Wazazi wanavyoweza kudhibiti WhatsApp za watoto wao

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha usalama wa watoto mitandaoni, Kampuni ya teknolojia ya Meta Platforms, inayomiliki programu ya WhatsApp, imetangaza kuanzisha mfumo mpya wa akaunti zinazodhibitiwa na wazazi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 13.

Tangazo hilo lililotolewa Machi 11, 2026, linakuja wakati dunia ikishuhudia ongezeko la wasiwasi kuhusu athari za mitandao ya kijamii na programu za mawasiliano kwa afya ya akili na usalama wa watoto.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, akaunti hizo mpya zitakuwa na mipaka maalumu ikiwemo uwezo wa kutuma ujumbe na kupiga simu pekee, huku vipengele vingine vikidhibitiwa kwa ukaribu na wazazi au walezi.

Mzazi au mlezi atasimamia akaunti ya mtoto, akipewa mamlaka ya kuamua nani anaweza kuwasiliana na mtoto, pamoja na makundi gani anaweza kujiunga nayo. Pia, wazazi wataweza kukagua maombi ya ujumbe kutoka kwa watu wasiowajua na kusimamia faragha ya akaunti.

“Tumepokea maoni mengi kutoka kwa wazazi wanaotaka huduma salama ya mawasiliano kwa watoto wao wadogo. Akaunti hizi zimewekewa mipangilio madhubuti ya awali pamoja na zana za udhibiti wa wazazi,” ilieleza sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo kupitia blogu yake rasmi.

Ili kuanzisha akaunti hiyo, mzazi atalazimika kuwa na simu yake pamoja na simu ya mtoto, licha ya udhibiti huo, kampuni imeeleza kuwa mazungumzo yote yataendelea kuwa ya siri na kulindwa kwa teknolojia ya usimbaji fiche (end-to-end encryption), jambo linalomaanisha kuwa hakuna mtu mwingine hata WhatsApp yenyewe anayoweza kuona au kusikiliza mawasiliano hayo.

Hata hivyo, hatua hiyo inafuatia mwelekeo wa baadhi ya nchi kuanza kuweka sheria kali zaidi kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto. Mfano hai ni Australia, ambayo mwaka uliopita ilipitisha marufuku ya matumizi ya mitandao ya kijamii kwa vijana, ikieleza hofu kuhusu athari za kiafya na kisaikolojia.

Mzazi Dorice Kimaro kutoka mkoani Kilimanjaro anasema: “Kiukweli itakuwa jambo la msingi akaunti hizi zikianza kutumika maana kama mimi wanangu wanapenda kutumia simu sana na nashindwa namna ya kuwadhibiti.”

“Huyu mkubwa wa miaka 17, anatumia simu na anatumia WhatsApp nafikiri itakuwa vizuri nikianza kufuatilia mienendo yake kupitia hizo akaunti,” anasema.

Mlezi Anitha Ludovick anayelea mtoto wa dada yake binti wa miaka 16 anasema watoto wa siku hizi ni tofauti na zamani akijitolea mfano kwa kusema hakukuwa na matumizi ya simu.

“Unajua watoto wanaona mengi mitandaoni natamani kila mtandao ungekuwa na udhibiti kama hivi unavyoniambia. Huyu mtoto anachati na wenziye na mara nyingi wanachati kwenye magrupu yao ya shuleni.”

“Haitoshi, lakini lazima nifuatilie anawasailiana na kina nani wapya kwa sababu sasa hivi mambo sio ya kuyaamini sana,” anasema Anitha.

Akaunti hizo zitaunganishwa moja kwa moja na kifaa cha mzazi au mlezi, ambapo uthibitisho wa akaunti utafanyika kwa kutumia msimbo wa QR, hatua inayolenga kuhakikisha mtoto hawezi kujisajili bila ridhaa ya mzazi.

Mbali na kudhibiti nani anaweza kuwasiliana na mtoto, wazazi watapokea taarifa za papo kwa papo (alerts) pindi mtoto anapofanya mabadiliko muhimu kama kuongeza au kuzuia mawasiliano, kuripoti akaunti, au kupokea ujumbe kutoka kwa watu asiowajua.

Katika maboresho hayo, wazazi pia wanaweza kuwasha taarifa za ziada zitakazowaarifu pale mtoto: anapobadilisha jina au picha ya wasifu, anapojiunga au kuondoka kwenye kundi, anapopokea maombi mapya ya mazungumzo na anapofuta mawasiliano au mazungumzo.

