SERIKALI ya Tanzania imesema imejipanga kuendeleza sekta ya michezo nchini, hususan mpira wa kikapu, kufuatia hatua ya taifa kuandika historia kwa kushiriki mashindano ya Afrika (BAL) kwa mara ya kwanza ikiwakilishwa na Dar City ambayo imebeba matumaini ya kufanya vizuri.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wakati wa kuiaga timu ya mpira wa kikapu ya Dar City, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema mafanikio hayo ni chachu kwa vijana kuacha dhana kuwa mpira wa kikapu ni mchezo wa burudani au wa watu matajiri pekee, na badala yake kuuona kama fursa ya ajira na maendeleo ya kiuchumi.
Alisema serikali ina imani kuwa Tanzania ina uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuweka historia itakayokumbukwa na vizazi vijavyo. Dar City imeondoka nchini jana kuelekea Afrika Kusini kushiriki michuano ya sita ya Ligi ya Afrika ‘BAL’ ambayo inatarajia kuanza Machi 27, mwaka huu jijini Pretoria ambapo pia ameikabidhi bendera ya taifa.
Makonda ameeleza kuwa mafanikio ya timu za soka za Simba na Yanga katika mashindano ya Afrika yamefungua milango kwa timu nyingine za Tanzania kujitokeza kimataifa, akihimiza pia timu za mpira wa kikapu kuiga mfano huo.
Aidha, alisema serikali imeanza juhudi za kuboresha miundombinu ya michezo, ikiwa ni pamoja na mpango wa kujenga viwanja vya kisasa vya mpira wa kikapu. Alibainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam tayari umetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaokidhi viwango vya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Makonda amewataka wadau mbalimbali, ikiwemo taasisi za umma, makampuni binafsi na mashirika ya kifedha, kujitokeza kuanzisha na kudhamini timu za michezo ili kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha ushindani wa ligi za ndani.
Alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika michezo kama sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufikia tamati Aprili 5, mwaka huu, Dar City itacheza dhidi ya Johannesburg Giants ya Afrika Kusini (Machi 27), Nairobi City Thunder ya Kenya (Machi 28), Al Ahly ya Libya (Machi 31), Petro De Luanda ya Angola (Aprili 3) na RSSB Tigers ya Rwanda (Aprili 4).