Ndege zafanya safari za Dubai zikiwa tupu, sababu yatajwa

Safari za ndege kuelekea Dubai zimeonekana zikiwa na safu za viti tupu huku hofu kuhusu usalama wa safari za anga ikiongezeka kufuatia vita vya Iran.

Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, takribani ndege 39 za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai zilikuwa zimetua au kuondoka ndani ya dakika tano tu baada ya kutolewa kwa onyo la mashambulizi ya makombora wakati wa mzozo huo.

Hali kama hiyo iliripotiwa pia katika uwanja wa ndege wa Abu Dhabi, ambapo ndege sita zilihusika, pamoja na 12 katika uwanja wa ndege wa Sharjah.

Aidha, takribani ndege tano zilizokuwa zimeegeshwa katika viwanja vya ndege Mashariki ya Kati ziligongwa na makombora ya Iran huku mashambulizi ya mara kwa mara yakitikisa eneo hilo.

Picha na video zilizosambazwa mitandaoni zimeonyesha safu za viti tupu ndani ya ndege zinazoelekea Dubai, huku mmoja akiandika: “Sijawahi kuona ndege ya Emirates ikiwa tupu namna hii.”

Jumatatu iliyopita, Uwanja wa Ndege wa Dubai ulifungwa kwa muda baada ya droni ya Iran kulipua tanki la mafuta na kusababisha moto mkubwa.

Safari za ndege zilielekezwa kwingine na barabara zinazoelekea uwanjani kufungwa, huku moshi mzito mweusi ukionekana kutoka umbali wa kilomita kadhaa.

Ndege za Emirates kutoka maeneo ya mbali kama Melbourne, Sydney na Thiruvananthapuram zililazimika kurejea zilipotoka baada ya kufungwa kwa uwanja huo.

Vilevile, safari kutoka London (Heathrow), Edinburgh, Manchester na Dublin nazo zilirejeshwa zilikotoka.

Takribani droni mbili zilishambulia uwanja huo, na kwa saa kadhaa shirika la Emirates liliwashauri abiria wasisafiri, huku baadhi ya safari zikielekezwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Dubai, kusitishwa kwa safari hizo kulikuwa hatua ya tahadhari kulinda usalama wa abiria na wafanyakazi baada ya shambulio lililotokea saa 10 alfajiri kwa saa za huko.

Hata hivyo, mamlaka zilihakikishia umma kuwa shambulizi hilo lilisababisha uharibifu mdogo na hakuna majeruhi, zikilitaja kama tukio la droni.

Wiki iliyopita, mabaki ya makombora matatu ya masafa marefu yalizigonga ndege tatu binafsi katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion Airport.

Ndege nyingine mbili zilizogongwa zikiwa zimeegeshwa ni Airbus A380 ya Emirates na Airbus A321 ya Saudia, zote zikiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai mwanzoni mwa mzozo.

Licha ya hatari inayoendelea ya mashambulizi ya makombora na droni, mashirika ya ndege Mashariki ya Kati yameanza kurejesha mamia ya safari kila siku.

Takwimu kutoka Flightradar24 zinaonyesha kuwa katika wiki mbili zilizopita, Emirates imekuwa ikiendesha takribani safari 300 kwa siku sawa na asilimia 60 ya uwezo wake kabla ya vita.

Kwa kushirikiana na mashirika kama Etihad Airways, Flydubai na Air Arabia, kampuni za UAE zimeendesha zaidi ya safari 11,000 tangu vita vilipoanza.

Ili kupunguza hatari, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeweka njia maalumu za anga kwa dharura na kupeleka ndege za kivita kulinda safari za kiraia.

Msemaji wa Etihad amesema: “Hatufanyi safari yoyote bila kuhakikisha imepimwa na kuthibitishwa kuwa salama.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Uwanja wa Ndege wa Dubai, Paul Griffiths, amenukuliwa na CNN akisema kuwa uwezo wa kugundua na kukabiliana na vitisho umekuwa mzuri na wa haraka.

Wakati huohuo, Daily Mail limeripoti kwamba mashirika ya ndege ya kigeni kama British Airways yamesitisha safari zote kuelekea Dubai hadi majira ya kiangazi, yakitaja hali ya kutotabirika na kutokuwa thabiti kwa anga.

Shirika hilo pia limesitisha safari kuelekea Amman, Bahrain na Tel Aviv hadi baada ya Mei 31.

Safari za kuelekea Doha zimesimamishwa hadi mwisho wa Aprili, huku zile za Abu Dhabi zikisitishwa hadi baadaye mwaka huu.

Zaidi ya Waingereza 63,000 wamerudi nyumbani kutoka UAE tangu kuanza kwa mzozo huo, kwa mujibu wa takwimu za serikali.

Haya yanajiri huku UAE ikijaribu kupunguza uzito wa hali halisi, ikichukua hatua kali kudhibiti usambazaji wa video za vita mtandaoni.

Mamlaka zimekaza sheria dhidi ya machapisho yanayoonyesha makombora, droni au mashambulizi, kwa lengo la kulinda taswira ya nchi kama eneo salama.

Maofisa wa Dubai wamekuwa wakiwaambia wananchi kuwa milipuko mikubwa angani ni sauti ya usalama, wakirejelea hatua za mifumo ya ulinzi wa anga.

Ijumaa, polisi wa Abu Dhabi walitangaza kuwakamata zaidi ya watu 100 kwa kurekodi na kusambaza taarifa zisizo sahihi mitandaoni.

Katika taarifa, walieleza kuwa watu 109 wa mataifa mbalimbali walikamatwa kwa kusambaza habari potofu, baadhi yao wakieneza taarifa zinazopotosha.

Vitendo hivyo, walionya, vinaweza kuchochea hofu na kusambaza uvumi katika jamii.

Mwanasheria Mkuu wa UAE pia ameagiza kukamatwa kwa watu 35 hadi sasa kwa kuchapisha taarifa zisizo sahihi, kurekodi au kusambaza picha za vita, au kusifu mataifa pinzani.

Hatua hiyo inafuatia kukamatwa kwa mtalii mmoja wa Ulaya mjini Dubai baada ya kuchapisha picha ya hoteli ya Fairmont The Palm ikiwa inawaka moto kufuatia shambulizi la droni la Iran.

Mwanaume huyo, baba wa watoto watatu, alikamatwa Machi 9,2026 na hajulikani alipo hadi sasa.

Wiki iliyotangulia, Mwingereza mwenye umri wa miaka 60 alishtakiwa pamoja na watu wengine 21 chini ya sheria za uhalifu wa mtandao kutokana na video na machapisho kuhusu mashambulizi ya makombora.

Anadaiwa kusambaza taarifa au propaganda zinazoweza kuvuruga usalama wa umma, ingawa alidai alifuta video hiyo baada ya kuombwa na hakukuwa na nia mbaya.

Hatua kama hizo pia zimechukuliwa katika nchi nyingine za Ghuba, huku Iran ikiendelea kulenga si tu mali za Marekani bali pia miundombinu ya kiraia kama viwanja vya ndege, maeneo ya makazi, pamoja na vituo vya mafuta na gesi.

Nchini Qatar, zaidi ya watu 300 wamekamatwa kwa kusambaza picha na taarifa zinazodaiwa kupotosha, huku Bahrain na Kuwait nazo zikichukua hatua kama hizo.