ni hasira iibuke na ishushwe, hatimaye iishe, jambo linaloweza kurudisha mshikamano wa Taifa.

“Tunawaambia kutoka hapa kwanza lazima Lissu atoke gerezani, Chadema ifunguliwe, kwa sababu huwezi kuongea na mtu mmoja mmoja kutoka kwenye chama ambacho umekifungia, atapata wapi baraka za kuja kuzungumza,” amesema.

Mei 31, 2022, Sugu aliadhimisha miaka 30 ya maisha yake ya muziki na kuzindua kitabu chake, tukio ambalo Rais Samia alialikwa na kuhudhuria kama mgeni rasmi.

Kutokana na tukio hilo, mwanasiasa huyo ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa muziki wa Bongoflava, amesema kuliibuka minong’ono kutoka miongoni mwa watu, wakihoji iweje amwalike Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, amesema alitaka kumsaidia Rais nje ya siasa kutimiza lengo la kuleta maridhiano.

Amesema kipindi anamwalika mkuu huyo wa nchi zilikuwa nyakati ambazo kiongozi huyo alikuwa amejikita katika harakati za kuviunganisha vyama na kujenga umoja.

“Nikaona tunaweza kumsaidia Rais kutimiza lengo lake la maridhiano, kwa hiyo nikaja na burudani, nikaalika mabalozi wote wa Magharibi na Afrika. Lile halikuwa tamasha la kawaida, ilikuwa tiba kwa Taifa lililotoka kwenye manung’uniko,” amesema.

Amesema kila mtu alihitajika kufanya jukumu lake kuhakikisha nchi inakuwa na mshikamano na umoja.

“Kwanini ilileta maneno baadaye ni kwa sababu kulishaanza kuwa na viashiria vya mabadiliko kutoka dhamira aliyokuwa nayo mkuu wa nchi wakati huo na wakati watu wanalalamika,” amesema.

 Katika kipindi hicho, Rais Samia alianzisha falsafa ya R4—majadiliano, maridhiano, mageuzi, na kujenga upya, akilenga kurejesha mshikamano kati ya viongozi na wananchi. Ni wakati huo, ndipo mkuu huyo wa nchi, aliruhusu mikutano ya vyama vya siasa iliyokuwa imezuiwa kwa takriban miaka sita.

Sugu amesema baada ya uchaguzi wa ndani wa Chadema na baadaye, amekuwa akiombwa na vyama mbalimbali vikubwa vya siasa ajiunge navyo, baadhi vikimuahidi ubunge.

Amesema amekuwa akiviambia vyama hivyo kwamba visijaribu kumshawishi kwa kumuahidi ubunge au nafasi nyingine, kwa kuwa yeye ameshavuka huko.

“Nilishakuwa mbunge miaka 10, mimi kama kurudi bungeni sasa hivi ni kwa ajili ya wananchi sio kwa ajili ya mimi binafsi, kwa hiyo siwezi kuwasaliti wananchi ambao wako na Chadema nikawe mbunge kupitia chama gani” amesema.

Mei 2024, Sugu aligombea uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, akishindana na Peter Msigwa, aliyekuwa kiongozi wa kanda hiyo kwa awamu mbili. Sugu alishinda kwa kupata kura 54, dhidi ya 52 za Msigwa.

Uchaguzi huo uliibua tuhuma za rushwa na malalamiko kutoka pande zote. Mwezi mmoja baadaye, Msigwa alihama Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kuhusu hilo, Sugu amekiri kulikuwepo vurugu za uchaguzi zilizokuwa chanzo cha mgawanyiko kati ya waliokuwa wanamuunga mkono yeye na wale wa Msigwa.

“Siku ya uchaguzi Sugu ndio akashinda, unajua kuna changamoto ya watu kunishusha hadhi sana yaani watu wanamchukulia Sugu mtu wa kawaida, lakini mimi naona ni sawa, hapohapo ndiyo natoboa katikati.

“Huwa siingii kwenye kitu bila kutathmini, kwa hiyo nikisema nakwenda kugombea ubunge huwa nimetathmini na nimejua kwamba nashindaje, nikikwambia nagombea uenyekiti wa Kanda nilikuwa naijua nguvu yangu,” amesema.

Amesema alikuwa na nguvu ndani ya Chadema hata kabla ya kuwa na cheo chochote, na wakati huo alikuwa katika jukwaa kuu.

Katika mahojiano hayo, amesema anaamini akishiriki uchaguzi katika Jimbo la Mbeya Mjini atashinda kama ilivyokuwa mwaka 2010 na 2015.

Imani yake hiyo, inatokana na kile alichoeleza, ni kawaida kwa ushindi wa wanasiasa unapungua kwa kadiri siku zinavyosogea, lakini kwake ilikuwa tofauti.

“Mimi nilishinda kwa kishindo mwaka 2010, lakini 2015 badala ya kushuka nikaongezeka mara mbili zaidi. Yaani kwenye uchaguzi wa kwanza nilishinda kwa kura zaidi ya 40,000 lakini kwenye uchaguzi uliofuata nikashinda kwa kura zaidi ya 100,000,” amesema.

Lakini, ushindi huo, amesema utatokea iwapo uchaguzi huo utakuwa katika mazingira ya haki na huru ingawa sio kwa asilimia 100.

“Sisi hatutaki haki ya asilimia 100 tunajua hawawezi kufanya, sisi tunataka tuachwe tupambane, usije na vifaru, njoo na pingu zako, virungu, kama unataka kuja na polisi, lakini usije na bunduki, vifaru, wanajeshi,” amesema.