SMZ kutumia teknolojia kuwanasa wanaokata misitu Zanzibar

Unguja. Kutokana na kasi ya ukataji misitu inayoendelea, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeandaa mpango wa kuanza kufuatilia na kudhibiti wanaokata misitu hiyo kwa njia ya kidijitali.

Hayo yamebainishwa leo Machi 23, 2026 wakati wa kuadhimisha siku ya upandaji miti duniani ambapo kitaifa kwa Zanzibar imefanyika katika Shehia ya Muyuni, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja kwa kupanda mikoko 2,500.

Kaulimbiu ya mwaka huu kwa Zanzibar inasema “misitu ya juu na mikoko ni uchumi endelevu, tuendelee kuitunza”.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali amesema licha ya faida nyingi za misitu lakini imekuwa ikikabiliana na changamoto nyingi zikiwemo za ukataji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii.

Wananchi na wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wakipanda miti ya mikoko katika pwani ya shehia ya Muyuni Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Ungujaikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya siku ya upandaji miti dunia.

“Changamoto kubwa ni ukataji misitu ya mikoko na sasa hivi imekuwa ni balaa hususani Ghuba ya Chwaka na Chakechake,” amesema.

Ameongeza kuwa licha ya kuwa na maji lakini watu wanavizia yanapotoka wanaingia kukata mikoko hiyo.

“Serikali ina mpango ambao kwa sasa tunaukamilisha kuwa na ulinzi wa kidijitali, mtu anapoingia popote pale tutakuwa tunamuona, kwa sasa kuna mtaalamu ambaye anatusaidia kila atakayeingia tunamuona na itakuwa rahisi kumdhibiti,” amesema mtaalamu huyo.

Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame amesema ipo haja ya kuendeleza ulinzi shirikishi wa misitu hiyo.

Amesema wanatarajia kupanda miti zaidi ya milioni tatu katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Katika ulinzi, Waziri Makame amesema kwa sasa Serikali inafanya marekebisho ya sheria ya misitu ya mwaka 2016 ili kuhakikisha inakuwa imara na kudhibiti changamoto hizo.

“Tunachokiomba sasa kwa jamii kuiendeleza misitu hii, hata wawekezaji wote ambao wameamua kuja kuwekeza eneo la misitu na sio jangwa, basi lazima wailinde na kuhifadhi misitu hii,” amesema.

Amesema kuna fursa nyingi za uwekezaji kwani zinasaidia katika ufugaji wa nyuki na kufuga kaa.

Katika kusisitiza suala hilo, Makame amesema: “Tunakuja na sheria ambayo itakuwa na mikakati madhubuti kuhakikisha tunalinda misitu na mikoko hii inatoa oksijeni safi kuliko miti yoyote.”

Amesema wageni wanaotoka maeneo mbalimbali duniani wanashangaa kuona miti hiyo, kwa hiyo kuna kila sababu kuitunza zaidi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Othman Maulid amesema katika mazingira ya misitu inachagiza utalii kwani watalii, mbali na kutalii lakini kutumia kama sehemu ya mapumziko.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame (kushoto), akiongoza wananchi na watumishi wa wizara hiyo kupanda mikoko katika pwani ya Shehia ya Muyuni Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya kupanda miti duniani. Picha na Jesse Mikofu

“Wakienda huko wanakuta hewa imebadilika lakini ukija huku wanakuta hewa safi,” amesema Maulid.

Jumuiya ya Usimamizi wa Misitu ya Jamii Zanzibar (Jumijaza) imesema wanaendeleza kutoa elimu na kuhakikisha jamii inajua umuhimu wa kuhifadhi na kulinda misitu

“Usimamizi wa misitu halina mjadala, tumejipanga kuimarisha bionuai na mbinu na kusaidia jamii na kuendeleza biashara ya hewa ukaa kupitia kamati za uhifadhi misitu,” amesema Khamis Haji.

Ndani ya kipindi cha miaka 15, jumuiya imeshirikiana na kamati za shehia 56 Unguja na Pemba katika kutunza na kusimamia rasilimali za asili.

Katika msimu huu wa mvua za masika Zanzibar imepanga kupanda miti 3.273 milioni, inayojumuisha ya matunda na viungo 2,117,458, misitu 637,173, minazi 16,200, mikarafuu 336,703 na mikoko 165,620.