Aliyehukumiwa jela miaka 30 kwa ubakaji, akata rufaa akwaa kisiki

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na mkazi wa Dar es Salaam, Sharif Tandila aliyekuwa akipinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka binti aliyekuwa anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kurasini.

Binti huyo aliyekuwa na umri wa miaka 15, alidaiwa kutoweka nyumbani kwao Mei 7 hadi Juni 23, 2022 ambapo baadaye alikutwa kwa mrufani aliyedai kukutana naye kwenye danguro, ambapo alimuhudumia mara tatu kisha wakakubaliana aache kazi hiyo na kwenda kuishi naye.

Majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Augustine Mwarija, Panterin Kente na Zainab Muruke waliotoa hukumu hiyo Machi 20, 2026 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Uamuzi huo ulianza kwa Mahakama kueleza kuwa wanachotakiwa kusuluhisha ni kama kumwokoa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 kutoka kwenye danguro na kuishi naye kama mke, kwa nia ya kumuoa ni utetezi dhidi ya ubakaji wa kisheria.

Katika uchambuzi wake, mahakama ilibainisha kuwa umri wa mwathiriwa ulithibitishwa ipasavyo kupitia ushahidi wa mama yake pamoja na cheti cha kuzaliwa kilichowasilishwa mahakamani.

Jaji Muruke amesema cheti hicho kilionyesha wazi kuwa mtoto huyo alizaliwa Juni 30, 2007, hivyo alikuwa na umri wa miaka 15 wakati wa tukio.

Mahakama pia ilieleza kuwa mrufani hakupinga ushahidi huo wakati wa kesi ya awali wala hakumuhoji shahidi kuhusu umri wake, jambo ambalo kisheria linaonekana kama kukubaliana na ushahidi uliotolewa.

Aidha, mahakama ilitupilia mbali hoja ya mrufani kuhusu kutofautiana kwa jina la mwathiriwa kati ya hati ya mashtaka na ushahidi wake, ikisema kuwa hiyo ilikuwa ni makosa madogo ya kiuandishi yasiyoathiri uhalali wa kesi.

Katika uamuzi wake, mahakama ilisisitiza kuwa sheria inalenga kulinda watoto dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, kwa kutambua kuwa watoto hawana uwezo wa kufanya uamuzi sahihi kuhusu masuala ya ngono kutokana na umri wao mdogo na ukuaji wao wa kimwili na kiakili.

Majaji walinukuu kifungu cha sheria kinachoeleza kuwa mwanaume atahesabika kufanya kosa la ubakaji endapo atafanya tendo la ndoa na msichana aliye chini ya miaka 18, bila kujali kama kulikuwa na ridhaa au la, isipokuwa tu kama msichana huyo ni mke wake halali mwenye umri unaokubalika kisheria.

Mahakama ilieleza wazi kuwa hoja ya mrufani kuwa alimwokoa mtoto huyo kutoka katika mazingira mabaya haiwezi kutumika kama kinga dhidi ya kosa la ubakaji, kwani kilicho muhimu ni umri wa muhusika na si mazingira aliyokutwa nayo.

“Kwa kuwa suala la kufanya tendo la ndoa halipingwi, na umri wa mwathiriwa umethibitishwa bila shaka, ni wazi kuwa kosa la ubakaji wa kisheria limetendeka,” ilieleza sehemu ya hukumu hiyo.

Kutokana na hoja hizo, Mahakama ya Rufani iliamua kuwa rufaa hiyo haina msingi wowote kisheria na hivyo kuitupilia mbali, huku ikithibitisha adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mrufani.

Awali, mrufani, alishtakiwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa makosa mawili ambayo ni ubakaji kinyume na kifungu cha 130 (1), 2 (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu na kumpa mimba mwanafunzi kinyume na kifungu cha 60 (1) (a) (2) cha Sheria ya Elimu Nambari 2 ya 2016.

Katika kesi hiyo Sharif alikutwa na hatia, kwa makosa yote mawili, hivyo akahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kila shtaka, hukumu ambazo ziliamriwa ziende sambamba.

Katika rufaa kwanza Mahakama Kuu, hatia ya shtaka la kumpa mimba mwanafunzi ilifutwa huku hatia ya shtaka la ubakaji, ikiendelea hivyo hivyo rufaa hii ya pili.

Katika kesi ya msingi, shahidi wa pili ambaye ni mama wa mwathiriwa wa tukio hilo alidai binti yake mwenye umri wa miaka 15, mwanafunzi wa kidato cha pili alitoweka kuanzia  Mei 7 hadi Juni 23, 2022.

Alidai Juni 2022, aliweza kumpata katika kituo cha mabasi cha Mtoni kwa Aziz Ally na alipoulizwa, alimtaja mrufani, kama mtu ambaye alikuwa akiishi naye kama mume na mke, ambapo binti huyo alipelekwa hospitali na kubainika kuwa alikuwa na ujauzito wa wiki mbili.

Alipokamatwa mrufani hakukana katika hatua yoyote wakati wa uchunguzi, hadi kesi hiyo iliposikilizwa na kusisitizia kuwa uhusiano wa kimapenzi ulikuwa wa makubaliano, na alikusudia kumuoa binti huyo ambaye alidai kumweleza kuwa alikuwa na umri wa miaka 22.

Katika rufaa ya sasa mrufani alikuwa na sababu tatu ikiwamo jina la ukoo la mwathiriwa wa tukio hilo kutofautiana na lile lililo kwenye hati ya mashtaka.

Majaji hao katika hukumu hiyo, waliangalia utetezi wa mrufani ambaye alikiri alikuwa akifanya ngono na mwathiriwa mara nyingi walipokuwa wakiishi nyumbani kwake kama mume na mke, ambapo sehemu ya utetezi wake amenukuliwa akieleza hayo.

“Sikumbaka mwathiriwa bali ni mpenzi wangu na tulipanga kuoana. Nakumbuka mara ya kwanza nilikutana na mwathiriwa kwenye danguro na amenihudumia mara tatu kabla hatujakubaliana kuacha biashara hiyo isiyo ya maadili na kuja nyumbani kwangu kukaa nami.

“Kufuatia makubaliano hayo, mwathiriwa alikuja kukaa nami na alikaa kwa wiki mbili tu. Baada ya hapo aliugua, hivyo akaniambia kwamba anaenda hospitalini, akiwa huko alinihitaji niende kulipia gharama za matibabu. Kufuatia simu hiyo nilienda hospitalini ambapo nilikamatwa na polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Maturubai ambapo niliarifiwa kwamba nilikuwa nikikabiliwa na kosa la ubakaji na kumpa mimba mwanafunzi.

“Kuhusu ujauzito ninachoweza kusema ni kwamba mwathiriwa hakubakwa na hana mimba. Mwathiriwa alikuwa kwenye danguro kwa hivyo ilikuwa vigumu kwangu kutambua kwamba alikuwa mtoto chini ya umri wa miaka 18. Ninachoweza kusema ni kwamba mwathiriwa alikuwa kwenye danguro na alikubali kufanya ngono,” alinukuliwa Sharif kwenye utetezi wake.