Global Publishers
March 23, 2026
0 Comments
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Elie Mpanzu, ameongeza mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Simba , hatua inayoimarisha kikosi hicho kuelekea msimu ujao wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Mpanzu, ambaye amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Simba kutokana na uwezo wake wa kiufundi na mchango wake uwanjani, ameonesha nia ya kuendelea kuipa timu hiyo huduma yake baada ya makubaliano mapya kufikiwa kati yake na uongozi wa klabu.

Uamuzi wa kumbakisha mchezaji huyo umehusishwa na juhudi za uongozi wa Simba chini ya Rais wa klabu, Mohammed Dewji, ambaye ameendelea kusimamia mikakati ya kuimarisha kikosi kwa lengo la kuongeza ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya CAF.
Mashabiki wa Simba wamepokea kwa furaha taarifa hiyo, wakiamini kuwa kuendelea kuwepo kwa Mpanzu kutaleta nguvu zaidi katika safu ya ushambuliaji na kiungo, sambamba na kuongeza uzoefu ndani ya timu.
Kwa hatua hii, Simba inaendelea kujipanga kuhakikisha inakuwa na kikosi imara kitakachoweza kutimiza malengo yake ya kutwaa mataji na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.