Mipangilio yote inalindwa kwa namba ya siri ya tarakimu sita (PIN) inayowekwa na mzazi, hivyo kuongeza kiwango cha usalama.

Tofauti na akaunti za kawaida, akaunti hizi hazitakuwa na matangazo yoyote, na pia zitanyimwa baadhi ya huduma kama Meta AI, ‘Status’ na ‘Channels’, hatua inayolenga kupunguza mwingiliano usio wa lazima kwa watoto.

Aidha, watoto watakapopokea ujumbe kutoka kwa mtu asiye kwenye orodha yao ya mawasiliano, wataonyeshwa taarifa maalumu zinazoeleza chanzo cha ujumbe huo, ikiwemo nchi ya mtumaji na kama wana makundi ya pamoja. Picha kutoka kwa watu wasiowajua pia zitafichwa (blurred).

Jinsi ya kufungua akaunti

Ingawa huduma hii bado inaendelea kutolewa taratibu, hivyo huenda isipatikane katika maeneo yote kwa sasa. Akaunti hizi zinawalenga watoto walio chini ya miaka 13 (au chini ya umri unaoruhusiwa kisheria katika nchi husika), na lazima zisimamiwe na mzazi au mlezi mwenye umri wa miaka 18 au zaidi.

Kwanza unapaswa kupakua WhatsApp kwenye simu ya mtoto, chagua lugha kisha bonyeza Kubali na Endelea, chagua akaunti ya mzazi, bonyeza Chaguo zaidi (More options).

Chagua Create a parent-managed account, sajili na thibitisha namba ya simu ya mtoto, weka tarehe ya kuzaliwa ya mtoto na kuthibitisha umri, unganisha na akaunti ya mzazi kwa bonyeza continue ili kuunganisha akaunti.

Tumia simu ya mzazi ku-scan na QR code iliyo kwenye simu ya mtoto, ambapo mzazi utapaswa kuthibitisha wewe ni mtu mzima, halafu tengeneza PIN ya tarakimu sita ya mzazi, PIN hii itatumika kudhibiti mipangilio ya mtoto hakikisha usimpe mtoto PIN hii. Mwisho kamilisha usajili kwa kuweka PIN kwenye simu ya mtoto, bonyeza continue na sasa akaunti ya mtoto itakuwa tayari kutumika.

Unapaswa kujua PIN ya mzazi ndiyo ufunguo wa udhibiti wote, mtoto ataweza kuweka jina na picha ya wasifu, akaunti hii inamwezesha mzazi kusimamia mawasiliano na faragha,

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa kitengo cha AI na Cloud kutoka Dynatech Solutions Limited, Mhandisi Noel Henjewele anasema kwanza hatua hiyo ina mtazamo wa kiusalama ambapo ina umuhimu kwa faragha ya watoto.

“Kwa muda mrefu, watoto wamekuwa wakitumia mitandao ambayo haikuundwa kwa ajili yao. Mfumo wa QR Code unampa mzazi mamlaka kamili ya ‘mlango wa kuingilia’ (gatekeeping), jambo ambalo ni muhimu katika kumlinda mtoto na maudhui yasiyofaa au watu baki,” anasema.

Henjewele anasema ingawa udhibiti ni muhimu, ni lazima kuwe na uwiano. Maoni yangu ni kwamba teknolojia hii isitumike kama kuwachunguza, bali kama chombo cha kumfundisha mtoto uungwana wa kidijitali.

“Mzazi kuona anachofanya mtoto siyo tu kumchunguza, bali ni kumpa mwongozo wa jinsi ya kuishi kwenye ulimwengu wa kidijitali,” anasema.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa uzinduzi wa akaunti hizi utaanza kutekelezwa taratibu katika maeneo mbalimbali duniani katika miezi ijayo, huku ikiendelea kupokea maoni ya watumiaji ili kuboresha zaidi huduma hiyo, kutoa mazingira salama kwa watoto kuanza kutumia teknolojia ya mawasiliano chini ya uangalizi wa wazazi.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya teknolojia wanaeleza kuwa mafanikio ya hatua hiyo yatategemea kwa kiasi kikubwa uelewa na ushiriki wa wazazi katika kusimamia matumizi ya watoto wao mtandaoni.