UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umetangaza kumrudisha ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Abdihamid Moallin ili kusaidiana na Pedro Goncalves.
Uamuzi huo umefanyika leo Jumatatu Machi 23, 2026 baada ya viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na Rais, Hersi Said kukutana na benchi la ufundi la Yanga chini ya Pedro na kuona kuna ulazima wa maboresho hayo.
Katika kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya Klabu ya Yanga yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam, Pedro aliongozana na msaidizi wake, Matthew Silva na Fernando Pereira ambaye ni kocha wa makipa.
Katika taarifa iliyotolewa na Yanga leo Machi 23, 2026, imesema uongozi umegundua kuna changamoto ya kiufundi inayofanya timu icheze aina tofauti na ile ambayo imezoeleka na kuendana na wachezaji walio ndani ya kikosi hicho.
“Changamoto hii ya kiufundi imekuwa sababu ya kuifanya timu kupata wakati mgumu kupata matokeo mazuri na kucheza vizuri pia kwenye baadhi ya michezo ya Ligi Kuu.
“Hivyo, katika kuitatua changamoto hii, Uongozi wa Young Africans Sports Club umefikia uamuzi wa kumuongeza kwenye benchi la ufundi, Kocha Abdihamid Moalin kama Kocha Msaidizi wa Kocha Pedro Goncalves,” imesema taarifa hiyo.
Moalin amewahi kuhudumu Yanga kama Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Msaidizi katika vipindi tofauti msimu uliopita 2024-2025 chini ya Kocha Sead Ramovic na Miloud Hamdi na kupata mafanikio ya kushinda Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Kombe la Muungano 2025.
“Uongozi wa Young Africans SC unamkaribisha Kocha Moalin na kumtakia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya kwa kushirikiana na makocha wengine ndani ya kikosi chetu,” imebainisha taarifa hiyo.
Wakati maboresho hayo ya benchi la ufundi ndani ya Yanga yakifanyika, takwimu zinaonesha timu hiyo katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara imemaliza ikiwa kileleni mwa msimamo huku ikicheza mechi 15, ikishinda 11 na sare tano, haijapoteza, ikifunga mabao 32 na kuruhusu matatu, ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi na ikiruhusu machache zaidi.
Licha ya kuongoza huko, uongozi wa Yanga umebainisha mambo makuu mawili nje ya ile ya kiufundi ambayo ni ratiba na majeruhi ikiyataja ni sehemu ya yaliyochangia kutopata matokeo mazuri kwa baadhi ya mechi kufuatia kupokea ripoti iliyowasilishwa na Pedro katika kikao hicho cha leo kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Yanga ambapo mbali na Hersi, alikuwepo Makamu wa Rais, Arafat Haji, Rodgers Gumbo na Munir Said ambao ni wajumbe wa kamati ya utendaji.
“Baada ya kuipitia kwa kina ripoti hiyo ya benchi la ufundi, uongozi umebaini changamoto kadhaa zilizoisumbua timu katika mzunguko wa kwanza wa ligi,” imesema taarifa hiyo ya Yanga.
“Ndani ya siku 21, kikosi chetu kimecheza michezo saba mfululizo, michezo sita ya Ligi Kuu na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho la CRDB. Ratiba hii pia ilijumlisha na safari ya umbali wa Kilomita 4,462 kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mechi za ugenini. Uongozi unaamini safari hizi na ratiba kubana kulipunguza ufanisi wa wachezaji kutokana na uchovu uliopatikana.
“Mpaka sasa, timu yetu ina wachezaji nane muhimu ambao wamepata majeraha tofauti tofauti yaliowapelekea kukosa michezo. Khomein Aboubakar, Clement Mzize, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Chadrack Boka, Edmund John, Prince Dube na Laurindo Maria ‘Depu’. Wachezaji watatu kwenye orodha hii wamepata majeraha yatakayowaweka nje mpaka mwisho wa msimu.”
Wachezaji ambao wanatajwa kukosekana hadi mwisho wa msimu ni Mzize, Khomein na Job ambao wote wanasumbuliwa na majeraha ya goti.