Polisi Morogoro yachunguza vifo viwili ikiwemo mtoto aliyejinyonga

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linachunguza matukio mawili ya vifo yaliyotokea kwa nyakati tofauti, likiwemo la mwanaume aliyefariki dunia ghafla katika stendi ya mabasi ya Msamvu na mtoto wa miaka 12 anayedaiwa kujinyonga baada ya kukemewa na wazazi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 23, 2026 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio la kwanza lilitokea Machi 22, 2026 jioni katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani ya Msamvu, Manispaa ya Morogoro.

Kamanda Mkama amesema mwanaume aliyefariki ametambulika kwa jina la Reuben Masimba Chedeco (70), mkazi wa Chalinze mkoani Pwani, aliyefariki ghafla muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi akitokea Dar es Salaam kwenda Morogoro.

“Awali, marehemu alishuka salama, lakini alipokuwa akielekea kujisaidia, ghafla aliishiwa nguvu na kudondoka. Aliwahishwa hospitali ya mkoa kwa matibabu, lakini ilibainika kuwa tayari alikuwa amefariki kabla ya kufikishwa,” amesema Kamanda Mkama.

Kamanda huyo ameongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kusubiri ndugu kwa utambuzi na taratibu za mazishi.

Katika tukio la pili, Kamanda Mkama amesema Jeshi la Polisi linaendelea, pia, kuchunguza kifo cha Rajabu Ally Mohammed (12), mkazi wa Java, kilichotokea leo Machi 23, 2026 katika kitongoji cha Kaloleni, kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkama, mtoto huyo alikutwa amejinyonga nyuma ya nyumba yao kwa kutumia mkanda wa suruali, baada ya kudaiwa kukemewa na wazazi wake kufuatia tuhuma za kuhusika katika tukio la wizi.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha mtoto huyo alikemewa baada ya kukamatwa na wenzake wawili wakidaiwa kuvunja nyumba ya jirani. Inadaiwa baada ya tukio hilo alichukua uamuzi wa kujitoa uhai,” amesema.

Amesisitiza kuwa uchunguzi wa matukio yote mawili unaendelea, huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuepuka kutumia ukatili katika malezi ya watoto.

“Ni muhimu kutumia njia sahihi za malezi na mazungumzo, kwani vitendo vya ukatili vinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha,” amesema Kamanda Mkama.