Wizara Maji na matumizi ya teknolojia katika utatuzi wa changamoto

Na: Dk. Reubeni Lumbagala

Wiki ya Maji Kitaifa nchini Tanzania na Siku ya Maji Duniani imemalizika Machi 22, 2026. Imekuwa ni wiki nzuri kwani mijadala mbalimbali yenye tija kuhusiana na sekta ya maji imefanyika kwa mafanikio makubwa. Kutokana na umuhimu wa maji, serikali, mashirika, asasi na wananchi kwa ujumla katika Siku ya Maji Duniani, hujadili masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya maji kwa maendeleo.

Kimsingi, mijadala ya kuangazia mafanikio na changamoto za sekta ya maji inafanyika kwa madhumuni ya kuboresha hali ya usambazaji wa maji kwa wananchi na kuangalia namna maji yatakavyosaidia sekta nyingine kama kilimo, viwanda, mifugo, uvuvi, nishati, kutaja kwa uchache katika kukuza uchumi kwa maendeleo endelevu.

Wizara ya Maji imefanikiwa katika maeneo mengi. Mathalani, suala la usambazaji wa maji kwa wananchi ambapo maeneo ya mijini usambazaji wa maji umefikia asilimia 92.5 na vijijini asilimia 85.2. Wizara ya Maji imefanikiwa pia kutekeleza miradi mingi kama Mradi wa Miji 28. Ipo miradi ya zamani na mipya iliyokamilika na kuanza kazi, hali inayozidi kuimarisha upatikanaji wa maji nchini.

Serikali pia imejitahidi sana kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, shilingi trilioni 1.01 ziliidhinishwa, huku fedha nyingi zikielekezwa katika kugharamia miradi ya maendeleo ili tija ya upatikanaji wa maji ionekane. Mpango mkubwa wa kihistoria wa ujenzi wa Gridi ya Taifa ya Maji unaendelea vizuri.

Pamoja na mengi yaliyofanikiwa katika Wizara ya Maji, lakini zipo changamoto kadhaa zinazoikabili Wizara ya Maji ambapo baadhi ya changamoto hizo zitatatuliwa kikamilifu endapo matumizi ya teknolojia za kisasa yatapewa msukumo mkubwa.

Kimsingi, maendeleo ya sayansi na teknolojia yamekuwa msaada mkubwa wa kupunguza changamoto katika jamii na kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali, hivyo Wizara ya Maji haina budi kuendana na ulimwengu unavyokwenda kwa kutumia teknolojia katika utatuzi wa changamoto na kuongeza ufanisi wa kiutendaji.

Machi 19, 2026, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alipata fursa ya kuzindua Taarifa ya Utendajikazi wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2024/2025 katika Hoteli ya Cate Mjini Morogoro. Katika hotuba yake, Aweso alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili Wizara ya Maji ambazo utatuzi wake unategemea sana matumizi ya teknolojia za kisasa. Mosi, upotevu wa maji. Kwa hisia kali, Aweso alionyesha kusikitishwa kwake na upotevu wa maji ambao umegubikwa na wizi wa maji. Taarifa inaonyesha upotevu wa maji umeongezeka kutoka asilimia 36 mwaka 2023/2024 hadi asilimia 42.3 mwaka 2024/2025.

Upotevu wa maji unaikosesha Wizara ya Maji mapato lakini pia unawakosesha wananchi maji. Aweso alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, kuhakikisha kuwa Watendaji wa Mamlaka za Maji wanapimwa utendajikazi wao kupitia udhibiti wa upotevu wa maji katika maeneo yao. “Yapo baadhi ya maeneo mengine maji yanamwagika, mwananchi anatoa taarifa jamani maji yanamwagika huku, hakuna anayejali.

Katika Mamlaka zetu tuwe na taskforce (kikosikazi) cha kushughulikia udhibiti wa upotevu wa maji, pia tuishirikishe jamii katika hili bila hivyo tutakwama, na muhimu pia ni kuja na teknolojia yenye kuonyesha mvujo wa maji,” amesisitiza Aweso.

Changamoto nyingine ni malalamiko ya ankara za maji. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia kubambikiziwa ankra ya maji tofauti na matumizi halisi wanayotumia. Wanalalamika kutumia maji kidogo lakini ankara inayokuja ni kubwa. Wizara ya Maji imekuja na teknolojia ya mita janja za malipo ya kabla (prepaid water meter) ili wananchi walipe ankara kulingana na matumizi yao halisi bila uonevu wala upendeleo.

Mita za malipo ya kabla hutumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupitia mita zao za Lipa Umeme Kadri Utumiavyo (LUKU). Hivyo, mita za malipo ya kabla za maji zitaepusha malalamiko ya muda mrefu. Zoezi la kubadilisha mita za maji za zamani na kufunga mita mipya linaendelea huku lengo likiwa ni kuhakikisha watumiaji wote wanatumia mita za kisasa ili kumaliza kabisa malalamiko ya kubambikiziwa ankara za maji.

Sambamba na hilo, lipo pia suala la ulinzi wa miundombinu na vyanzo vya maji. Malengo ya kuwafikishia wananchi maji na kuyatumia maji katika shughuli za kimaendeleo hayataweza kufikiwa endapo hakutakuwa na mkakati madhubuti wa kutumia teknolojia ya kisasa katika ulinzi wa miundombinu na vyanzo vya maji. Wizara ya Maji inapaswa sasa kutekeleza mpango wa kutumia teknolojia ili kuwanasa wale wote wanaohujumu miundombinu ya maji na kuharibu vyanzo vya maji ili kuwa na uhakika wa maji katika shughuli za kimaendeleo.

Kwa kumalizia, wananchi tunalo jukumu kubwa kuhakikisha tunakuwa mabalozi wazuri wa kutunza mazingira ili kustawisha sekta ya maji. Uharibifu wa vyanzo vya maji na miundombinu yake ni adui mkubwa wa mipango ya maendeleo ndani ya Wizara ya Maji. Kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, Wizara ya Maji ina mchango mkubwa kufanikisha mipango mizuri iliyomo hasa katika kuinua uchumi na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati juu.

Si Wizara ya Maji pekee, hata wizara nyingine zinazo jukumu la kuhakikisha zinatumia teknolojia za kisasa katika programu zake ili kuongeza tija na ufanisi, hatimaye kusukuma ajenda za maendeleo kwa kasi inayotakiwa, kwani tunapaswa kukimbia badala ya kutembea katika kushughulikia masuala ya maendeleo kwa manufaa yetu sisi wenyewe.

Maoni: 0620 800 462.