Wakulima wahimizwa kutumia taarifa za TMA kuongeza tija

Mbeya. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ikiadhimisha siku ya hali ya hewa duniani, wakulima Nyanda za Juu Kusini wameipongeza mamlaka hiyo wakieleza utabiri wao umewasaidia kuendesha kilimo chao kwa tija huku jamii ikitakiwa kuzingatia ushauri unaotolewa.

Kila ifikapo Machi 23, TMA huungana na mamlaka nyingine za hali ya hewa duniani kusherekea siku hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 1950, ambapo Nyanda za Juu Kusini imeadhimisha siku hiyo ikitaja mafanikio makubwa ikiwamo uwekezaji, elimu na mabadiliko ya kisasa.

Wakizungumza leo Machi 23, 2026 katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Mbeya, baadhi ya wakulima wamesema utabiri wa hali ya hewa umewasaidia kuendana na wakati na kupangilia ratiba za misimu ya kilimo.

Pius Mkombe, mkazi wa Iringa amesema taarifa za hali ya hewa imewasaidia kujua ratiba za mvua na kujua ni mazao gani yanaweza kuendana na wakati husika, akiwaomba wananchi kuendelea kuzingatia ushauri wa TMA.

“Mfano, mwaka huu walisema mvua zitakuwa za wastani na tukajua ni mazao gani tulime na ndio maana mavuno kwa awamu ya kwanza yamekuwa ya tija, huku Bonde la Usongwe tunazingatia sana utabiri huu,” amesema Mkombe.

Kwa upande wake, Sarafina Mwaigaga, mkazi wa Kijiji cha Ikumbi amesema TMA imekuwa na msaada mkubwa katika kuwaandaa msimu wa kilimo, akiiomba kuendelea kutoa taarifa kwa wakati ili kusaidia jamii zaidi.

“Hata wananchi nao wazingatie ushauri unaotolewa na TMA kwa kuwa asilimia kubwa utabiri wao wa hali ya hewa umekuwa sahihi, tuendelee kuchukua tahadhari na hatua zaidi,” amesema Sarafina.

Kaimu Meneja wa TMA Nyanda za Juu Kusini, Isaya Kapakala amesema wakati wakiadhimisha siku hiyo, wanajivunia taarifa zilizo sahihi kwa jamii na mabadiliko ya utendaji kutoka mifumo ya zamani hadi kuwa kidijitali.

Amesema Serikali imefanya maboresho makubwa ikiwekeza zaidi ya Sh6 bilioni katika kufunga mitambo ya kisasa inayosaidia ufanisi mkubwa kwa wafanyakazi na Taifa kwa ujumla.

 “Tumejiandaa vizuri kutoa uelewa kwa jamii ili kuweza kufuatilia hali ya hewa kwa lengo la kupanga mipango na kuepuka majanga yanayosababishwa na hali ya hewa, tunajivunia kwa kutoa utabiri ulio sahihi na matokeo yake yanakuwa kweli,” amesema Kapakala.

Ameongeza kuwa kwa sasa mamlaka hiyo imepiga hatua zaidi kwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutumia mitambo ya kisasa baada ya Serikali kuamua kuwekeza gharama kubwa zaidi ya Sh6 bilioni.

Amesema ukanda huo unagusa kundi kubwa la wakulima, wavuvi na wasafiri kutoka ndani na nje, akieleza kuwa msingi mkubwa ni kuwezesha makundi hayo kufanya shughuli zao salama.

“Lipo janga kubwa la mabadiliko ya tabianchi, msingi wa kilimo, uvuvi na usafiri hivyo tusifanye mazoea, kazi yetu ni kupima na kutoa taarifa za utabiri ikiwamo ndege, hivyo kabla ya kupaa au kutua lazima rubani azingatie.

“Ndio maana muda mwingine ndege haitui, hivyo malalamiko ya baadhi ya abiria kuhusu ndege kutotua ni kwa ajili ya usalama wao, ndege haiwezi kutua kwa sababu ya kuweka usalama wa abiria” amesema.

Naye, fundi mitambo wa mamlaka hiyo, Hatibu Mpota amesema uwapo wa vifaa vya kisasa umesaidia ufanisi kutoka analojia kwenda kidijitali akibainisha kuwa hali hiyo imeondoa makosa ya kibinadamu kwenye mfumo.