Dar es Salaam. Wakati Serikali ikianza michakato ya uboreshaji wa Soko la Nguo na Vyakula Ilala Boma jijini Dar es Salaam, wafanyabiashara sokoni humo, wameanza kujihesabu na kupeana namba ili wasikose nafasi baada ya ukarabati.
Hofu ya wafanyabiashara hao, imetokana na yaliyotokea katika Soko la Kariakoo lililoungua Julai mwaka 2021, baada ya ukarabati, kuliibuka malalamiko ya baadhi ya waliokuwa wafanyabiashara kukosa nafasi, huku wasiokuwepo wakipewa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, lilipo soko hilo linalotarajiwa kukarabatiwa, Edward Mpogolo, amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa, hakutakuwa na atakayeachwa kwa kuwa ukarabati ukianza watashirikishwa kila hatua.
Mpango wa ukarabati wa soko hilo lililoanzishwa miaka ya 1970, unatarajiwa kufanywa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP). Hata hivyo, bado haijawekwa wazi kuwa, lini ukarabati huo utaanza rasmi.
Hatua ya wafanyabiashara hao kujihesabu, imeelezwa na Mwenyekiti wa soko hilo, Ally Mbiku, wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake.
Baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Ilala Boma wakiendelea na shughuli zao ndani ya soko hilo ambalo linatarajiwa kuboreshwa.
Wafanyabiashara wajipanga
Ili kuepuka mkanganyiko wakati wa kupisha ujenzi na kurudi, Mbiku, amesema wameamua kuanzia wiki ijayo wafanyabiashara watahesabiwa na kupewa namba ili kujuana na maeneo yao ya biashara.
Hilo, amesema litaambatana na kuwapiga picha wafanyabiashara hao na kuwaweka katika mfumo maalumu utakaowezesha utambuzi pale watakapotakiwa kurudi sokoni.
Ameeleza wameamua kufanya hivyo, baada ya kusikia tetesi kuwa soko hilo litafanyiwa ukarabati mwaka huu, hivyo wanajua watahamishwa kwa muda kupisha ujenzi.
“Hii itasaidia hata tutakapohamishwa katika maeneo mengine na baadaye soko kukamilika na kutakiwa kurejea kusiwe na watakaoachwa, kwani tumejifunza kwa yaliyotokea kwa wenzetu Soko Kuu la Kariakoo na masoko mengine kuwa na migogoro ya aina hii.
“Hivyo mamlaka ikileta orodha yao na sisi tutawaonyesha ya kwetu ili kila upande uridhike, lakini tukiwa na ushahidi wa kujitosheleza nani ni nani na alikuwa anakaa wapi,” amesema Mbiku.
Ameeleza kwa makadirio kwa sasa, soko hilo lina zaidi ya wafanyabiashara 6,000, idadi waliyoipata mwaka jana, ingawa anaamini wameongezeka kwa kuwa kuna wanaomaliza vyuo na shule wanakimbilia kujiajiri hapo.
Mbiku, amesema wakati wa ukarabati, angependa kuona wafanyabiashara hawahamishwi kwenda mbali ili kuepusha kuyumbisha mitaji na litakapokamilika wote warudishwe kuepuka mgogoro.
Mwenyekiti wa soko hilo, Ally Mbiku
Amependekeza ikitokea watahamishwa, wahamishiwe katika Soko la Wamachinga, akisema kutawafaa hasa wafanyabiashara wa bidhaa za nguo za mitumba.
Eneo lingine alilopendekeza wahamishiwe ni ulipo Uwanja wa Mpira wa Karume, ambao kwa muda mrefu hautumiki na Serikali inapoteza mapato.
Mfanyabiashara, Juma Msulau, amesema wakati soko likiwa katika mchakato huo wa kujengwa, ni vema wakaboreshewa mazingira ya barabara za kuingia.
“Huku sokoni kipindi hiki cha mvua bila kuvaa mabuti huwezi kuingia kutokana na miundombinu mibovu ya barabara, watujazie hata vifusi, kwani ukiacha wateja, wafanyabiashara wanapata tabu kuingia. Hata gari za taka zinakwama,” amesema.
Mfanyabiashara mwingine, Osimunda John, amesema mazingira ya sokoni humo ni magumu, hivyo likiboreshwa itakuwa vema, kwa kuwa wanalipa ushuru na Serikali inapata fedha.
Mamalishe, Magreth Chabai, amesema changamoto kwao ni udogo wa eneo lao la kazi, akisisitiza wakati wa maboresho wazingatiwe.
Mwenyekiti wa wauza mitumba, Norbert Msulau, amekiri miundombinu ya soko hilo imechakaa, hivyo Serikali haijafanya makosa kuamua kulikarabati.
Ameshauri soko litakalojengwa liwe rafiki kwa biashara zao, zionekane na lisiwe ghorofa refu, kwani wateja hawapendi kupanda juu.
Baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Ilala Boma wakiendelea na shughuli zao ndani ya soko hilo ambalo linatarajiwa kuboreshwa.
Akizungumzia hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amekiri mpango wa kuliboresha soko hilo na kwamba upo chini ya DMDP.
“Ni kweli kuna mpango wa kuboresha miundombinu ya soko la Ilala Boma, ambao upo chini ya mradi wa DMDP, hivyo kipindi ujenzi utakapoanza niwahakikishie wafanyabiashara watashirikishwa kila hatua na hakuna atakayeachwa hata pale litakapomilika,” amesema.
Alipoulizwa ni lini hasa ujenzi huo utaanza, Mpogolo amesema asingependa kuliongelea zaidi kwa kuwa lipo chini ya DMDP na watakapokuwa tayari, wafanyabiashara watashirikishwa kwa kila hatua.
Mpogolo, amesema soko hilo ndio kubwa zaidi ya yote katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lina bidhaa mchanganyiko, hivyo hata Serikali haitapenda kupoteza mapato yake kwa kutowarejesha wafanyabiashara waliokuwepo awali.
